Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani
Kitaifa mwaka 2019 yanatarajiwa kufanyika kesho katika Uwanja wa Halmashauri
ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, ambapo Mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile
akimwakilisha Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewakaribisha
wakunga wote hapa nchini na kuwahakikishia kuwa Mkoa umefanya maandalizi
ya kutosha ili maadhimisho hayo yaweze kufana.
"Nitumie nafasi hii kama Mkuu wa
Mkoa kuwaalika familia ya Wakunga wote Tanzania ambao wameanza safari kuja
kwenye shughuli yao ya Kitaifa ndani ya mkoa wetu, niwahakikishie kuwa
tumefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha shughuli yao inaenda vizuri"
alisema Mtaka
Katika hatua nyingine Mtaka amelishukuru
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu Duniani (UNFPA)
kuwa sehemu ya kuwezesha Maadhimisho hayo Kitaifa kufanyika Mkoani Simiyu, pamoja na mchango mkubwa wa Shirika hilo na wadau
wengine katika sekta ya afya ndani ya Mkoa.
Naye Makamu Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA
hapa nchini, Dkt.Hashina Begum amesema Kauli Mbiu ya Siku ya Wakunga Duniani
mwaka 2019 inayosema"Wakunga ni Watetezi wa Haki za Wanawake" inakumbusha
umuhimu wa wakunga katika kuwatetea kina mama wakati wa ujauzito, wakati wa
kujifungua na baada ya kujifungua.
Ameongeza kuwa UNFPA imeendelea
kushirikiana na Serikali katika ukarabati wa vituo 38 vya afya, wodi za
wazazi na vyumba vya upasuaji, ununuzi wa vifaa na mashine za kumwezesha
Mkunga kutoa huduma ya mama na mtoto kwa urahisi na kuwajengea uwezo wakunga 90
kutoka vituo vilivyokarabatiwa kutoa huduma za dharura kwa mama na mtoto.
Naye Rais Chama Cha Wakunga Tanzania
(TAMA), Feddy Mwanga amesema TAMA inafanya kazi na Mkoa wa Simiyu kutoka mwaka
2016 kuwaelimisha Wakunga, ili waweze kutoa huduma za dharura kwa mama na mtoto
hususani katika vituo vya pembezoni, huku akiishukuru UNFPA kwa mchango wake
kifedha na utaalamu kuwezesha mafunzo hayo.
Ameongeza kuwa Dira ya TAMA ni kuona kuwa
kila mama mjamzito anayejifungua na watoto wachanga wanahudumiwa na Wakunga
wataalam na wanapata huduma bora, huku akitoa wito wananchi wa Simiyu
kujitokeza kwa wingi katika Maadhimisho hayo ili waweze kupata huduma za
upimaji bila malipo.
MWISHO.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(katikati) akizungumza na waandishi wa
habari ( hawapo pichani) juu ya
Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo Kitaifa yatakayofanyika kesho Mei
05, 2019 Mkoani Simiyu katika uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Baadhi ya waandishi wa habari wa mkoa wa Simiyu
wakiwa katika Mkutano na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo
pichani) uliolenga kutoa taarifa juu ya Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo Kitaifa yatakayofanyika
kesho Mei 05, 2019 Mkoani Simiyu katika uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Makamu Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA hapa nchini, Dkt.Hashina Begum(wa pili
kushoto) akitoa taarifa mbele ya waandishi wa habari juu ya Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo Kitaifa
yatakayofanyika kesho Mei 05, 2019 Mkoani Simiyu katika uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Rais Chama Cha Wakunga Tanzania (TAMA), Feddy Mwanga(katikati)
akizungumza kwa niaba ya Chama hicho mbele ya mbele ya waandishi wa habari juu
ya Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo Kitaifa yatakayofanyika kesho
Mei 05, 2019 Mkoani Simiyu katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
0 comments:
Post a Comment