Saturday, November 28, 2020

WANANCHI SIMIYU WATAKIWA KUSHIRIKI MICHEZO KUIMARISHA AFYA

 

Mkuu wa Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, Mhe. Benson Kilangi ametoa wito kwa wananchi na viongozi mkoani hapa kuona umuhimu wa kushiriki michezo kwa ajili ya kuimarisha afya. 

Kilangi ameyasema hayo Novemba 28, 2020 katika Tamasha la Simiyu Jambo Festival lililofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, likihusisha mashindano ya baiskeli, mbio fupi , ngoma za asili na mashindano ya taaluma kwa wanafunzi wa shule za sekondari; alipokuwa akitoa salamu za Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka. 

"Hii michezo tunayoifanya pamoja na kwamba ni burudani tunapaswa kuelewa kwamba michezo ni afya; ni wajibu wetu kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anashiriki michezo, siyo lazima iwe kama hii tu, hata nyumbani tunaweza kufanya mazoezi madogo madogo kama kukimbia, kuruka kamba na mengine kwa afya," alisema Kilangi. 

Aidha, Kilangi aliongeza kuwa michezo ni ajira kwakuwa wapo watu wanajipatia vipato kupitia michezo na vile vile michezo ni biashara na inasaidia  kujenga mahusiano na undugu katika jamii. 

Akizungumzia Kauli Mbiu ya Tamasha la Simiyu Jambo Festival mwaka 2020 inayosema, “WAWEZESHE WANAWAKE NA WATOTO WA KIKE ILI KUWA NA DUNIA BORA” Kilangi amesema ni vema watoto wa kike na wanawake wakawezeshwa kwa kuwa ni wakombozi wa familia na ndiyo wanaorudisha maendeleo nyumbani kwa asilimia kubwa ikilinganishwa na wanaume.

 

Katika hatua nyingine Kilangi ametoa rai kwa wadau wakashirikiana na mkoa wa Simiyu kuona namna ya kuwa na matamasha yanayohusu michezo, sanaa na utamaduni kuanzia ngazi ya wilaya, ili kuendelea kuujenga Mkoa wa Simiyu katika nyanja mbalimbali.

 

Katibu Tawala wa  Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga amesema  kwa sasa Tamasha hilo limekuwa likishirikisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, huku akibainisha kuwa nia ya Mkoa ni kupata washiriki wa ndani na nje ya nchi ili litumike pia katika kutangaza na kukuza fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo Simiyu. 

Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani ( UNFPA) ambao ndiyo wadhamini wakuu, Dkt. Amir Batenga amesema  Shirika hilo litaendelea kushirikiana na mkoa wa Simiyu katika masuala mbalimbali ya kuwawezesha watoto wa kike na wanawake katika nyanja mbalimbali kama kauli mbiu ya tamasha la Simiyu Jambo Festival mwaka 2020 inavyosema. 

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum (Vijana), Mhe. Lucy Sabo ameupongeza uongozi wa Mkoa kwa maandalizi mazuri na kutoa rai kuwa Tamasha la Simiyu Jambo Festival liwe endelevu kwa ajili ya kuinua vipaji kwa vijana na kuwahamasisha kushiriki katika utamaduni, sanaa na michezo. 

Baadhi ya washiriki wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival ambalo linafanyika kwa mara ya tatu mkoani Simiyu, wamewashukuru waandaji kwa maandalizi mazuri na ambapo wamebainisha kuwa mwaka huu ulinzi umeimarishwa zaidi. 

"Tunawapongeza waandaaji mwaka huu mashindano ni mazuri, Ulinzi umeimarika sana kuanzia tulipoanza, njiani kote mpaka tulipofika eneo la kumalizia,  kwa hali ilivyokuwa hakuna  ambaye angeweza kubebwa kwa namna yoyote ile ili kutafutiwa ushindi," alisema Paul Michael mshindi wa kwanza mbio za baiskeli wanaume kilomita 140. 

Katika mashindano ya baiskeli washiriki kutoka mikoa ya Mwanza na Shinyanga wameonekana kung'ara zaidi ambapo Paul Michael  kutoka Shinyanga ameibuka mshindi na kujinyakulia kitita cha shilingi 800,000/= na  Laurencia Luzuba ameongoza upande wa wanawake na kujinyakulia shilingi 600,000/= , upande wa walemavu Emmanuel John kutoka Simiyu ameibuka kidedea na kujipatia kitita cha shilingi 200,000/=

MWISHO.

Baadhi ya waendesha baiskeli wanawake wakiondoka eneo la  kuanzia mashindano ya baiskeli kilomita 80 Salunda Mjini Bariadi, Mashindano yaliyofanyika wakati wa tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Paul Michael kutoka mkoani Shinyanga akishengilia baada ya kuibuka mshindi wa kwanza mbio za baiskeli kilomita 140 wanaume katika Tmasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga akimkabidhi zawadi ya fedha taslimu shilingi 600,000/= mshindi wa kwanza mbio za baiskeli kilomita 80 wanawake, Bi. Laurencia Luzuba kutoka mkoani Mwanza , katika Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washindi nane wa kwanza katika mashindano ya mbio za baiskeli kilomita 80 wanawake, wakati wa  Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.


Baadhi ya viongozi, watumishi na wananchi wa mkoa wa Simiyu wakikimbia mbio fupi za kilomita tano katika ufunguzi wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani (UNFPA) Dkt. Amir Batenga  akimkabidhi Emmanuel John  zawadi ya fedha taslimu shilingi 200,000/= baada ya kuibuka  mshindi wa kwanza katika mbio za baiskeli kilomita tano (kwa watu wenye ulemavu), wakati wa  Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi (katikati walioketi) ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo(kushoto), Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga na washindi nane wa mbio za baiskeli kilometa 140 wanaume, wakati wa  Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Kwiyeya Buluba mwanafunzi wa Kidato cha kwanza kutoka shule ya sekondari Simiyu, akipokea zawadi ya fedha taslimu kutoka kwa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi (aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ), mara baada ya kuibuka mshindi wa tatu katika uandishi wa isha, wakati wa  Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Ngoma za asili kutoka kundi la Wagalu wakitoa burudani wakati wa  Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Baadhi ya viongozi na watumishi wa mkoa wa Simiyu wakiburudika na ngoma za asili zilizokuwa zikitoa burudani wakati wa  Tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Baadhi ya washiriki wa mashindano ya mbio fupi kilomita 10 wanawake wakiondoka eneo la  kuanzia mashindano  hayo Salunda Mjini Bariadi, ambayo yamefanyika wakati wa tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP. Richard Abwao akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa mbio fupi kilometa 10 wavulana, wakati wa tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.


Baadhi ya viongozi wa mkoa wa Simiyu wakiwa katika picha ya pamoja na washindi watano wa mashindano ya baiskeli kilometa tano walemavu, wakati wa tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Mbunge wa Viti maalum Vijana, Mhe. Lucy Sabo akizungumza na wananchi wa mkoa wa Simiyu, wakati wa tamasha la Simiyu Jambo Festival liliofanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

TAZAMA PICHA MBALIMBALI ZA TUKIO LA SIMIYU JAMBO FESTIVAL

















 

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!