SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu imepanga kufufua viwanda viwili vya kuchambua pamba na kukamua mafuta ya pamba musimu huu wa ununuzi wa zao la pamba wa mwaka 2022/2023.
Miongoni mwa viwanda vitakavyofufuliwa ni pamoja na Kiwanda cha Kuchambua Pamba cha Sola(Maarufu kwa jina la Sola Ginnery) kilichoko mjini Maswa pamoja na kiwanda cha Lugulu kilichoko wilaya ya Itilima.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu,David Kafulila mara baada ya kukitembelea kiwanda hicho ambacho kimeacha uzalishaji miaka mingi iliyopita kikiwa chini ya Chama cha Ushirika Cha Mkoa wa Shinyanga(SHIRECU) lakini kwa sasa kipo chini ya Chama Cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU).
Amesema kuwa baada ya mkoa huo kufanya vizuri katika uzalishaji wa zao la pamba ndiyo maana serikali imeamua kutoa fedha kwa ajili ya kuvifufua viwanda hivyo ili shughuli za kuchakata pamba na kukamua mafuta viweze kufanya kazi mwaka huu.
Mkuu huyo wa mkoa amewataka viongozi wa SIMCU kuona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati maghala ya kuhifadhia pamba na marobota ya pamba katika kiwanda hicho.
Awali Afisa Ushirika wa wilaya ya Maswa,Cosmas Budodi akisoma taarifa ya kiwanda hicho kwa niaba ya Uongozi wa SIMCU pamoja na kuipongeza serikali kwa hatua yake hiyo ya kukifufua kiwanda hicho hivyo wameomba pia serikali kusaidia kutatua changamoto ya deni kubwa la umeme na maji katika kiwanda hicho sambamba na kuwaondoa wananchi waliovamia eneo la kiwanda na kufanya shughuli mbalimbali za kibinadamu. Mwisho.
0 comments:
Post a Comment