Waziri wa viwanda,biashara na uwekezaji Mhe.
Charles Mwijage amesema serikali inaendelea kujenga uchumi wa Kitaifa(jumuishi)
ulio imara na wenye ushindani kuelekea uchumi wa kati ifikapo
2025 kwa kuanzia uzalishaji mashambani hadi sokoni.
Hayo ameyasema wakati akihitimisha
Maonesho ya (SIDO) Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi
Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, yakiwa na Kauli Mbiu: “PAMOJA
TUJENGE VIWANDA KUFIKIA UCHUMI WA KATI”
Mhe. Mwijage amezitaja baadhi ya sifa za
uchumi wa Kitaifa (Jumuishi) kuwa ni pamoja na Kipato cha wastani kwa Mtanzania
kufikia dola 3000 kwa mwaka ifikapo 2025, Watanzania kuwa na maisha mazuri,
watu kuwa na elimu na wepewi kwa kujifunza, pamoja na kuwa na uchumi imara ulio
shindani.
“Tunataka mwaka 2025 tuwe na uchumi
imara na shindani lakini tuendelee kudumisha amani na msihikamano; njia rahisi
ya kufikia mahali mbapo kipato cha wastani cha Mtanzania kuwa dola 3000 kwa
mwaka ni kupitia uchumi wa viwanda na uchumi wa viwanda ni zaidi ya viwanda,
uchumi wa viwanda unaanzia shambani hadi sokoni” alisema.
Katika hatua nyingine alitoa wito kwa
Watanzania kulinda viwanda vya ndani hapa nchini kwa kununua bidhaa zinazozalishwa
hapa nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Mhe. Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka amesema Mapinduzi ya viwanda yanatokana na Shirika la
Viwanda Vidogo (SIDO), hivyo ni vema wizara ya viwanda ,biashara na
uwekezaji ikaliwezesha shirika la kuhudumia viwanda vidogo ili
kutekeleza azma ya Tanzania ya viwanda.
Akizungumzia maonesho ya Viwanda vidogo
Mkurugenzi Mkuu wa SIDO Prof. Silvester Mpanduji, amesema jumla ya wajasiriamali
515 kutoka mikoa 23 nchini na nchi jirani za Uganda na Burundi, wameshiriki
manesho haya na kupata fursa ya kuonesha bidhaa wanazozalisha na kubadilisha
uzoefu katika masuala mbalimbali.
Aidha, amesema kupitia maonesho hayo
mashine za kuongeza thamani katika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu
zenye thamani ya zaidi ya shilingi 800 zimenunuliwa na nyingine kuwekewa ahadi
ya kununuliwa.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa UNDP anayeshughulikia
miradi Amoni Manyama ameahidi kuwa Shirika hilo liko tayari kushirikiana na
Serikali hapa nchini katika Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda kwa kutoa msaada wa kifedha
na utaalam wa kuchambua miradi ya viwanda katika Mkoa wa Simiyu na mikoa
mingine pia.
Maonesho ya Viwanda Vidogo SIDO Kitaifa
yaliyofanyika kwa muda wa siku sita katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu
yalifunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim
Majaliwa Oktoba 23, 2018, pamoja na wajasirimali 515 kushiriki takribani
taasisi za Umma na Binafsi 24 zimeshiriki maonesho haya.
MWISHO
PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI: https://simiyuregion.blogspot.com/2018/10/mwijage-viwanda-vidogo-biashara-ndogo.html
0 comments:
Post a Comment