Mkurugenzi Bodi ya Pamba nchini, Bw. Marco Mtunga amemwakikishia
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omari Mgumba kuwa mkoa wa Simiyu utapokea chupa
milioni tatu za viuadudu lengo likiwa kukabiliana na changamoto ya
wadudu waharibifu wa zao la hilo.
Mtunga ameyasema hayo wakati wa ziara ya Naibu Waziri
wa Kilimo, Mhe.Omari Mgumba mkoani Simiyu Machi 06, 2019 ambapo amebainisha kuwa
tayari bodi imeshasambaza chupa milioni moja na laki tatu za viuadudu hivyo kwa
mkoa huu na kuongeza Simiyu pekee itapokea chupa milioni tatu za
viuadudu kwa msimu huu.
“Mpaka sasa chupa milioni moja zimeshafika Mwanza kwa
ajili ya Mkoa wa Simiyu kila wilaya itapata chupa laki mbili, awali tulishagawa
chupa milioni moja na laki tatu; kutokana na pamba iliyomwa kwa wingi Simiyu lengo
letu ni kuipa Simiyu chupa milioni tatu kati ya chupa milioni nane
tutakazosambaza nchini msimu huu” alisema Mtunga
Aidha, Mtunga amesema Mkoa wa Simiyu uko katika nafasi
ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo la pamba kutoka kilo milioni 113 za msimu
uliopita mpaka kufikia kilo zaidi ya 300 msimu huu, kutokana na pamba ilivyolimwa
kitaalamu na uwepo wa idadi ya miche inayotakiwa kwa ekari.
Akiwa ziarani mkoani hapa Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary
Mgumba amesema suala la mbegu za pamba limeenda vizuri hivyo ni
vema likaenda sambamba na usambazaji wa viuadudu na kuongeza kuwa
wakulima wa zao hilo wameongezeka kutokana na zao hilo kufanya vizuri hususani
mkoa wa Simiyu ambao umeongoza kwa uzalishaji ikilinganishwa na mikoa mingine
inayolima pamba hapa nchini.
“Suala la mbegu lilienda vizuri lakini kubwa zaidi ni
mahitaji makubwa kuliko matarajio kutokana na hamasa mliyofanya mwaka jana watu
wengi walihamasika kulima pamba, hata mwaka huu wengi zaidi watakuwa wamelima,
maana wakulima wengi huwa wanahamasika kulima zao ambalo limefanya vizuri msimu
uliopita” alisema Mgumba.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka
amesema kuwa lengo la mkoa ni kuongeza uzalishaji kwa ekari kuanzia kilo 500
hadi 1000 kwa ekari badala ya kuongeza idadi ya wakulima pekee.
“Tungehitaji kuongeza uzalishaji kwa ekari badala ya
kuongeza uzalishaji kwenye idadi ya wakulima, mwaka 2018 tulivuna kilo milioni
113, mwaka huu uzalishaji utaongeza lakini unaweza kuongezeka kutokana na
ongezeko la wakulima na ekari zilizolimwa; wakati tunaweza kupata kilo kama
hizo kwenye pungufu ya ekari na idadi ya wakulima kama tutaongeza uzalishaji
kwa ekari”
“Msukumo wa Mkoa ni kuona tunaongeza uzalishaji kwa
ekari, ukienda Mwabusalu kuna wakulima wanazalisha kuanzia kilo 500 hadi 1000
kwa ekari , kwa hiyo kama mkoa tumejipanga kuhakikisha uzalishaji unaongezeka
kwa ekari na idadi ya wakulima pia inaongeza” alisema Mtaka.
Naibu Mgumba yuko mkoani Simiyu katika ziara ya kikazi
yenye lengo la kukagua shughuli za kilimo na ushirika zinavyoendelea pamoja, kukagua
shughuli za miradi ya umwagiliaji akiwa Wilayani Itilima amepata nafasi ya
kuzugumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara.
MWISHO
Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Bw. Marco Mtunga akizungumza na wadau mbalimbali wa kilimo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omary Mgumba mkoani humo Machi 06, 2019.
Naibu Waziri wa Kilimo,
Mhe.Omary Mgumba akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu na baadhi ya wadau wa kilimo, wakati wa ziara
yake mkoani Simiyu Machi 06, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka (wa pili kushoto) akizungumza na wadau mbalimbali wa kilimo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa
Kilimo, Mhe.Omary Mgumba mkoani humo Machi
06, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka akizungumza viongozi wa mkoa na wadau mbalimbali wa kilimo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa
Kilimo, Mhe.Omary Mgumba mkoani humo Machi
06, 2019.
Baadhi ya viongozi na
wadau wa Kilimo mkoani Simiyu wakiwa katika kikao na Naibu Waziri wa Kilimo,
Mhe.Omary Mgumba wakati wa ziara yake mkoani humo Machi 06, 2019.
0 comments:
Post a Comment