WAZIRI wa nishati Medard Kalemani ameweka jiwe la msingi kla ujenzi wa kituo cha kupozea umeme ambacho kitajengwa na wataalam wa ndani kwa jumla ya shilingi bilioni 75 fedha za ndani mpaka kukamilika huku akilitaka shirika la ugavi wa umeme nchini (TANESCO) kuanza ujenzi wa kituo hicho mara moja.
Kituo hicho kitajengwa eneo la Imalilo mjini Bariadi mkoani Simiyu ambacho kitazalisha Megawati 100 huku mahitaji ya mkoa huu yakiwa ni Megawati 12 na ujenzi utafanywa na TANESCO kupitia wataalamu wake wa ndani huku akiwataka kujenga kwa ufanisi wa hali ya juu.
Dkt Kalemani ameyasema hayo leo huku akiongeza kuwa mradi huo ni mkubwa na kilovolti 220 ambapo utazalisha umeme mkubwa utakaotosha kwa matumizi ya viwanda vikubwa, vya kati na vidogo na hatimaye kukidhi mahitaji ya mkoa wa Simiyu.
"ujenzi wa mradi huu ni miezi 12 lakini nataka ukamilike kwa muda na si lazima itimie miezi kumi na mbili hata miezi tisa sawa ,mradi huu utachochea shughuli za uchumi na umeme utasambaa vijijini na utatosheleza mahitaji ya mkoa...wananchi wanaozunguka mradi huo niwatake kuwa wasimamizi kwa kuulinda na kuutunza lakini TANESCO mtoe kipaumbele cha ajira za kawaida kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo kwenye shughuli za ujenzi" alisema Dkt Kalemani.
Awali mkurugenzi mtendaji wa TANESCO dkt Tito Mwinuka amesema mradi huo utakapokamilika unatarajiwa kufungua fursa mbalimbali za maendeleo ya uchumi na uwekezaji wa viwanda mkoani hapa na tayari wameshafanya uthamini wa ekari 15.5 zenye thamani ya shilingi milioni arobaini na sita laki saba elfu thelathini na moja mia moja hamsini (46,731,150.00)
Akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Simiyu, mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga amesema kitendo cha umeme kufika maeneo mengi mkoani hapo kitakuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi na kitasaidia kuondoka changamoto ya kukatika mara kwa mara kwa umeme.
Martin Mata ni mkazi wa Imalilo amesema wamepokea ujio wa kituo hicho kwa mikono miwili na kuahidi kushirikiana na wananchi wenzie kukilinda.
0 comments:
Post a Comment