Mkuu wa Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, Mhe. Benson Kilangi ametoa wito kwa wananchi na viongozi mkoani hapa kuona umuhimu wa kushiriki michezo kwa ajili ya kuimarisha afya.
Kilangi ameyasema hayo Novemba 28, 2020 katika Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, likihusisha mashindano ya baiskeli, mbio fupi , ngoma za asili na mashindano ya taaluma kwa wanafunzi wa shule za sekondari; alipokuwa akitoa salamu za Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka.
"Hii michezo tunayoifanya pamoja na kwamba ni burudani tunapaswa kuelewa kwamba michezo ni afya; ni wajibu wetu kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anashiriki michezo, siyo lazima iwe kama hii tu, hata nyumbani tunaweza kufanya mazoezi madogo madogo kama kukimbia, kuruka kamba na mengine kwa afya," alisema Kilangi.
Aidha, Kilangi aliongeza kuwa michezo ni ajira kwakuwa wapo watu wanajipatia vipato kupitia michezo na vile vile michezo ni biashara na inasaidia kujenga mahusiano na undugu katika jamii.
Akizungumzia Kauli Mbiu ya Tamasha la Simiyu Jambo Festival
mwaka 2020 inayosema, “WAWEZESHE WANAWAKE NA WATOTO WA KIKE
ILI KUWA NA DUNIA BORA” Kilangi
amesema ni vema watoto wa kike na wanawake wakawezeshwa kwa kuwa ni wakombozi
wa familia na ndiyo wanaorudisha maendeleo nyumbani kwa asilimia kubwa ikilinganishwa
na wanaume.
Katika hatua nyingine Kilangi ametoa rai kwa wadau
wakashirikiana na mkoa wa Simiyu kuona namna ya kuwa na matamasha yanayohusu
michezo, sanaa na utamaduni kuanzia ngazi ya wilaya, ili kuendelea kuujenga
Mkoa wa Simiyu katika nyanja mbalimbali.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga amesema kwa sasa Tamasha hilo limekuwa likishirikisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, huku akibainisha kuwa nia ya Mkoa ni kupata washiriki wa ndani na nje ya nchi ili litumike pia katika kutangaza na kukuza fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo Simiyu.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani ( UNFPA) ambao ndiyo wadhamini wakuu, Dkt. Amir Batenga amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na mkoa wa Simiyu katika masuala mbalimbali ya kuwawezesha watoto wa kike na wanawake katika nyanja mbalimbali kama kauli mbiu ya tamasha la Simiyu Jambo Festival mwaka 2020 inavyosema.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum (Vijana), Mhe. Lucy Sabo ameupongeza uongozi wa Mkoa kwa maandalizi mazuri na kutoa rai kuwa Tamasha la Simiyu Jambo Festival liwe endelevu kwa ajili ya kuinua vipaji kwa vijana na kuwahamasisha kushiriki katika utamaduni, sanaa na michezo.
Baadhi ya washiriki wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival ambalo linafanyika kwa mara ya tatu mkoani Simiyu, wamewashukuru waandaji kwa maandalizi mazuri na ambapo wamebainisha kuwa mwaka huu ulinzi umeimarishwa zaidi.
"Tunawapongeza waandaaji mwaka huu mashindano ni mazuri, Ulinzi umeimarika sana kuanzia tulipoanza, njiani kote mpaka tulipofika eneo la kumalizia, kwa hali ilivyokuwa hakuna ambaye angeweza kubebwa kwa namna yoyote ile ili kutafutiwa ushindi," alisema Paul Michael mshindi wa kwanza mbio za baiskeli wanaume kilomita 140.
Katika mashindano ya baiskeli washiriki kutoka mikoa ya Mwanza
na Shinyanga wameonekana kung'ara zaidi ambapo Paul Michael kutoka Shinyanga
ameibuka mshindi na kujinyakulia kitita cha shilingi 800,000/= na Laurencia
Luzuba ameongoza upande wa wanawake na kujinyakulia shilingi 600,000/= , upande
wa walemavu Emmanuel John kutoka Simiyu ameibuka kidedea na kujipatia kitita cha
shilingi 200,000/=
MWISHO.
Paul Michael kutoka mkoani
Shinyanga akishengilia baada ya kuibuka mshindi wa kwanza mbio za baiskeli
kilomita 140 wanaume katika Tmasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba
28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu,
Bibi. Miriam Mmbaga(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washindi nane wa
kwanza katika mashindano ya mbio za baiskeli kilomita 80 wanawake, wakati wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika
Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Baadhi ya viongozi, watumishi na
wananchi wa mkoa wa Simiyu wakikimbia mbio fupi za kilomita tano katika
ufunguzi wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020
katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.
Benson Kilangi (katikati walioketi) ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo(kushoto), Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu,
Bibi. Miriam Mmbaga na washindi nane wa mbio za baiskeli kilometa 140 wanaume,
wakati wa Tamasha la Simiyu Jambo
Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa
Bariadi.
Kwiyeya Buluba mwanafunzi wa
Kidato cha kwanza kutoka shule ya sekondari Simiyu, akipokea zawadi ya fedha
taslimu kutoka kwa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi
(aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ), mara baada ya
kuibuka mshindi wa tatu katika uandishi wa isha, wakati wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika
Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Ngoma za asili kutoka kundi la
Wagalu wakitoa burudani wakati wa
Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika
Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Baadhi ya viongozi na watumishi
wa mkoa wa Simiyu wakiburudika na ngoma za asili zilizokuwa zikitoa burudani
wakati wa Tamasha la Simiyu Jambo
Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa
Bariadi.
Baadhi ya washiriki wa mashindano
ya mbio fupi kilomita 10 wanawake wakiondoka eneo la kuanzia mashindano hayo Salunda Mjini Bariadi, ambayo yamefanyika
wakati wa tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika
Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu,
ACP. Richard Abwao akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa mbio fupi
kilometa 10 wavulana, wakati wa tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika
Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Baadhi ya viongozi wa mkoa wa
Simiyu wakiwa katika picha ya pamoja na washindi watano wa mashindano ya
baiskeli kilometa tano walemavu, wakati wa tamasha la Simiyu Jambo Festival
liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Mbunge wa Viti maalum Vijana,
Mhe. Lucy Sabo akizungumza na wananchi wa mkoa wa Simiyu, wakati wa tamasha la
Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa
Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
TAZAMA PICHA MBALIMBALI ZA TUKIO LA SIMIYU JAMBO FESTIVAL