Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba ametoa
wito kwa wakulima Mkoani Simiyu kuondokana na dhana potofu kuwa matumizi ya
mbolea yanazeesha ardhi badala yake wazingatie
matumizi sahihi ya mbolea katika kilimo
ili kuongeza mavuno, tija na uzalishaji katika kilimo.
Mhe. Mgumba ameyasema hayo Machi 06, 2019 wakati
akizungumza na wananchi wilayani Itilima Mkoani Simiyu, katika Mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Kijiji cha Bukingwaminzi kata ya Zagayu wilayani humo wakati
wa ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu.
Ameongeza kuwa siyo kweli kwamba matumizi ya mbolea
yanazeesha ardhi badala yake mbolea inasaidia kutibu ardhi na kupelekea
wakulima kuongeza mavuno na tija katika uzalishaji wa mazao na kuwawezesha
kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Nimeambiwa
hamtaki kutumia mbolea kwa madai kwamba mkitumia mbolea inazeesha ardhi siyo
kweli, mbolea hizi haziharibu ardhi yetu bali zinakwenda kutibu ardhi;ndiyo
maana watu wa Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya , Songwe, Rukwa na Katavi
wanaongoza kwa kuzalisha mahindi nchini wenzetu ni wajanja wanatumia Mbolea”alisema
Akizungumzia
suala la viuatilifu Mgumba amewahakikishia wakulima wa zao la pamba mkoani
Simiyu kuwa tayari bodi ya pamba imeshatoa chupa 1000 za viuatilifu/viuadudu
ambapo kila wilaya itapata chupa 200.
Katika
hatua nyingine Mhe. Naibu Waziri amezungumzia suala la bei ya pamba ambapo
amesema Serikali inaendelea kuandaa mazingira wezeshi kwa wanunuzi wa pamba wa
ndani na nje ya nchi kununua pamba ya wakulima kwa bei nzuri na kubainisha kuwa
utaratibu utakaotumika ni wa soko huria.
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga pamoja na kuomba pamba
iuzwe kwa bei ya soko huria na kuongezewa viuatilifu, ameomba maghala ya
kuhifadhia pamba yajengwe kupitia sehemu ya fedha inayotolewa na wakulima
katika Vyama vyao vya Ushirika ili pamba ihifadhiwe vizuri na tija ionekane.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi amesema jitihada zinaendelea
kufanyika kuwahamasha wakulima wote wa pamba kujiunga na vyama vya ushirika
ambapo amesema hadi sasa ni wakulima 11,700 kati ya 38,910 wako katika vyama vya ushirika vipavyo
56.
Nao
baadhi ya wananchi waliopata nafasi ya kuwasilisha maombi na kero zao kwa Naibu
Waziri wa Kilimo wameomba viuatilifu/viuadudu vilivyotolewa na bodi ya pamba viwafikie
wakulima kwa wakati.
Naibu Waziri Mgumba yuko mkoani Simiyu
katika ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua shughuli za kilimo na ushirika
zinavyoendelea na kukagua shughuli za miradi ya umwagiliaji akiwa Wilayani
Itilima amepata nafasi ya kuzugumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara.
MWISHO
Naibu Waziri wa Kilimo,
Mhe.Omary Mgumba akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu
katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Bukingwaminzi Kata ya Zagayu
wakati wa ziara yake wilayani humo Machi 06, 2019.
Naibu Waziri wa Kilimo,
Mhe.Omary Mgumba(kushoto) akiteta jambo na Mbunge wa Itilima Mhe. Njalu Silanga
wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika
Kijiji cha Bukingwaminzi Kata ya Zagayu wakati wa ziara yake wilayani humo
Machi 06, 2019.
Mbunge wa Itilima Mhe.
Njalu Silanga akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu
katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Bukingwaminzi Kata ya Zagayu
wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary Mgumba wilayani humo Machi
06, 2019.
Diwani wa Kata ya
Zagayu Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu akizungumza na wananchi katika Mkutano
wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Bukingwaminzi Kata ya Zagayu wakati wa ziara
ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary Mgumba wilayani humo Machi 06, 2019.
Mbunge wa Itilima Mhe.
Njalu Silanga(kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Bw. Marco Mtunga katika Mkutano wa hadhara uliofanyika
Kijiji cha Bukingwaminzi Kata ya Zagayu wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa
Kilimo, Mhe.Omary Mgumba wilayani humo Machi 06, 2019.
Mkuu wa Wilaya ya
Itilima, Mhe. Benson Kilangi akiwasilisha taarifa ya wilaya kwa Naibu Waziri wa
Kilimo, Mhe.Omary Mgumba wakati alipotembelea wilaya hiyo Machi 06, 2019.
Baadhi ya wananchi waliowasilisha kero zao kwa Naibu waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba katikati ni Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Silanga
0 comments:
Post a Comment