Sunday, September 8, 2019

RC MTAKA AWAHAKIKISHIA WAKULIMA SIMIYU PAMBA YAO KUNUNULIWA NA KULIPWA FEDHA ZAO

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewakikishia wakulima wa pamba mkoani Simiyu kuwa Serikali itahakikisha mwezi huu pamba yote inanunuliwa kwa bei elekezi ya shilingi 1200 kwa kilo na wakulima kulipwa fedha zao, ambapo amesema hadi sasa zaidi ya kilo milioni 54 zenye thamani ya shilingi bilioni 65.1 zimenunuliwa na wakulima wamelipwa fedha zao.


Mtaka ameyasema hayo wakati wa ziara ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu katika vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) na Kiwanda cha Kuchambua pamba cha Alliance Ginneries Limited  wilayani Bariadi, iliyofanyika Septemba 08, 2019 kwa lengo la kujionea mwenendo wa ununuzi wa pamba, ambapo amewataka wanunuzi kutumia fedha walizopewa dhamana na Serikali kwa ajili ya kununua pamba zitumike kuwalipa wananchi badala ya kuzielekeza mahali pengine au kufanya tofauti na makubaliano.


Amesema makisio ya mkoa ya mavuno yalikuwa ni kuvuna kilo milioni 180 ambapo hadi sasa pamba iliyokusanywa ni kilo milioni 132 ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 159.3 na kati ya hizo kilo milioni 54 zenye thamani ya shilingi bilioni 65.1 zimelipiwa na  ambazo bado hazijalipiwa ni kilo milioni 78.5 ambayo thamani yake ni zaidi ya shilingi milioni 94.2
.
Ameongeza kuwa kuelekea katika kipindi cha mvua za vuli Mtaka ni vema wakulima kutoa pamba majumbani na kupeleka pamba kwenye vyama vya ushirika ili itunzwe katika mazingira salama na iweze kununuliwa, huku akitoa wito pia kwa wanunuzi kujielekeza kwenye maeneo ambayo ni magumu kufikika kipindi cha mvua na maeneo ambayo maghala yake si salama sana.

Aidha, Mtaka amewakata viongozi wa vyama vya ushirika kuwa waadilifu badala ya kushirikiana na machinga kuwanyonya wakulima kwa kuuza pamba chini ya bei elekezi ya shilingi 1200 na kuwataka wanunuzi kununua pamba kwa mujibu wa utaratibu kwa kuwa watakaobainika wananunua kama machinga watachukuliwa hatua na pamba hiyo itapigwa mnada.

“Ujumbe huu uwafikie wanunuzi wote wa pamba wanaokuja kununua pamba Simiyu , pamba itanunuliwa kwenye vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS)kwa bei elekezi ya shilingi 1200 kwa kilo, pamba haitanunuliwa kienyeji kwenye nyumba za watu usiku kwa bei ndogo, atakayekamatwa asije akalaumu vyombo vya sheria”alisema Mtaka.

Naye Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Enock Yakobo amewataka wanunuzi wa pamba mkoani Simiyu kuhakikisha kuwa wanawalipa wakulima fedha zao kwa wakati ili waweze kujikimu namahitaji yao na kujiandaa na msimu ujao wa kilimo.

Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba nchini, Bw. Boaz Ogola amesema Serikali imewahakikishia wanunuzi wote kuwa itakuwa tayari kufidia hasara itakayopatikana endapo watapata hasara wakinunua pamba kwa shilingi 1200, hivyo mwenendo wa ununuzi wa pamba nchini ni mzuri  ambapo hadi tarehe 01/09/2019 kilo milioni 210 zimeshanunuliwa nchi nzima.

Kwa upande wao Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shelakaghe  wamesema pamba inaendelea kununuliwa katika maeneo yao huku wakisema wataendelea kusimamia na kuhakikisha pamba inanunuliwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na wananchi wanapata fedha zao.

Awali  wakulima wamesema kuwa baadhi ya makampuni ya ununuzi pamba hayajawalipa fedha zao hivyo wakaomba  Serikali kuwasaidia kuongea na wanunuzi wa zao hilo ili fedha zao zipatikane kwa wakati waweze kununua chakula na mahitaji mengine na kujiandaa na msimu ujao.

"Sisi tunaitegemea pamba na hapa kuna makampuni tunawadai hela zetu tunaiomba serikali itusaidie tupate fedha zetu tuna mambo mengi ya kufanya,tunataka tununue chakula kabla bei haijapanda sasa hivi kila mara bei ya mahindi inapanda"alisema Charles Ng'andwe kutoka Kijiji cha Ibulyu Bariadi.
MWISHO


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza jambo katika Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginneries Limited kilichopo Bariadi Mkoani Simiyu, wakati wa ziara ya viongozi wa mkoa huo ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.
Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba nchini , Bw. Boaz Ogola ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginneries Limited kilichopo Bariadi Mkoani Simiyu, akimweleza jambo viongozi wa Mkoa huo walipotembeelea kiwandani hapo kwa lengo la kujionea namna kiwanda hicho kinavyonunua pamba kutoka kwa wakulima katika ziara iliyofanyika Septemba 08, 2019.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wakulima wa Kijiji cha UIbulyu wilayani Bariadi wakati wa ziara ya viongozi wa mkoa huo ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.
Mkulima wa pamba Bw. Charles Ng’wande kutoka katika Chama cha Ushirika cha Msingi (AMCOS) cha Ibulyu wilayani Bariadi akitoa hoja yake wakati wa ziara ya viongozi wa mkoa wa Simiyu,  wakiongozwa na Mkuu wa mkoa Mhe. Anthony Mtaka  ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.
Mkulima wa Pamba Bw. Musa Makelemo kutoka katika Chama cha Ushirika cha Msingi (AMCOS) cha Mbiti wilayani Bariadi akitoa hoja yake wakati wa ziara ya viongozi wa mkoa wa Simiyu,  wakiongozwa na Mkuu wa mkoa Mhe. Anthony Mtaka  ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Mbiti wilayani Bariadi wakati wa ziara ya viongozi wa mkoa huo ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akiangalia pamba iliyochambuliwa na kufungwa kwenye robota katika kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginneries Ltd, wakati wa ziara ya viongozi wa mkoa huo ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo akizungumza na wakulima wa pamba katika Kijiji cha Mbiti wilayani Bariadi, wakati wa ziara ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akizungumza na baadhi ya wakulima wa pamba wa Kijiji cha Ibulyu wilayani humo, wakati wa ziara ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU), Bw. Cahrles Madata akizungumza na baadhi ya wakulima wa pamba katika Chama cha Ushirika cha Msingi (AMCOS) cha Kasoli wilayani Bariadi, wakati wa ziara ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe(mwenye miwani katikati) akizungumza na baadhi ya wakulima wa pamba kijiji cha Ibulyu katika ziara ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.
Kushoto ni Kiongozi wa Chama cha Ushirika cha msingi(AMCOS)  cha Kasoli akimweleza jambo Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (wa tatu kushoto) katika ziara ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akizungumzia hali ya ununuzi wa pamba ilivyo katika wilaya hiyo wakati wa kikao kilichofanyika mara baada ya ziara ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika leo Septemba 08, 2019.



0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!