Aliyekuwa Katibu
Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amemkabidhi rasmi ofisi mrithi
wake Bi. Miriam Mmbaga ambaye aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Julai 03, 2020 kuchukua nafasi hiyo.
Makabidhiano hayo
yamefanyika Julai 08, 2020 mjini Bariadi na kushuhudiwa na baadhi ya viongozi
wa Chama na Serikali, viongozi wa dini, wakuu wa mashirika na taasisi za umma
na binafsi pamoja na watumishi.
Akizungumza kabla
ya makabidhiano hayo Sagini amemshukuru Mhe. Rais kwa kumuamini na kumteua ili
aweze kuwatumikia wananchi kwa nafasi ya Katibu Tawala wa Mkoa huku
akiwashukuru viongozi, watumishi na wananchi wa mkoa wa Simiyu kwa ushirikiano
waliompatia katika kipindi chote alichokuwepo Simiyu.
“Namshukuru sana
Mhe. Rais kwa imani yake kwangu nakumbuka mwezi Desemba 2015 alipoteua Makatibu
Wakuu, makatibu wakuu tisa tuliachwa tukapangiwe kazi nyingine lakini baada ya
muda akaniteua kuwa katibu tawala wa mkoa, nakumbuka katika wale tisa ni mimi
peke yangu ndiyo niliteuliwa kuwa katibu tawala wa mkoa; hii ni imani kubwa
sana kwangu,” alisema Sagini.
Aidha, Sagini
ametoa wito kwa viongozi, watumishi na wananchi na wadau mbalimbali wa mkoa wa
Simiyu kumpa ushirikiano Katibu Tawala mpya wa mkoa kama walivyokuwa wanampa
yeye ili aweze kutimiza wajibu na majukumu yake kama inavyotakiwa.
Wakizungumzia
aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini viongozi wa
serikali, chama, wakuu wa taasisi na watumishi wamesema Sagini alikuwa kiongozi
na mwalimu wao katika utendaji kazi wao huku wakibainisha kuwa amewasaidia
katika utatuzi wa changamoto mbalimbali za kiutendaji.
“Sagini tumeshirikiana
naye katika kipindi chote tulichokuwa pamoja naye, amefanya kazi iliyoacha alama
kwenye mkoa hata zawadi alizopewa hapa ni moja ya alama za kazi yake nzuri,
tunamtakia kila la heri; nitumie nafasi hii pia kumkaribisha RAS wetu mpya mimi
na wenzangu tunakuhakikishia kukupa ushirikiano,” alisema Mhe. Anthony Mtaka Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu.
“Binafsi kaka
yangu Sagini alikuwa si kiongozi tu bali mwalimu kwangu amenifundisha vitu vingi sana maana
mimi nimefanya kazi muda mfupi sana serikalini, miaka mingi nimefanya kazi
katika sekta binafsi na nilikuwa sijui mambo mengi , yeye ndiye aliyenielekeza namna
sahihi ya kutekeleza majukumu yangu,” alisema Mkuu wa wilaya ya Busega Mhe.
Tano Mwera.
“Tunampongeza
ndugu yetu Sagini kwa namna alivyokiunganisha Chama Cha Mapinduzi na watendaji
wa Serikali kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa mawasiliano na mahusiano kati
yetu sasa hivi yameimarika sana; pia nampongeza
kwa namna alivyokuwa mwepesi kushughulikia changamoto za watumishi,
wananchi na viongozi wa chama alizokuwa anapelekewa,” katibu wa itikadi na
uenezi CCM Mkoa wa Simiyu, Bw. Mayunga George.
Kwa upande wake
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga amemshukuru Mhe. Rais kwa
kumteua kushika nafasi hiyo huku akiahidi kushirikiana na wadau wote kuendelea kuleta matokeo chanya katika mkoa
ili uendelee kuwa mkoa bora ndani ya nchi na Afrika Mashariki na watu wengine
wajifunze Simiyu.
Aidha, Bi. Mmbaga
ametoa wito kwa watumishi kuzingatia nidhamu katika utumishi wao kwa kufuata sheria,
kanuni na taratibu na kuwataka kila mmoja atimize wajibu wake huku akibainisha
kuwa kila mtu akitimiza wajibu wake kero mbalimbali za wananchi zitatatuliwa na
rasilimali za umma zitaokolewa.
Bw. Jumanne Sagini
alikuwa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa pili tangu mkoa wa Simiyu uanzishwe mwaka
2012 na alikabidhiwa rasmi ofisi na mtangulizi wake Bi. Mwamvua Jilumbi Mei 02,
2016.
MWISHO
Aliyekuwa
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini (kushoto) akimkabidhi
Katibu Tawala mpya wa Mkoa huo, Bi. Miriam Mmbaga nyaraka mbalimbali ikiwa ni
ishara ya makabidhiano ya Ofisi yaliyofanyika mjini Bariadi 08 Julai, 2020.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (katikati), Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga (kulia) na aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini wakiwa na zawadi ya unga uliotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa , ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa Bw. Sagini katika maendeleo ya viwanda wilayani Maswa, mara baada ya makabidhiano ya Ofisi kati katibu Tawala wa Mkoa Mpya na anayeondoka, 08 Julai, 2020.
Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Jumanne Sagini akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu kabla ya kufanya makabidhiano ya ofisi kati yake na Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga 08 Julai, 2020.
Kutoka kushoto walioketi aliyekuwa Katibu Tawala wa
Mkoa, Bw. Jumanne Sagini, Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam
Mmbaga na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakiwa katika picha ya
pamoja na wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala wa wilaya
na viongozi wa dini, mke na mtoto wa Bw. Sagini kabla ya makabidhiano kati ya
Bw. Jumanne Sagini na Bi. Miriam Mmbaga
08 Julai, 2020.
Katibu Tawala mpya wa Mkoa, Bi. Miriam Mmbaga
akizungumza na viongozi wa Chama na Serikali, wakuu wa taasisi na mashirika ya
umma na binafsi, viongozi wa dini na watumishi katika hafla ya makabidhiano ya
ofisi kati yake na aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne
Sagini, 08 Julai, 2020.
MATUKIO KATIKA PICHA MAKABIDHIANO YA OFISIKATI YA ALIYEKUWA KATIBU TAWALA WA MKOA WA SIMIYU, BW. JUMANNE SAGINI NA MRITHI WAKE MIRIAM MMBAGA
MATUKIO KATIKA PICHA MAKABIDHIANO YA OFISIKATI YA ALIYEKUWA KATIBU TAWALA WA MKOA WA SIMIYU, BW. JUMANNE SAGINI NA MRITHI WAKE MIRIAM MMBAGA
0 comments:
Post a Comment