Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umefunga kambi ya
Kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha Sita iliyokuwa ikifanyika katika Shule ya
Sekondari ya Wasichana Maswa , ikiwa ni sehemu ya tahadhari dhidi ya Homa kali
ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona.
Akifunga kambi hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu,
Bw. Jumanne Sagini amesema uongozi wa mkoa umefikia hatua hiyo kuchukua
tahadhari kama ilivyoelekezwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa juu ya kuzuia
mikusanyiko ya watu wengi isiyo ya lazima katika kipindi hiki ambacho
kumeripotiwa idadi ya watu kadhaa kubainika kuwa na virusi vya Corona katika
nchi mbalimbali.
“Kutokana na Maelekezo ya Serikali Mkoa umeona kambi
hii ifungwe kwa ajili ya tahadhari dhidi ya Corona, Mhe. Rais amesitisha mbio za Mwenge wa Uhuru
kwa mwaka 2020, Mhe. Waziri Jafo amesitisha UMISETA na UMITASHUMTA na tahadhari
mbalimbali zimeendelea kutolewa na Serikali ikiwemo ya kuzuia mikusanyiko; sisi
hapa tuna wanafunzi takribani 1000 kutoka
shule 10 hivyo tumekubaliana kwa pamoja tuifunge kambi hii,” alisema Sagini.
Aidha, Sagini amesema pamoja na kambi za kitaaluma
kufungwa Mkoa utaendelea kusimamia utekelezaji wa mkakati wa taaluma wa mkoa
ili walimu, wanafunzi na wadau wengine wa elimu waweze kutimiza wajibu wao
kuhakikisha Mkoa unatimiza adhma yake ya kuwa miongoni mwa mikoa itakayofanya
vizuri katika mitihani yote ya Kitaifa.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.
Ernest Hinju amesema wanafunzi hao walitakiwa kukaa kambini muda wa wiki sita
kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa unaotarajiwa kufanyika mwezi Mei
2020, hivyo pamoja na kusitisha kambi hiyo walimu wamehimizwa kutimiza wajibu
wao katika ufundishaji na wanafunzi wametakiwa kwenda kusoma kwa bidii ili
kufikia lengo la Mkoa.
Awali akitoa elimu ya ugonjwa wa homa ya mapafu
unaosababishwa na virusi vya Corona kwa wanafunzi na walimu kabla ya kambi
kufungwa, Afisa Afya wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Reuben Malimi amesema ugonjwa huo hauna
tiba matibabu yanayofanyika yanazingatia dalili zinazoonekana kwa mgonjwa,
hivyo ni vema kila mmoja akachukua
tahadhari kwa kuzingatia maelekezo na elimu inayotolewa na wataalamu wa afya
katika maeneo mbalimbali.
Nao wanafunzi wa Kidato cha Sita wa Mkoa wa Simiyu
wameshukuru uongozi wa Mkoa kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona kwa kutoa
elimu kuhusu Corona kabla ya kufunga
kambi, huku wakieleza namna ambavyo kufungwa kwa kambi kunaweza kuathiri malengo
yao waliyojiwekea.
“Tunashukuru uongozi wa Mkoa kutoa elimu na kuchukua tahadhari ya Corona kwa kufunga
kambi ni hatua ya kutuhakikishia usalama, lakini kambi ilitusaidia kujua namna
ya kujibu maswali ya mtihani wa Taifa na kujifunza mada ngumu tulizoshindwa shuleni
kupitia kwa walimu mahiri, tutatumia muda huu kujisomea kwa bidii ili tufaulu vizuri
mtihani wa Taifa,” alisema Isack Ndassa kutoka Shule ya Sekondari Kanadi
Itilima.
MWISHO
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha Sita wakimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini(hayupo pichani) akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoani humo, kabla ya kufunga kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi hao jana ambayo ilikuwa ikiendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa kwa lengo la kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
Afisa Afya wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Reuben Malimi akitoa elimu ya tahadhari dhidi ya Homa ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Korona kwa wanafunzi wa kidato cha Sita mkoani humo waliokuwa katika kambi ya Kitaaluma shule ya Sekondari ya Wasichana ya Maswa, kabla ya kambi hiyo kufungwa jana ili kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha Sita wakimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini(hayupo pichani) akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoani humo, kabla ya kufunga kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi hao jana ambayo ilikuwa ikiendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa kwa lengo la kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju akitoa taarifa ya hali ya kambi ya kitaaluma kwa waanfunzi wa kidato cha sita mkoani humo, kabla ya kumkaribisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini kuzungumza na wanafunzi hao, kabla ya kufunga kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi hao jana ambayo ilikuwa ikiendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, kwa lengo la kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
Mwanafunzi wa kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Nyaranja wilayani Meatu Mkoani Simiyu, Ndebile Charles akizungumzia hali ya kambi ya kitaaluma, kabla ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini kuzungumza na wanafunzi hao na kufunga kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi hao jana ambayo ilikuwa ikiendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, kwa lengo la kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
Mmoja wa walimu mahiri katika Kambi ya Kitaaluma ya Kidato cha Sita iliyokuwa ikiendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, Mwl. Haruna Boniface akitoa maelezo juu ya kambi hiyo kabla ya kambi hiyo kufungwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini kwa lengo la kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
Baadhi ya walimu na
wanafunzi wakimfuatilia Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini(hayupo
pichani) akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita mkoani humo, kabla ya
kufunga kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi hao jana ambayo ilikuwa ikiendelea katika Shule ya
Sekondari ya Wasichana Maswa kwa lengo la kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
0 comments:
Post a Comment