Na
Stella Kalinga, Simiyu RS
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini
amesema mkoa huo umejipanga kikamilifu kuwapokea wanafunzi wa kidato cha sita kwa
ajili ya kuanza masomo Juni Mosi, 2020 kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari leo 23 Mei,2020
Sagini amesema Simiyu iliandaa mkakati maalum kwa kushirikiana na wadau
kuwawezesha wanafunzi kujisomea hivyo, mkoa utahakikisha muda uliotolewa na
Wizara ya elimu kufanya maandalizi ya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita (Juni
Mosi-Juni 28) unatumika vizuri na walimu na wanafunzi kwa ajili ya rejea na
kukamilisha mada.
“Sisi kama mkoa elimu ni kipaumbele cha kwanza hivyo tumejipanga kikamilifu kuwapokea vijana
wetu wa kidato cha sita, ikumbukwe pia kuwa kama mkoa tuliandaa mkakati wa kuwasaidia
wanafunzi kujisomea hususani madarasa ya mitihani wakati walipokuwa likizo ya
tahadhari ya Corona; tutahakikisha muda uliotolewa na wizara ya elimu kujiandaa
na mtihani wa Taifa unatumika vizuri kufanya marejeo na kukamilisha mada
zilizobaki,”alisema Sagini.
Aidha, Sagini amesema viongozi katika maeneo yote
watahakikisha tahadhari zote zinazotolewa na Wizara yenye dhamana na Afya katika
kujikinga na maambukizi ya Virusi vya
Corona zinazingatiwa katika shule zote za kidato cha sita Mkoani Simiyu.
Vile vile Sagini ametoa wito kwa wazazi na walezi
mkoani Simiyu kuendelea kuwahimiza na kuwasimamia watoto wao walioko majumbani kujisomea
wakati huu ambao wengine bado wako likizo mpaka shule zitakapofunguliwa, huku
akisisitiza kuwa mkakati wa mkoa wa kuwawezesha wanafunzi kujisomea wakati
wakiwa likizo utaendelea kutekelezwa.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju
amesema pamoja na utekelezaji wa mkakati maalum wakati likizo, kabla ya
serikali kutangaza kufunga shule wanafunzi wa kidato cha sita walikuwa katika
kambi ya kitaaluma, ambapo takribani mada zote zilikuwa zimeshakamilika na wanafunzi
walikuwa wakipewa majaribio na kurudia mada ambazo hazikueleweka vizuri.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu,
Bw. Fabian Manoza amesema idara ya elimu
katika Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na waratibu elimu kata wamejipanga kuhakikisha kuwa wanakamilisha
mahitaji yote ya kujisomea kwa wanafunzi wa kidato cha sita yanaandaliwa na
kukamilika kwa wakati ili kuwawezesha kujiandaa na mtihani wa Taifa.
Kwa
upande wake mmoja wa wazazi wenye wanafunzi wa kidato cha Sita mjini Bariadi,
Bw. Chambwite Sadala amesema anaunga mkono uamuzi wa Mhe. Rais wa wanafunzi wa
kidato cha sita kurudi shuleni, hivyo akatoa wito kwa wanafunzi hao kwenda kufanya
bidii katika kujisomea katika muda waliopewa ili waweze kufanya vizuri na
hatimaye kufikia malengo yao.
Mkoa wa Simiyu una jumla ya shule 13 za sekondari za
Kidato cha tano na Sita, ambapo kwa mwaka 2020 jumla ya wanafunzi 953 wa kidato
cha Sita wanatarajiwa kufanya mtihani wa Taifa kuanzia tarehe 29 Juni 2020 kama
ilivyotangazwa na Waziri wa elimu, sayansi na teknolojia, Prof. Joyce
Ndalichako.
MWISHO
Katibu
Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akizungumza na waandishi wa habari
(hawapo pichani) Mei 23, 2020 kuhusu utayari wa mkoa katika kuwapokea wanafunzi
wa kidato cha sita kwa ajili ya kuanza masomo Juni Mosi, 2020 kama
ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli.
Afisa
Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju akitoa ufafanuzi wa jambo kwa waandishi
wa habari (hawapo pichani) Mei 23, 2020
kuhusu utayari wa mkoa katika kuwapokea wanafunzi wa kidato cha sita kuanza
masomo Juni Mosi, 2020 kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
0 comments:
Post a Comment