Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa amesema Serikali
itachimba visima kumi vya maji mara moja katika eneo la Mto Semu Kijiji cha
Magwila wilayani Meatu na kujenga mtandao wa bomba kutoka katika visima hivyo mpaka mjini Mwanhuzi wilayani humo Mkoani Simiyu, ili
kukabiliana na adha ya maji kwa wananchi baada ya kukauka kwa bwawa la
Mwanyahina.
Prof. Mbarawa amesema hayo jana Novemba 19, 2019 wakati
akizungumza na wananchi wa Mwanhuzi mara baada ya kutembelea na kuona Bwawa la
Mwanyahina lililokauka ambalo ndiyo chanzo kikuu cha maji katika Mji huo na
eneo la Mto Semu kilipo kisima kinachotumiwa sasa, ambapo watu wanachota maji
kwa magari na kuwauzia wananchi mjini Mwanhuzi.
“ Mhe.Rais amenielekeza kwamba tutachimba visima
kumi haraka kutoka kule ambako maji yanachotwa sasa, tutajenga mtandao wa bomba
kutoka kwenye visima mpaka hapa mjini,
ili maji yale yatolewe visimani na kuletwa kwenye mfumo wa maji wa hapa mjini,”
alisema Mbarawa.
Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa amesema Wizara
ya maji imetoa magari matatu kwa ajili ya kusaidia kubeba maji kutoka kisima na
kusambaza kwa wananchi, huku akiagiza ukarabati wa Bwawa la Mwanyahina
kufanyika kwa kutoa tope.
Awali akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji,
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani amesema Bwawa la Mwanyahina
limekauka kutokana na kujaa tope na ukame uliotokea wilayani humo katika msimu
wa mvua wa mwaka 2018/2019.
Aidha, Dkt. Chilongani ameomba Wizara ya maji iweze
kutoa kipaumbele kwa miradi yote ya maji iliyosanifiwa iweze kutekelezwa katika
Wilaya ya Meatu, ili kuongeza hali ya upatikanaji wa maji vijijini na mjini.
Kwa upande wao wananchi wa Mji wa Mwanhuzi wameishukuru
Serikali kwa kukubali kuwachimbia visima ambavyo vitawasaidia kuondokana na
adha maji baada ya Bwawa la Mwanyahina kukauka na kusababisha wao kununua ndoo
moja ya lita 20 kwa shilingi 100 hadi 200.
“Sasa hivi tunauziwa ndoo ya lita ishirini kwa
shilingi 200, tunaishukuru Serikali kuona kilio chetu, pia tunamshukuru Waziri
wetu wa Maji kwa mpango aliokuja nao wa kutuchimbia visima na kutuletea
maji hapa mjini, tunaomba mpango huu
ufanyike haraka, ili tuondakane na shida ya maji tuliyonayo sasa,” alisema
Mariam Kashinje mkazi wa Mwanhuzi.
“Binafsi namshukuru Mbunge wetu kwa kutoa gari lake
ambalo linatoa huduma ya maji bure, pia tunamshukuru Mhe. Diwani wetu Zakaria
kuruhusu watu kuchota maji kwenye kisima chake na kubeba kwenye maboza na sisi wananchi tunanunua; lakini nimefurahishwa sana na
mpango wa Waziri wa Maji aliyesema Mhe.
Rais anataka tuchimbiwe visima naamini tatizo hili litaisha,” alisema Mboi
Ngidinga.
MWISHO
Mkuu
wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani (kushoto) akimuongoza Waziri wa Maji Prof.
Makame Mbarawa(wa tatu kulia) kuelekea katika kisima kilichopo eneo la Mto Semu
kijiji cha Magwila wilayani Meatu Novemba 19, 2019, ambacho kinatumiwa kutoa
huduma kwa sasa kwa wananchi wa Mji wa Mwanhuzi baada kukauka kwa Bwawa la Mwanyahina
ambalo ndiyo chanzo kikuu cha Maji katika Mji wa Mwanhuzi.
Mbunge
wa Jimbo la Meatu Mhe. Salum Khamis (mwenye kofia) akimuonesha jambo Waziri wa
Maji Prof. Makame Mbarawa(mwenye miwani kulia)alipotembelea kuona eneo la
chujio la Maji katika Mji wa Mwanhuzi wilayani Meatu Novemba 19, 2019.
Mkuu
wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Maji
Prof. Makame Mbarawa(wa pili kulia) kuhusu Bwawa la Mwanyahina chanzo kikuu cha
Maji katika Mji wa Mwanhuzi ambalo limekauka kwa sasa, wakati wa ziara yake Novemba
19, 2019.
Sehemu
ya Bwawa la Mwanyahina chanzo kikuu cha Maji katika Mji wa Mwanhuzi ambalo
limekauka kwa sasa ambalo Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa ameagiza
lifanyiwe ukarabati kuondolewa tope.
Baadhi
ya wananchi wa Mjini Mwanhuzi wilayani Meatu wakipata huduma ya maji kutoka
kwenye magari yanayosomba maji kutoka katika Kisima baada ya changamoto ya maji
katika mji huo iliyosababishwa kukauka kwa Bwawa la Mwanyahina.
Baadhi
ya wananchi wa Mji wa Mwanhuzi wakiwa katika foleni ya kupata huduma ya maji kutoka
kwenye magari yanayosomba maji kutoka katika Kisima baada ya changamoto ya maji
katika mji huo iliyosababishwa kukauka kwa Bwawa la Mwanyahina.
Waziri
wa Maji Prof. Makame Mbarawa(wa tatu kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya
ya Meatu, Mhe. Joseph Chilongani moja ya
gari litakalotumika kwa dharura kusomba maji kutoka kisima kilichopo eneo la
mto Semu kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi kabla ya kuchimbwa kwa visima
kumi , wakati wa ziara yake Novemba 19, 2019.
Baadhi
ya wananchi wa Mji wa Mwanhuzi wakimsikiliza Waziri wa Maji Prof. Makame
Mbarawa(hayupo pichani) wakati akizungumza nao, Novemba 19, 2019 mara baada ya kutembelea na kuona Bwawa la
Mwanyahina lililokauka na eneo la Mto Semu kilipo kisima kinachotumiwa sasa
ambapo maji yanachotwa na kubebwa kwa magari na kupelekwa mjini ambapo wananchi
wananunua.
Baadhi
ya vijana wakipakia maji katika matanki kwa ajili ya kuwapelekea wananchi huduma
ya maji katika Mji wa Mwanhuzi baada ya changamoto ya maji katika mji huo
iliyosababishwa kukauka kwa Bwawa la Mwanyahina.
Waziri
wa Maji Prof. Makame Mbarawa(mwenye miwani katikati) akiangalia maji yanayotoka
katika kisima kilichopo eneo la mto Semu kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi
kabla ya kuchimbwa kwa visima kumi , wakati wa ziara yake Novemba 19, 2019.
Waziri
wa Maji Prof. Makame Mbarawa akiwa na baadhi ya viongozi katika eneo la Chujio
la Maji Mjini Mwanhuzi wakati wa zaira yake wilayani Meatu Novemba 19, 2019.
0 comments:
Post a Comment