Shirika
lisilo la kiserikali la World Vision limekabidhi msaada wa vifaa vya kujikinga
na maambukizi ya Virusi vya Corona pamoja na Jengo la zahanati kwa uongozi wa
mkoa wa Simiyu vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 95.7.
Akikabidhi
msaada huo jana Mei 08, 2020 kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne
Sagini katika kijiji cha Wigelekelo wilayani Maswa, Meneja wa World Vision
Kanda ya Ziwa, Bw. John Massenza amesema pamoja na zahanati wamekabidhi mipira
ya kuvaa mikononi, vitakasa mikono,vipaza sauti, barako na mavazi maalum ya
wataalam wa afya.
"Pamoja na zahanati leo tunakabidhi mipira ya kuvaa
mikononi boksi 500,vitakasa mikono lita 200,vipaza sauti 26 kwa wahudumu wa
afya ngazi za jamii na mavazi ya kujikinga na maambukizi 60 na barakoa
aina ya N95, vyote vikiwa na thamani ya shilingi 95,755,000/=, "alisema Massenza.
Aidha, ameongeza kuwa shirika hilo kwa kushirikiana na ofisi ya
mganga mkuu wa mkoa wa Simiyu na waganga wakuu wa wilaya litaendelea kutoa
misaada ya vifaa , vitendea kazi, kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na
kuhakikisha wanasambaza elimu ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID
19) inayosababishwa na virusi vya Corona. .
" Shirika limeendelea kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa
wa homa ya mapafu kwa njia ya matangazo na tumewezesha mafunzo kwenye
makundi tofauti ya watu ambayo yatasambaza elimu hii kwa jamii mfano wa makundi
hayo ni viongozi wa dini,wahudumu wa afya ,viongozi wa serikali, "alisema Massenza.
Akipokea vifaa hivyo pamoja na zahanati Katibu Tawala Mkoa wa
Simiyu, Bw Jumanne Sagini ameishukuru World Vision kwa msaada huo ambao
umetolewa kwa Halmashauri zote sita pamoja na kuwa shirika hilo linafanya
kazi na halmashauri ya wilaya ya Maswa na Itilima; huku akibainisha kuwa vifaa
kinga hivyo vitawajengea ujasiri watoa huduma za afya kuwahudumia
watakaobainika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Naye mganga mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt.Festo Dugange amesema
wamekuwa wakitekeleza afua mbalimbali za kuhakikisha wananchi wanakuwa salama
dhidi ya ugonjwa wa COVID 19 kwa kutoa
elimu ya namna ya kujikinga, huku akiongeza kuwa mkoa upo vizuri na tayari umeshatenga
vituo endapo watapatikana washukiwa wa ugonjwa huo.
Akiongea kwa niaba ya wakurugenzi wa halmashauri mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Dkt. Frederick Sagamiko
amelishukuru shirika hilo kwa kuwa msaada mkubwa kwenye shughuli za maendeleo
mkoani hapo hususani katika wilaya ya Itilima na Maswa ambapo kwa Maswa mbali
na kuwajengea zahanati pia limesaidia katika ujenzi wa kiwanda cha viazi lishe
na wilaya ya Itilima kiwanda cha sabuni.
Kwa upande wao wananchi wa kijiji cha Wigelekelo wakiwemo Mbuke
Kemakema na Mashauri Ngeme wamelipongeza shirika hilo kwa ujenzi wa zahanati
ambayo itawasaidia kupata huduma za afya karibu kwani awali walikuwa wakitembea umbali mrefu
kufuata huduma za afya.
MWISHO
Meneja wa World Vision
Kanda ya Ziwa, Bw. John Massenza akitoa maelezo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa
Simiyu, Bw. Jumanne Sagini(kulia) kuhusu mavazi maalum kwa watoa huduma yatakayovaliwa
wakati wa kuwahudumia watakaobainika kuwa na maambukizi ya Corona ikiwa ni
sehemu ya vifaa kinga vilivyotolewa msaada na Shirika lisilo la Kiserikali la
World Vision kwa Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya Virusi
vya Corona, makabidhiano hayo yamefanyika katika kijiji cha Wigelekelo wilayani
Maswa, Mei 08, 2020.
Katibu Tawala wa Mkoa
wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akiangalia
moja ya vitakasa mikono vilivyotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la World
Vision kwa Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya
Corona, katika makabidhiano yaliyofanyika
katika kijiji cha Wigelekelo wilayani Maswa, Mei 08, 2020.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akiwa na viongozi wengine wakitoka kukagua jengo la zahanati ya Wigelekelo iliyojengwa na Shirika lisilo la Serikali la World Vision kwa kushitrikiana na wananchi na kukabidhiwa kwa serikali Mei 08, 2020 Wilayani Maswa.
Mganga mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Festo Dugange akizungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini kutoa salamu za mkoa wakati wa makabidhiano ya msaada wa zahanati pamoja na vifaa kinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona vilivyotolewa na Shirika lisilo la Serikali la World Vision kwa Mkoa wa Simiyu katika Kijiji cha Wigelekelo wilayani Maswa, Mei 08, 2020.
Katibu Tawala wa Mkoa
wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akiwa na
viongozi wengine katika ukaguzi wa jengo la zahanati ya Wigelekelo iliyojengwa
na Shirika lisilo la Serikali la World Vision kwa kushitrikiana na wananchi na
kukabidhiwa kwa serikali Mei 08, 2020 Wilayani Maswa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akimuuliza jambo Meneja wa World Vision Kanda ya Ziwa, Bw. John Massenza baada ya kukabidhiwa vifaa kinga vilivyotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la World Vision kwa Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona, katika makabidhiano yaliyofanyika katika kijiji cha Wigelekelo wilayani Maswa, Mei 08, 2020.
Katibu Tawala wa Mkoa
wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akipokea maelezo kutoka kwa Meneja wa World
Vision Kanda ya Ziwa, Bw. John Massenza baada ya kukabidhiwa vifaa kinga vilivyotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali
la World Vision kwa Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya
Virusi vya Corona, katika makabidhiano
yaliyofanyika katika kijiji cha Wigelekelo wilayani Maswa, Mei 08, 2020.
0 comments:
Post a Comment