Mkoa wa Simiyu, umeshika nafasi ya tatu(3) kitaifa matokeo ya kidato cha nne(IV), ukiwa mkoa pekee wenye halmashauri mbili zilizoongeza ufaulu kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo (halmashauri hizo ni halmashauri ya Meatu na Busega).
Aidha katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa Elimu ya Msingi (PSLE) 2021 kwa shule za Msingi za Serikali, kati ya shule kumi bora zilizoongoza katika ufaulu wa mtihani huo, shule ya kwanza na iliyongoza katika ufaulu kitaifa ni shule ya Msingi Mwanhegele yenye usajili Namba PS2705086 iliyopo wilayani Maswa,mkoani Simiyu.
Hali kadhalika kati ya watahiniwa bora kumi (10) kitaifa kutoka shule za Serikali kwa mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi (PSLE),2021, mmojawapo kati ya wanafunzi kumi bora ametokea mkoa wa Simiyu.
Aidha, kati ya Wasichana kumi (10) bora kitaifa, katika mtihani huo, asilimia 50 ya wasichana bora kitaifa wametoka Mkoa wa Simiyu. Wakiongozwa na Mwanafunzi, Hollo Seni Mbuga, kutoka shule ya Msingi Inonelwa - Meatu, ambaye ni wa kwanza kitaifa, Lydia Kija Mashala toka shule ya msingi Mwanhegele-Maswa akiwa namba tatu, Dorica Yusuph Joseph toka shule ya msingi Mwanhengele-Maswa, akiwa namba 5, Kundi Shibu Satto toka Mwakaluba-Meatu akiwa namba 6 na Jackline Luswaga Emmanuel toka shule ya Msingi Mwanhegele-Maswa akiwa mshindi namba 10.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.David Kafulila amewapongeza Wanafunzi,Waalimu,maafisa elimu wa ngazi zote sanjali na wakuu wa wilaya, Wakurugenzi na wanataaluma wote kwa usimamizi imara na kuendelea kuchapa kazi licha ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nao.
Pamoja na kuongoza kielimu Mkoa wa Simiyu ni kianara wa Pamba Tanzania. Kazi iendelee.
0 comments:
Post a Comment