Zaidi ya wanamichezo 300 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini wanatarajia kushiriki Tamasha la Simiyu Jambo Festival ambalo litahusisha mashindano ya mbio za baiskeli, ngoma za asili(wagika na wagalu), mbio fupi (kilometa kumi) pamoja na mashindano ya kitaaluma kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival Bi. Zena Mchujuko wakati akizungumza na waandishi wa habari Mjini Bariadi leo Novemba 26, 2020 juu ya tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Novemba 28, 2020 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
“Zawadi
zitatolewa kwa mshindi wa kwanza mpaka wa kumi wanawake na wanaume (mbio za
baiskeli), walemavu zitatolewa kwa mshindi wa kwanza mpaka wa tano; mbio fupi
tutatoa kwa mshindi wa kwanza mpaka wa tatu,” alisema Bibi. Mchujuko.
Afisa
Miradi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu
Duniani (UNFPA) ambalo ndiyo mdhamini Mkuu wa Simiyu Jambo Festival, Bw. Dennis Swai amesema shirika hilo limeamua
kudhamini tamasha hilo kwa kuwa ni fursa mojawapo ya kuiweza jamii kutambua
haki za watoto wa kike na wanawake katika kufikia malengo yao, huku akiahidi kuwa wataendelea kushirikiana na
Serikali kama wadau wa maendeleo.
Kaimu
Katibu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Simiyu, Bw. Mbezi Ally amesema chama hicho
kimeandaa washiriki ambao ni wazuri katika mbio, ambapo amebainisha kuwa baadhi yao wameshiriki
mbio ndefu (kilomita 21 na Kilomita 42) ikiwemo Serengeti Safari Marathon na
kutoa wito kwa washiriki kutoka maeneo yote ndani na nje ya mkoa kushiriki
mashindano haya.
Mwakilishi
wa Mwenyekiti wa Mbio za Baiskeli Mkoa wa Simiyu, Bw. Buyaga George amesema
pamoja na washiriki kutoka mkoa wa Simiyu, washiriki kutoka mikoa ya Shinyanga,
Mwanza, Tabora na Arusha wamethibitisha kushiriki mashindano ya mbio za
baiskeli kwa wanaume (Kilomita 140) ,wanawake (kilomita 80) na walemavu
(kilomita tano).
Katibu
Tawala wa mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga amesema mkoa wa Simiyu ni maarufu
kwa kutumia baiskeli kama nyenzo ya usafiri hivyo mkoa umeona haja ya kuwaendeleza
wana Simiyu kwa utamaduni wao wa kutumia baiskeli ili waitumie fursa hiyo
kuingia katika mashindano yanayoweza kuwafanya wawe waendeshaji bora wa
baiskeli.
Aidha,
Mmbaga ametoa wito kwa wadau na wafanyabiashara mkoani hapa kushiriki katika
tamasha hili kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulitumia kutangaza huduma
na bidhaa zinazopatikana Simiyu.
Tamasha hili la Simiyu Festival linafanyika kwa mara
ya tatu sasa likiwa na Kauli Mbiu, “WAWEZESHE WANAWAKE NA WATOTO WA KIKE ILI
KUWA NA DUNIA BORA” chini ya udhamini wa UNFPA, Jambo Food Products, Alliance
Ginnery Ltd, Busega Mazao na SweetDreams Hotel,
Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment