Friday, March 8, 2019

NAIBU WAZIRI MGUMBA AAGIZA TUME YA UMWAGILIAJI KUFANYA TATHMINI UJENZI WA BWAWA SKIMU YA UMWAGILIAJI MASWA


Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba amemuagiza Mhandisi wa Umwagiliaji Tume ya Umwagiliaji Kanda ya Mwanza, Ebenezer Kombe kufanya tathmini katika Skimu ya Umwagiliaji ya Kinamwigulu Wilayani Maswa, kuona kama kuna uwezekano wa kujenga bwawa, ili Serikali iweke mipango ya kujenga bwawa hilo kuwawezesha wananchi kulima bila kutegemea mvua.

Mhe. Mgumba ameyasema hayo wakati alipotembelea eneo la skimu hiyo na kupokea ombi kutoka kwa wananchi la kuomba kujengewa bwawa na kuboreshewa mundombinu mingine, wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua shughuli za kilimo na miradi ya umwagiliaji wilayani Maswa Machi 07, 2019.

Amesema mara baada ya kupokea taarifa ya tathmini itakayofanywa na wataalam wa umwagiliaji ikionekana katika eneo hilo Bwawa linaweza kujengwa Serikali itahakikisha inaweka  katika Mpango wa bajeti fedha kwa ajili ya bwawa hilo, ili kukidhi haja ya wananchi ya kulima kwa umwagilia kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.

“Mhandisi wa Umwagiliaji wa Kanda ni vizuri ukaja hapa na wataalam mkafanya tathmini kuona je inawezekana kujenga mabwawa hapa, baada ya tathmini tukishafahamu kuwa panafaa kujenga bwawa ndiyo tuweke katika mpango wa bajeti” alisema Mgumba.

Kwa uapnde wao Wananchi hao wamesema wakijengewa bwawa na kuboreshewa miundobinu umwagiliaji watakuwa na uhakika wa kulima bila kutegemea mvua angalau mara mbili kwa mwaka, ambapo pia wameomba kuwezeshwa zana bora za kilimo.

“Tunaiomba Serikali itujengee bwawa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili  kusudi tuwe tunalima mara mbili kwa mwaka badala ya kutegemea mvua peke yake” alisema mkulima wa Kinamwigulu

“Pamoja na ombi la kutujengea bwawa litakalotusaidia kulima misimu miwili kwa mwaka tunaomba pia Serikali ituletee mikopo ya matrekta ili tuweze kulima maeneo makubwa zaidi” alisema Charles Hege mkulima wa Kinamwigulu

Katika hatua nyingine Mhe. mgumba amesisitiza suala la Halmashauri kutenga asilimia 20 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo kwa kuwa zina mchango mkubwa katika mapato ya Halmashauri, badala ya kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi ya kutoa huduma pekee.

Awali akitoa taarifa ya Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe ameiomba Bodi ya Pamba kuwashirikisha viongozi wa Wilaya na Halmashauri katika kuandaa mwongozo wa ununuzi wa pamba, ili waweze kupata nafasi ya kutoa maoni yao kwa kuwa ni wadau muhimu na wasimamizi wakubwa katika uzalishaji wa zao hilo.

Akiwa Wilayani Maswa, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba ametembelea skimu ya umwagiliaji ya Kinamwigulu na shamba la pamba lenye ukubwa wa ekari tano linalomikiliwa na kikundi cha wanawake kiitwacho Upendo, kilichopo Kijiji cha Busamda.
MWISHO 

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe ( mwenye shati la bluu mbele) akimuongoza Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary Mgumba(katikati) na viongozi wengine alipotembelea Skimu ya Umwagiliaji ya Kinamwigulu wilayani humo wakati wa ziara yake Machi 07, 2019.



 Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba(mbele kulia) akitembelea shamba la kikundi cha wanawake cha Upendo kilichopo Kata ya Busangi wilayani Maswa, wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo Machi 07, 2019.
Mhandisi wa Umwagiliaji Kanda ya Mwanza, Mhandisi. Ebenezer Kombe(kushoto) akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe(katikati) na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea Skimu ya Umwagiliaji ya Kinamwigulu wilayani Maswa  akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo Machi 07, 2019.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mhe. Paulo Maige  mara baada ya kuwasili wilayani Maswa kwa ajili ya ziara yake ya kikazi Machi 07, 2019..
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba akisalimiana na wakina mama wa Kikundi cha Upendo kinachojishughulisha na shughuli za kilimo cha pamba wilayani Maswa, wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo Machi 07, 2019.




Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Maswa mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili ya ziara yake ya kikazi Machi 07, 2019.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa,Dkt. Seif Shekalaghe akiwasilisha taarifa ya Wilaya kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba (kushoto) wakati Naibu Waziri huyo akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo Machi 07, 2019.
Baadhi ya viongozi na wataalam wa Kilimo wa wilaya ya Maswa na Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba (hayupo pichani) wakati Naibu Waziri huyo akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo Machi 07, 2019.
Baadhi ya miundombinu ya Umwagiliaji katika Skimu ya Umwagiliaji Kinamwigulu wilayani Maswa mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba(kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt.Seif Shekalaghe  mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili ya ziara yake ya kikazi Machi 07, 2019.







0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!