Wednesday, September 11, 2019

WANAFUNZI WA DARASA LA SABA SIMIYU WAAHIDI KUFANYA VIZURI MTIHANI WA TAIFA


Wanafunzi wa darasa la saba katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani  Simiyu wamemuahidi Mkuu wa mkoa Anthony Mtaka hawatamuangusha katika mtihani wa Taifa  Septemba 11-12, kwa kuwa wamejiandaa vizuri na wanaimani watafanya vizuri.

Wanafunzi hao wa shule ya msingi Somanda A na B wametoa ahadi hiyo kwa niaba ya wanafunzi wote  wa darasa la saba wa mkoa wa Simiyu, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthoy Mtaka wakati akizungumza nao na kuwatakia heri katika Mtihani huo.

Wamesema wana imani ya kufanya vizuri kwa sababu hata Mtihani wa Mkoa Utilimilifu(Mock) walifanya vizuri, wameandaliwa vizuri kwa kupewa mazoezi na mitihani ya mara kwa mara na wamepata mbinu na maarifa mapya ya kujibu maswali ya mitihani kupitia  kambi za kitaaluma zilizofanyika katika kila shule.

“Sisi tumejiandaa vizuri sana na nina uhakika tutafanya vizuri katika Mtihani wa Taifa kama tulivyofanya vizuri kwenye Mock, walimu wametuandaa vizuri tulikuwa na kambi ya kitaaluma ambayo imetusaidia kukutana na walimu tofauti waliotufundisha vizuri zaidi, tunamuahidi Mkuu wa Mkoa kuwa hatutamuangusha” alisema Luhinda Nalisha kutoka S/M Somanda A.

“Tumejiandaa vizuri na tumejipanga kufanya vizuri, pia tunamshukuru Mkuu wa Mkoa kuja kututembelea na kutupa mawaidha tutayafanyia kazi, shule ipo vizuri kitaaluma na nidhamu  hivyo tuna uhakika wa kufaulu mtihani wa Taifa” alisema Bugumba Nindwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Somanda B

Akizungumza na wanafunzi hao, Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewatakia mtihani mwema na kuwataka watumie mbinu walizopewa na walimu kufanya vizuri, huku akiwaonya  kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wa aina yoyote.

Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa wahitimu wa vyuo vikuu  kufundisha masomo ya maandalizi ya Kidato cha kwanza(Pre-form one) kwa wanafunzi watakaohitimu darasa la saba  kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi na masomo ya elimu ya sekondari.

Naye Afisa elimu Msingi Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mwl. Christopher Ligonda akishukuru kwa niaba ya walimu amesema wanafunzi wameandaliwa vizuri na wamefundishwa vizuri na wako tayari kwa ajili ya mtihani na matarajio yao ni kupata ufaulu mzuri kama  walivyoahidi wenyewe.

Mkoa wa Simiyu una jumla ya wanafunzi 29, 248 wa darasa la saba wanaotarajia kufanya mtihani wa Taifa mwaka huu, ambao kati yao wavulana ni 13, 594 na wasichana 15, 654.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi wa darasa la Saba katika Shule ya Msingi Somanda A na B Mjini Bariadi wakiwa katika maandalizi ya Mtihani wa Taifa utakaofanyika Septamba 11-12, 2019, wakati akiwatakia heri katika mtihani huo kwa niaba ya wenzao wote wa mkoa wa Simiyu Septemba 10, 2019.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akifurahia jambo na  wanafunzi wa darasa la Saba katika Shule ya Msingi Somanda A na B Mjini Bariadi wakiwa katika maandalizi ya Mtihani wa Taifa utakaofanyika Septamba 11-12, 2019, wakati akiwatakia heri katika mtihani huo kwa niaba ya wenzao wote wa mkoa wa Simiyu Septemba 10, 2019.


Baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Somanda A na B Mjini Bariadi wakimshika mkono Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kama ishara ya kupokea mkono wake wa heri kwao katika Mtihani wa Taifa utakaofanyika Septemba 11-12, 2019


Baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Somanda A na B Mjini Bariadi wakimshika mkono Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kama ishara ya kupokea mkono wake wa heri kwao katika Mtihani wa Taifa utakaofanyika Septemba 11-12, 2019
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Somanda A na B Mjini Bariadi wakishangilia mara baada ya kupokea salamu za heri ya Mtihani wa Taifa utakaoanza Septemba 11-12, 2019 kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati alipowatembelea Septemba 10, 2019 shuleni hapo kwa lengo la kuwatakia heri katika mtihani huo.
Afisa Elimu Msingi Halamashauri ya Mji wa Bariadi,  Mwl. Christopher Legonda akitoa neno la shukrani mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kuzungumza na wanafunzi wa darasa la Saba katika Shule ya Msingi Somanda A na B Mjini Bariadi wakiwa katika maandalizi ya Mtihani wa Taifa utakaofanyika Septemba 11-12, 2019, kwa lengo la kuwatakia heri katika mtihani huo kwa niaba ya wenzao wote wa mkoa wa Simiyu Septemba 10, 2019.
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Somanda A na B Mjini Bariadi wakiimba wimbo wa Tanzania Tanzania na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu =, Mhe. Anthony Mtaka wakati alipowatembelea Septemba 10, 2019 shuleni hapo kwa lengo la kuwatakia heri katika mtihani wa Taifa utakaofanyika Septemba 11-12, 2019.


0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!