Wednesday, February 23, 2022

Mhe. Kafulila Ampongeza Diaspora wa Kike ( Dkt. Ashley Lucas) toka Simiyu, Daktari aliyeamua kuwekeza nyumbani.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila ametoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea kituo cha afya cha Barikiwa kilichopo Wilayani Maswa, kituo ambacho kimejengwa na mwanadada Mtanzania, mzaliwa wa Maswa ambaye ni Daktari.Akitoa Pongezi hizo Mhe. Kafulila amefurahishwa sana, mara baada ya kuona baadhi vijana wa kitanzania ambao ni wazalendo na wanaokumbuka kwao,kwani vijana wengi mara wapatapo fursa za kuenda nchi za nje huzamia na kutokukumbuka kabisa kirudi nyumbani.  “ Nikupongeze sana Dkt. Ashley kwa kukumbuka kurudi nyumbani na si kurudi tu bali na kuwekeza nyumbani na hasa kwa ndoto kubwa ulizonazo kuelekea Maswa”.Amesema Kafulila.
 
Akielezea Maswa ijayo Mhe. Kafulila amesema “Kipindi kifupi kijacho,Maswa, haitakuwa Maswa ya sasa, ujenzi wa reli ya SGR, utaleta fursa nyingi sana za uwekezaji, kwani majengo yanayotumika sasa kama ofisi kwa ajili ya ujenzi, baada ya ujenzi kukamilika ofisi hizo zitatumika kama chuo cha kilimo na mifugo na hivyo kuzalisha ajira na kuongeza shughuli za kiuchumi. Aidha Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mama Samia Suluhu Hassan ina mpango wa kufungua (Logistic Hub) pamoja na dry Port/ Bandari kavu Maswa,  hivyo bila shaka unaona jinsi Maswa itakavyokuwa na shughuli nyingi na za kutosha. Hivyo wakati unaendelea na uwekezaji wako wa ujenzi wa hospitali ya Barikiwa ni vyema ukafikiria pia ujenzi wa chuo cha afya Barikiwa, kwani Mkoa wa Simiyu una changamoto kubwa sana ya ukosefu wa vyuo vya afya na utalii”. Amesema Kafulila.
 
“Kwa kawaida uwepo wa hospital huenda sambamba na uwepo wa chuo cha afya kwani hii huwezesha wanafunzi wa chuo cha afya kufanya elimu ya vitendo hapohapo hospitalini. Mfano mzuri ni hospitali ya Bugando Mwanza, Muhimbili- Dsm,Hubert Kairuki-Dsm na kadhalika hospitali zote hizo zina vyuo vya afya eneo katika eneo la hospital husika”.Amesisitiza Kafulila
 
Dkt Ashley Lucas,ni mke na mama wa watoto watatu, mzaliwa wa Maswa ambaye amepata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Binza,Maswa, elimu ya sekondari shule ya sekondari Mwamapalala ambapo amesoma kidato cha kwanza na baadae akaenda Kampala Uganda na kujiunga na shule ya sekondari Kampala, ambapo alipata elimu ya kidato cha pili hadi cha sita kisha chuo cha habari, Kampala (UMCAT) na baadae kupata wafadhili na kwenda nchini Marekani ambapo alikaa kwa kipindi cha miaka mitano huku akisoma na kutunukiwa digrii ya udaktari wa Kinywa na Meno ( Dental Surgery). Baada ya kumaliza masomo yake Dkt. Ashley aliamua kurejea nyumbani  Tanzania huku akiwa na lengo la kuwasaidia Watanzania wenzake na hasa wakazi wa Maswa, na hivyo kuwiwa kutumia elimu yake katika kutoa huduma za afya za kinywa na zinginezo.
 
“Hii Zahatani inaitwa Barikiwa,lakini baada ya wiki mbili hivi itapanda daraja na kuwa hospitali ya Barikiwa”. Ameeleza Dkt Ashley.
 
Zahanati hiyo ipo kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari saba. Akielezea ndoto zake Mwana dada huyo Dkt.Ashley ameeleza kuwa “lengo langu ni  Kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za Wizara ya afya. Ninataka kujenga hospital ambayo itatoa huduma kiasi cha kwamba Wagonjwa toka Maswa au hata mkoa mzima wa Simiyu  hawatahitaji tena kwenda Bugango kwa ajili ya matibabu. Lengo langu kubwa ni kuwasaiida wakazi wa Maswa na Simiyu katika viwango vya huduma ya afya vya hali ya juu.

Vifaa tiba kwa ajilii ya wagonjwa wote hii ikiwa ni pamoja na huduma ya afya kwa mama na motto vyote vipo tayari, duka la dawa la nje, maabara,chumba cha upasuaji na chumba cha kujifungulia vyote vipo katika hatua za mwisho mwisho na hivyo vitakuwa tayari katika kipindi cha wiki mbili zijazo” Amesema Ashley.
 
Akizungumzia changamoto za mradi huu Dkt. Ashley ametaja janga la UVIKO-19, limesababisha madaktari kutoka nje ambao mara kwa mara wamekuwa wakija kujitolea kushindwa kuja, aidha alifanikiwa kupata msaada wa kontena mbili za vifaa ambalo nalo limekwama kwa sababu ya changamoto hiyo.
 
Pamoja na huduma ya kujenga majengo ambayo yatatumika kutoa huduma za kiafya, Dkt.Ashley, anatarajia kujenga nyumba za madaktari na wafanyakazi ambazo zitawezesha kukaa karibu na hospitali na hivyo kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na salama za afya kwa masaa ishirini na nne na siku saba kwa wiki.Mwisho.








0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!