Sunday, February 13, 2022

SIKU YA MKULIMA NYAKABINDI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mheshimiwa David Kafulila hii leo (11.02.2022) amegawa miche zaidi ya 12,000 ya viazi lishe kwa wakulima wa Mikoa ya Simiyu na Mara wakati  wa ufunguzi wa siku ya mkulima (Farmers Field Day) uliofanyika  katika Kituo Mahiri na atamizi cha usambazaji teknolojia za Kilimo cha TARI kilichopo  Nyakabindi, Wilayani Bariadi.

Mheshimiwa Kafulila ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Siku hiyo maalum  ya Mkulima ameipongeza TARI kwa kuanzisha Kituo hicho  ambacho kinasaidia kutoa elimu ya nadharia na vitendo kwa wakulima na wadau wengine kwa kipindi chote cha mwaka kwa kulima kilimo chenye tija na kuepukana na kilimo cha mazoea.

Akiwa Kituoni hapo Mheshimiwa Kafulila alipata fursa ya kutembelea vipando vya mazao ya aina mbalimbali kama vile mtama, ulezi, mahindi, njegere, maharage ya soya lishe, migomba, viazi lishe, mihogo na mazao ya bustani. Pia alitembelea vipando vya  mazao ya kimkakati ambayo ni Pamba, Miwa ya sukari, mkonge, michikichi na korosho.

Mheshimiwa Kafulila alifurahishwa na kustawi kwa vipando vya mazao ya kimkakati ya mkonge na korosho na kuwataka wakulima pamoja na kuendelea na kilimo cha pamba, alizeti, mbaazi, dengu na choroko wafikirie kulima mazao hayo  ya kudumu ya kimkakati  ili yawasaidie pindi nguvu za kulima zitakapowaishia. Amewaagiza wakulima wa Wilaya ya Bariadi kulima zao la mkonge huku wakulima wa Wilaya ya Busega kulima zao la korosho kwa kuwa maeneo yao yanastawisha vizuri mazao hayo.

Awali akisoma taarifa ya TARI, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TARi alimweleza Mgeni Rasmi kuwa Lengo kubwa la siku ya Mkulima ni kufikisha matokeo ya utafiti kwa wakulima ambao hufika kituoni hapo kujifunza kwa nadharia na vitendo ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kuzingatia kilimo chenye tija huku wakiongeza kipato katika kaya na Taifa kwa ujumla. Kauli mbiu ya siku ya Mkulima ni “Tumia tekinolojia bora za kilimo za TARI kuongeza tija na mavuno. 

 Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Kafulila amezindua shamba la vitunguu maji  la vijana 50  wa skauti lililopo katika eneo la NaneNane baada ya kupatiwa mafunzo katika  Kituo cha TARI Nyakabindi. 

Vijana hao kutoka Wilaya ya Bariadi ambao wanafadhiliwa na Serikali kupitia Mkoa wa Simiyu wameanza kulima na kupanda ekari nne za vitunguu maji huku wakisimamiwa kwa karibu na TARI Nyakabindi kwa kila hatua mpaka watakapovuna vitunguu vyao. 

Mheshimiwa Kafulila ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Bariadi kuhakikisha vijana hao wanapatiwa fedha zote za mkopo walizoomba na waongezewe eneo la kilimo ili wapanue wigo wa kilimo chao na kuwapa hamasa vijana wengi zaidi kushiriki katika sekta ya Kilimo kama ajira na kuinua uchumi  wao binafsi, Wilaya na Taifa kwa ujumla. Ameuagiza uongozi wa TARI kuendelea kuwajengea uwezo na kuwasimamia vijana hao ili waweze kufikia lengo walilokusudia. 

Kituo mahiri  na atamizi cha usambazaji teknolojia bora za kilimo Nyakabindi ni Kituo cha mfano kilichoanzishwa na kuanza kufanya kazi mwezi Julai, 2020  kikisimamiwa na TARI kupitia Vituo vya Ukiriguru na Maruku.Mwisho.
0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!