Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Kilele cha Maadhimisho ya
Siku ya Wanawake Duniani ambayo Kitaifa yatafanyika katika Uwanja wa
Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake Mjini Bariadi
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Maadhimisho haya yanaongozwa
na kauli Mbiu "Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya Sasa na
ya baadaye" ambapo yataanza
tarehe 02 Machi 2020 mpaka tarehe 08 Machi 2020.
"Katika Maadhimisho haya tunawatarajia wageni mbalimbali na
shughuli mbalimbali kufanyika; mathalani kuanzia Tarehe 02 Machi 2020 maonesho
ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wanawake zitaoneshwa, wajasiriamali
kutoka maeneo yote nchini wamethibitisha kushiriki pia kutakuwa na upimaji kwa
magonjwa mbalimbali ya Wanawake,"
"Siku ya tarehe 06 Machi 2020 kutakuwa na Jioni ya mwanamke
ambapo wake za Viongozi waliopo madarakani na wastaafu na Watendaji mbalimbali
wa Taasisi watashiriki; mpaka sasa Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya
nne, Mama Tunu Pinda, Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Tanzania na viongozi
mbalimbali Wanawake wamethibitisha kushiriki, wakiongozwa na Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu," alisema
Mtaka.
Aidha, Mtaka ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu
kushiriki katika shughuli zote zitakazofanyika katika Wiki ya Maadhimisho
ya Siku ya Wanawake Duniani Kitaifa na kilele chake ambazo zitafanyika katika
Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Katika hatua nyingine Mtaka amesema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya siku
tatu Mkoani Simiyu kuanzia tarehe 06 Machi 2020 hadi 08 Machi 2020.
Amesema tarehe 06 Machi, 2020 Mhe. Makamu wa Rais atafungua Tawi
la Benki ya NMB katika Kata ya Nyashimo makao Makuu ya Wilaya ya Busega na
baadaye kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Tawi la Chuo cha Usimamizi (IFM),
katika Kata ya Sapiwi wilayani Bariadi.
Ameongeza kuwa tarehe 07 Machi, 2020 Mhe. Makamu wa Rais
atafungua Ofisi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ya Mkoa na siku hiyo hiyo
ataweka jiwe la msingi Ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Halmashauri ya Mji wa
Bariadi kilichopo Kata ya Somanda.
"Nitumie nafasi kuwaomba Wananchi wa Mkoa wa Simiyu
hususani katika maeneo yote ambayo Mhe. Makamu wa Rais atapita kujitokeza kwa
wingi kumsikiliza kwa kuwa katika maeneo yote ambayo Mhe. Makamu wa Rais
atafungua na kuweka mawe ya msingi miradi, atazungumza na wananchi,
" alisema Mtaka.
Mhe. Makamu wa Rais atahitimisha ziara yake Mkoani Simiyu tarehe
08 Machi kwa kuwaongoza wananchi katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya
Wanawake Duniani Kitaifa.
MWISHO
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza
na Waandishi wa habari(hawapo pichani) Ofisini kwake Mjini Bariadi, kuhusu Maadhimisho
ya Siku ya Wanawake Duniani Kitaifa yanayofanyika Mkoani Simiyu pamoja Ziara ya
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
0 comments:
Post a Comment