Thursday, November 12, 2020

MTAFITI TPRI AAINISHA SABABU ZA VIUATILIFU KUSHINDWA KUUA WADUDU KWENYE PAMBA

Matumizi ya viuatilifu chini ya kiwango kilichoelekezwa, matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu,unyunyiziaji na utunzaji wa viuatilifu usio sahihi na uwezo mdogo wa wakulima kutambua visumbufu vya mazao,vimetajwa kuwa ni miongoni mwa sababu za viuatilifu kushindwa kuua wadudu katika zao la pamba. 

Hayo yamebainishwa na Mtafiti wa kudhibiti visumbufu vya mazao/mimea kutoka Taasisi ya Utafiti wa viuatilifu nchini(TPRI), Bw. Ramadhan Kilewa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya taaluma maalum kwa watoa huduma ya unyunyiziaji wa viuatilifu kwa zao la pamba mkoani Simiyu jana Novemba 11, 2020 mjini Bariadi.

“TPRI imeamua kabla ya msimu kuanza tuwajee uwezo wadau wetu ili wakafanye kazi nzuri itakayoleta tija katika uzalishaji wa pamba; tumeanza na wadau wanaofanya kazi mashambani ili tuwawezeshe kuwa na mbinu sahihi za kuchagua viuatilifu vilivyyo sahihi, utunzaji sahihi wa viuatilifu na utupaji wa viwekeo tupu kwa kufuata taratibu ili wasilete madhara kwa binadamu, wanyama na mazingira,” alisema Bw. Kilewa.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kutimiza takwa la kisheria la Sheria Namba 4 ya Afya ya Mimea ya mwaka 2020 sehemu ya 37 inayosisitiza mafunzo ya usimamizi na udhibiti wa viuatilifu ili kuhakikisha mazao yatokanayo na kilimo na mifugo yanayoweza kutumika na wadau nchini yawe safi na yasiwe na mabaki yenye madhara kwa afya binadamu.

Akifungua mafunzo hayo Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi, Miriam Mmbaga ametoa wito kwa watoa huduma ya unyunyiziaji wa viuatilifu kwa zao la pamba kutekeleza jukumu hilo kwa kuwasaidia wakulima kwa mujibu wa sheria na maelekezo waliyopewa huku akiwaasa kutowapotosha na kuwaibia wakulima.

Aidha, Mmbaga amezitaka Halmashauri zote mkoani Simiyu kuhakikisha zinaandaa maafisa Kilimo watakaowasimamia watao huduma hao na kusisitiza watoa huduma hao kutambulishwa kwa maafisa kilimo wa kata  na kwa wakulima wa pamba katika vijiji ili waeze kutambulika na kufikiwa kwa urahisi wanapohitajika kutoa huduma ya unyunyiziaji.

Kaimu Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Bibi, Kija Kayenze amesema, mara baada ya mafunzo haya matarajio mkoa ni kuongeza tija ya uzalishaji wa pamba mwaka huu kutoka wastani wa kilo 175 mpaka kilo 450 kwa ekari; ambapo amebainisha kuwa tija ndogo ilichangiwa na kukosa elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu.

Jumla ya vijana 600 mkoani Simiyu wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya taaluma maalum ya huduma ya unyunyiziaji wa viuatilifu kwa zao la pamba.

MWISHO

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga akifungua mafunzo ya taaluma maalum kwa watoa huduma ya unyunyiziaji wa viuatilifu kwa zao la pamba Tanzania jana Novemba 11, 2020 yanayofanyika kwa muda wa siku tatu mjini Bariadi hadi kufikia 13 Novemba 2020 TPRI, Gatsby Africa kwa kushirikiana na Mkoa wa Simiyu, ambayo yameandaliwa na TPRI, Gatsby Africa kwa kushirikiana na Mkoa wa Simiyu.

Mtafiti wa kudhibiti visumbufu vya mazao/mimea kutoka Taasisi ya Utafiti wa viuatilifu nchini(TPRI), Bw. Ramadhan Kilewa  akitoa maelezo ya awali katika mafunzo ya taaluma maalum kwa watoa huduma ya unyunyiziaji wa viuatilifu kwa zao la pamba Tanzania jana Novemba 11, 2020 yanayofanyika kwa muda wa siku tatu mjini Bariadi hadi kufikia 13 Novemba 2020 ambayo yameandaliwa na TPRI, Gatsby Africa kwa kushirikiana na Mkoa wa Simiyu. 

Baadhi ya watoa huduma ya unyunyiziaji wa viuatilifu kwa zao la pamba Tanzania wakimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo wa watoa huduma hiyo Mjini Bariadi jana Novemba 11, 2020 ambayo yameandaliwa na  TPRI, Gatsby Africa kwa kushirikiana na Mkoa wa Simiyu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi. Miriam Mmbaga akifungua mafunzo ya taaluma maalum kwa watoa huduma ya unyunyiziaji wa viuatilifu kwa zao la pamba Tanzania jana Novemba 11, 2020 yanayofanyika kwa muda wa siku tatu mjini Bariadi hadi kufikia 13 Novemba 2020 TPRI, Gatsby Africa kwa kushirikiana na Mkoa wa Simiyu, ambayo yameandaliwa na TPRI, Gatsby Africa kwa kushirikiana na Mkoa wa Simiyu.


0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!