Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary
Mgumba amewataka wakulima wa pamba kata ya Mwabusalu wilayani meatu
Mkoani Simiyu iliyochaguliwa kuzalisha mbegu za pamba kuzingatia kanuni za
kilimo bora lengo likiwa kupata mbegu bora zitakazotumika katika maeneo
yanayolima zao hilo hapa nchini.
Ameyasema hayo akiwa kwenye ziara
ya kikazi wilayani hapo yenye lengo la kukagua shughuli za kilimo,
kusikiliza kero za wakulima katika kujiletea maendeleo wakati akiongea kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya mwabusalu iliyopo wilayani
hapo.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa
Kilimo Mgumba, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani amesema
kuwa bado wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima waliopewa dhamana ya kuzalisha
mbegu za pamba kutochanganya mazao huku akiongeza kuwa mbegu hiyo itazalishwa
ya kutosha.
“Mbegu inazalishwa hapa Mwabusalu na
baadaye inapelekwa maeneo mengine yanayolima pamba nchini, isingependeza kukawa
na maotea kwenye eneo ambalo limepewa dhamana ya kuzalisha mbegu, tunaendelea kuwaelimisha
wakulima na kuhakikisha kuwa maotea yasiwe sehemu ya pamba itakayonunuliwa kwa
ajili ya mbegu” alisema Dkt. Chilongani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mkuu wa
Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga amemuomba Mkuu wa Wilaya ya
Meatu na Kamati yote ya Ulinzi na Usalama isimamie operesheni ya kuondoa maotea
kwenye mashamba ya pamba iliyokuwa imesitishwa ili kulinda ubora wa mbegu na
mfumo wa kuzalisha mbegu za pamba.
“Tulikuwa tunaendesha operesheni ya
kuhakikisha mashamba yote ya kuzalisha mbegu hapa Mwabusalu yanazingatia
taratibu za kuzalisha mbegu, ilisitishwa kutokana na vitisho vya wana Mwabusalu
kutaka kuwapiga waliokuwa wakipita kwenye mashamba kuondoa maotea, Mhe. DC
kuanzia kesho Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya isimamie zoezi hili ili
tusipoteze mfumo wa kuzalisha mbegu bora” alisema Mtunga”
Baadhi ya wakulima wa pamba katika Kata
ya Mwabusalu wameiomba Serikali kuendelea kuwapata pembejeo kwa wakati na kutoa
wito kwa viongozi wa kisiasa kuwaongoza katika kuzingatia kanuni za kilimo bora
badala ya kuwapotosha ili waweze kulima
kwa tija na kutoka kwenye umaskini.
“Ninaomba Serikali iendelee kutoa madawa
na mbolea kwa wakati ili tuweze kuzalisha kwa tija maana mwaka huu tumeongeza
uzalishaji na tunatarajia mavuno mengi kwa kuwa pamba haijashambuliwa sana na
wadudu kama mwaka jana” alisema Charles Thomas mkulima Mwabusalu
“Baadhi ya viongozi wa kisiasa waache kuhubiri
habari mbaya kwenye kilimo cha pamba maana hawahubiri suala la kufuata sheria,
mfano wanapotuambia tuchanganye pamba na mazao mengine wakati wataalam wanasema
haitakiwi je wanatusaidia kutoka kwenye umaskini au wanataka tuendelee kuwa
maskini” alisema Bupolo Mahangi
Akijibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa
kwenye mkutano huo Naibu Waziri Mgumba amewataka baadhi ya wanasiasa kuwa
sehemu ya kutoa elimu na kuwaongoza wakulima hao kuzingatia kanuni za kilimo
bora ili waweze kulima kwa tija, kuzalisha mbegu bora na kuongeza mavuno.
Naibu Mgumba jana amemaliza ziara
yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Simiyu kwa kutembelea mradi wa
kilimo cha umwagiliaji, kutembelea mashamba ya pamba na kuzungumza na wananchi
wilayani Maswa, akiwa wilaya Meatu alitembelea shamba la kuzalisha mbegu za
pamba na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo la Mwabusalu lililopo wilayani
hapo.
MWISHO
Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary
Mgumba akitembelea moja ya shamba la mfano la pamba katika Kata ya Mwabusalu
Wilayani Meatu, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi Machi 07, 2019 wilayani humo
Naibu Waziri wa kilimo, Mhe. Omary
Mgumba akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Kijiji cha Mwabusalu wilayani Meatu, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi Machi
07, 2019 wilayani humo.
0 comments:
Post a Comment