Tamasha kubwa la michezo ambalo hufanyika
kila mwaka Mkoani Simiyu (Simiyu Jambo Festival) linatarajiwa kufanyika Juni
30, mwaka huu katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi huku takribani
shilingi milioni 32 zikishindaniwa.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo Juni 25, Mratibu wa tamasha hilo Bi. Zena Mchujuko amesema Mgeni
rasmi katika Tamasha hili anatarajiwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson.
Amesema katika Tamasha hilo
kutafanyika mashindano ya mbio za baiskeli wanaume na wanawake, mbio fupi
kilometa tano wanaume na wanawake na mashindano ya mdahalo kwa wanafunzi wa
shule za sekondari.
“Jumla ya shilingi milioni 32 zitashindaniwa
kwa michezo yote, mshindi wa kwanza mbio
za baiskeli kwa wanaume atapata 1,000,000, Wanawake 700, 000, walemavu
500, 000 na tutatoa zawadi mpaka kwa mshindi wa 25; ngoma za asili mshindi atapata 1,000,000”
alisema Bi. Zena
Aidha, amesema fomu za ushiriki zinapatikana kataika
ofisi ya Chama cha Baiskeli Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi na katika Tovuti: www.simiyutalent.co.tz
kwa gharama za shilingi elfu tano(5000) kwa mashindano ya baiskeli na shilingi elfu
mbili (2000) kwa ajili ya mashindano ya mbio fupi.
Katika hatua nyingine Bi. Mchujuko amesema kupitia
Tamasha la Simiyu Jambo Festival jamii ya watu wa Simiyu itapata ujumbe wa
kupinga mimba za utotoni jambo litakalopelekea watoto wa kike waweze kutimiza
ndoto zao kupitia Kauli Mbiu ya Tamasha ambayo ni :-WEZESHA MTOTO WA KIKE ATIMIZE
NDOTO ZAKE, INAWEZEKANA KUZUIA MIMBA KATIKA UMRI MDOGO”
Mratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
Idadi ya watu Duniani(UNFPA) Mkoa wa Simiyu, Dkt. Amir Batenga amesema shirika
hilo limekuwa likishirikiana na Serikali katika jitihada za kupunguza vifo
vitokanavyo na uzazi, ambapo waathirika wakubwa ni wasichana wenye umri mdogo,
hivyo anaamini kupitia Tamasha hilo wananchi watapata ujumbe mahususi wa
kukabiliana na mimba katika umri mdogo.
Naye Katibu wa Chama cha Mbio za Baiskeli Mkoa wa
Simiyu, Bw, Samwel Richard washiriki takribani 260 kutoka mikoa ya Simiyu, Shinyanga,
Mara, Mwanza, Geita na Kagera wanatarajia kushirikia mashindano ya baiskeli, huku
akiwahakikishia wananchi kuwa wachezaji wao wamejiandaa vizuri na wamekuwa
kambi kwa takribani wiki mbili.
Kwa upande wake Kiongozi wa Ngoma za Asili Mkoa wa
Simiyu, Bw. Buhimila Shala amesema kupitia ngoma za wagika na wagalu watatoa
ujumbe uliobebwa na Kauli mbiu ya Tamasha kwa lengo la kuwaokoa wasichana
kupata mimba katika umri mdogo.
Tamasha la Simiyu Festival mwaka
2019 limedhaminiwa na Jambo Food Products Company, Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani-UNFPA, NGM Gold Mine Limited, NGS Petroleum,
Alliance Ginneries Limited, Busega Mazao Limited, Maswa Standard Chalk, Ms
Hotel na Vetreces Company Limited.
MWISHO
Mratibu wa Tamasha la
Simiyu Jambo Festival Bi. Zena Mchujuko(kulia) akizungumza na waandishi wa
habari na kutoa taarifa ya tamasha hilo ambalo linatarajiwa kufanyika Juni 30,
2019 Mjini Bariadi.
Mratibu wa Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu Duniani(UNFPA) Mkoa wa Simiyu,
Dkt. Amir Batenga(kushoto) akizungumza na waandishi wa habari na kutoa taarifa
ya namna Shirika hilo liakavyotumia Tamasha la Simiyu Jambo Festival kupeleka
ujumbe wa Kupinga mimba za utotoni tamasha ambalo linatarajiwa kufanyika Juni 30,
2019 Mjini Bariadi.
Kiongozi wa Ngoma za
Asili, Bw. Buhimila Shala (kushoto) akizungumza katika Mkutano wa Waandishi wa
Habari na kueleza namna ngoma za asili
zitakavyopamba Tamasha la Simyu Jambo Festival ambalo linatarajiwa kufanyika
Juni 30, 2019.
Katibu wa Chama cha
Baiskeli Mkoa wa Simiyu, Bw. Samwel Richard(kulia) akizungumza na waandishi wa
habari juu ya namna chama hicho kilivyojiandaa na mashindano ya baiskeli katika
Tamasha la Simiyu Jambo Festival, linalotarajiwa kufanyika Juni 30, 2019
0 comments:
Post a Comment