Wednesday, March 3, 2021

CHOROKO ZILIZONUNULIWA NJE YA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI ZIPELEKWE GHALA KUU: RAS SIMIYU

Wafanyabiashara wa choroko mkoani Simiyu wametakiwa kuwasilisha choroko zote zilizokusanywa kutoka kwa wakulima nje ya utaratibu wa mfumo wa stakabadhi ghalani na kuzipeleka katika ghala kuu kwa ajili ya kuingia katika utaratibu wa mauzo kwa njia ya mnada. 

Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga katika kikao chake na baadhi ya viongozi, watendaji na baadhi ya wafanyabiashara wa choroko, kilichofanyika jana Mjini Bariadi. 

"Mfumo unaotakiwa kufuatwa katika ununuzi wa choroko kwa manufaa ya mkulima kupata bei nzuri ni mfumo wa stakabadhi ghalani, wanaosimamia mfumo huu wahakikishe kwamba mwongozo huu unazingatiwa kwenye malipo ya wakulima ambao unawataka kufanya malipo kwa wakulima saa 48 baada ya mnada kufanyika," alisema Mmbaga. 

Katika hatua nyingine Mmbaga amezitaka Halmashauri zote mkoani hapa kuimarisha usimamizi na kuhakikisha Wafanyabiashara na wote wanaohusika na biashara ya choroko kulipa kodi na tozo zote zilizoainishwa katika mwongozo kutoka kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, huku akisisitiza wadau wote kuzingatia mwongozo huo ili kuepuka hasara isiyo ya lazima. 

Ameongeza kuwa mwongozo wa mfumo wa stakabadhi ghalani usimamiwe ili wadau wa zao la korosho wakiwemo wakulima na wanunuzi kila mmoja apate stahili zake na kubainisha kuwa watakaokiuka watakuna na mkono wa sheria.

 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Itilima, Bi. Elizabeth Gumbo amesema wao kama watekelezaji maelekezo ya ununuzi wa choroko yaliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa, Bi. Miriam Mmbaga yanatekelezwa kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na kuwaasa wafanyabiashara kutokiuka sheria na mwongozo huo kwa kuwa watakapokiuka watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria..

 

Naye Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Simiyu, Bw. Ibrahim Kadudu amesema umuhimu wa utaratibu huu utamnufaisha mkulima katika bei ambapo badala ya choroko kununuliwa kwa kwa bei holela na ya kificho lakini kupitia mfumo huu wakulima watalipwa kwa bei ya ushindani ambayo kwa sasa kuwa mnada uliofanyika Februari 25, 2021 katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga bei ilikuwa shilingi 1650. 

Ameongeza kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani utaisaidia Serikali kupata takwimu sahihi zitakazosaidia katika mipango ya kilimo kwa kuwa wakulima watakuwa wakipeleka choroko zao kwenye AMCOS kabla ya kuzipeleka katika maghala makuu kusubiri mnada hivyo takwimu za wakulima na mile walichozalisha kitapatikana kwa usahihi na kwa urahisi. 

Mfumo huu pia utazisaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa kukusanya mapatokwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakisafirisha choroko kwa njia za panya na kukwepa kulipa ushuru na tozo zilizowekwa kisheria.

MWISHO

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga akizungumza na baadhi ya viongozi, watendaji na baadhi ya wafanyabiashara wa choroko, kilichofanyika jana Februari 27, 2021 Mjini Bariadi.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga akizungumza na baadhi ya viongozi, watendaji na baadhi ya wafanyabiashara wa choroko, kilichofanyika jana Februari 27, 2021 Mjini Bariadi.

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika akitoa ufafanuzi wa jambo katika kikao cha Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga (kulia) na baadhi ya viongozi, watendaji na baadhi ya wafanyabiashara wa choroko, kilichofanyika jana Februari 27, 2021 Mjini Bariadi.

 

 

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!