Takribani kilo 145,000 za zao la choroko mkoani Simiyu zimeuzwa kupitia mnada uliofanyika kwa mara ya kwanza katika ghala lililopo kiwanda cha zamani cha kuchambua pamba cha Sola wilayani Maswa, ambapo kilo moja ya choroko imeuzwa kwa shilingi 1578 kwa kilo( kwa bei ya mnada) na mkulima kulipwa shilingi 1610 kwa kilo baada ya kupunguzwa kwa baadhi ya tozo.
Akizungumzia mnada huo Katibu Tawala wa Mkoa wa
Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga amesema bei hiyo ya choroko kwa njia ya mnada inamkomboa
mkulima na itamsaidia kuona faida na tija zaidi ya kilimo ikilinganishwa na bei
ya awali ambayo mkulima alikuwa akilipwa shilingi 800 mpaka shilingi 1200 kwa
kilo.
“Bei ya leo ya mnada ilikuwa shilingi 1578 kwa kilo
ambayo kwa maoni ya wakulima ina faida, lakini Halmashauri kwa kushirikiana na
ushirika wameongeza shilingi 32 kwa kilo ili kumsaidia mkulima kufanya
maandalizi ya msimu unaofuata wa mazao mengine na shughuli nyingine, kwa hiyo
leo mkulima amepata shilingi 1610 kwa kilo,” alisema Mmbaga.
Aidha, Mmbaga amewahakikishia wakulima usalama wa
mazao yao yatakapopokelewa katika maghala makuu kwa kuwa watunza maghala
wamekata bima zote ikiwepo bima ya moto na wizi kwa ajili ya kubeba dhamana
ikiwa kutatokea majanga au wizi.
Wakati huo huo Mmbaga ametoa wito kwa wakulima
kulima kilimo biashara ili waweze kupata faida na kuona tija katika kilimo chao
huku akiwasisitiza kutumia fedha zao vizuri kwa kuwekeza kwenye shughuli za
maendeleo ili waweze kutatua mahitaji mbalimbali ya kijamii.
Katika hatua nyingine Mmbaga ametoa wito kwa
Wafanyabiashara kutoka mikoa yote nchini kushiriki katika minada ya ununuzi wa
choroko katika maghala yaliyopo mkoani hapa na kuwahakikishia ushirikiano
wakati wowote watakapohitajika.
Bw. Daniel Mipawa ambaye ni mkulima kutoka Chama cha
ushirika cha Msingi cha Nhaya amesema uuzaji wa choroko kupitia mnada ameupokea
vizuri kwa kuwa umekuwa msaada kwenye suala la bei maana wakulima wamekuwa
wakiwauzia choroko baadhi ya wafanyabiashara shilingi 800 mpaka shilingi 1200.
Naye mfanyabiashara Ibrahim Musa akizungumzia hali
ya mnada na bei ya choroko amesema “Bei ya mnada wa leo wa choroko ya shilingi
1578 kwa kilo ilikuwa haitulipi lakini tumekaa na viongozi wa serikali wameamua
kutupunguzia baadhi ya tozo, kwa kuwa wametupunguzia baadhi ya tozo na
kuturudishia gharama za usafiri sasa hivi tutaenda vizuri.”
Kwa upande wake Msimamizi wa ghala kuu Maswa, Bw.
Abdallah Ngozi amesema mnada wa choroko umeenda vizuri na kushauri wakulima
pamoj na kuwa na nafasi ya kuamua kuuza au kutokuuza kulingana na bei ya mnada
wa siku husika wawe makini kwa kuwa wanaweza kukataa kuuza na bei ikashuka
zaidi ya ile ya awali
MWISHO
Baadhi ya vijana wakishusha choroko zilizokusanywa kutoka kwa wakulima kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) na kuzipeleka ghala kuu ili zihifadhiwe kwa ajili ya kuuzwa kupitia mnada katika mfumo wa stakabadhi ghalani
Baadhi ya Vijana
wakipakia choroko katika mifuko maalum yenye nembo ya alama ya Chama Kikuu cha
Ushirika cha Mkoa wa Simiyu (SIMCU) tayari kwa ajili ya kuzihifadhi kwa ajili
ya kusubiri mnada.
Baadhi ya vijana
wakishusha choroko zilizokusanywa kutoka kwa wakulima kupitia Vyama vya
Ushirika vya Msingi (AMCOS) na kuzipeleka ghala kuu ili zihifadhiwe kwa ajili
ya kuuzwa kupitia mnada katika mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mkuu wa Wilaya ya
Maswa, Mhe. Aswege Kaminyoge(kulia) akiteta jambo na Katibu Tawala wa Mkoa wa
Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga mara baada ya mara baada ya muda wa choroko za Simiyu
kumalizika Machi 02, 2021.
Katibu Tawala wa Mkoa
wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga akiangalia namna mnada wa choroko unavyofanyika
kupitia mtandao kwa kutumia kompyuta iliyokuwa mbele yake (haipo pichani)
katika eneo la Sola Wilayani Maswa Machi 02, 2021 wengine ni wafanyabiashara wa
choroko wakifuatilia mnada huo pia.
Afisa Kilimo wa Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Iman Matimbwa (kulia) akimuonesha jambo Mkuu wa
Wilaya ya Maswa, Mhe. Aswege Kaminyoge (kushoto) kuhusu mnada wa choroko
kupitia mtandao, mara baada ya muda wa choroko za Simiyu kumalizika Machi 02,
2021.
Katibu Tawala wa Mkoa
wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga akiangalia namna mnada wa choroko unavyofanyika
kupitia mtandao kwa kutumia kompyuta iliyokuwa mbele yake (haipo pichani)
katika eneo la Sola Wilayani Maswa Machi 02, 2021.
0 comments:
Post a Comment