Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka nchini (DPP), Bw. Biswalo Mganga amewasimamisha kufanya
kazi za mashtaka mawakili wa Serikali mkoani Simiyu, Amani Kirua na Twahab
Yahaya kwa tuhuma za kuwaachia huru watuhumiwa saba wa mauaji ya
bibi kikongwe Nchambi Sing’hini mkazi wa
kijiji cha Kinamwigulu wilayani Maswa kinyume na taratibu.
DPP ameyasema hayo Julai
10, 2020 mjini Bariadi wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo pia
amemuagiza naibu mkurugenzi wa mashitaka kuwachukulia hatua za kinidhamu haraka;
huku akibainisha kuwa mawakili hao hawataenda mahakamani wala kupewa majalada
ya mashtaka wakati taratibu za kinidhamu zikiendelea.
“Kuanzia leo mawakili
hawa nimewasimamisha kufanya kazi za mashtaka yaani hawataenda mahakamani wala
hawatapewa jalada lolote,wakati taratibu za kinidhamu zikiendelea, wakati huo
huo jeshi la polisi liendelee kuchunguza kujua ukweli juu ya ‘involvement’ (ushiriki)
yao, nkama kuna rushwa na mambo mengine yoyote yamefanyika,” alisema DPP Mganga.
Aidha, DPP Mganga
amesema yapo maelekezo yanayopaswa
kufuatwa na mawakili kabla ya kufuta
kesi ambayo ni pamoja na kuandika kwenye jalada sababu zilizofanya kesi ifutwe na
mkuu wa mashtaka katika eneo husika kutoa kibali cha kesi kufutwa, ambayo yote
yalionekana kutozingatiwa katika ufutaji wa kesi hiyo.
Katika hatua nyingine
DPP Mganga amelitaka jeshi la polisi liendelee kuwatafuta watuhumiwa wa mauaji
walioachiwa kinyume na taratibu na liwarejeshe mahakamani huku akibainisha kuwa
jeshi hilo limeshawakamata watuhumiwa wawili ambao hakuwataja majina kwa sababu
za kiupelelezi na watapelekwa mahakamani Julai 13, 2020.
Kwa upande wake
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga amesema serikali
haitawavumilia watumishi wa umma wanaokiuka taratibu kwa maslahi yao binafsi
hivyo itaendelea kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Mmbaga ametoa wito kwa wananchi kuwa na imani
na serikali yao na vyombo vyake kwa kuwa mifumo ya serikali ipo na inafanya
kazi huku akiwataka kuwa huru kutoa taarifa wakati wowote kupitia vyombo vya
ulinzi na usalama.
Mawakili wawili wa
Serikali waliosimamishwa kufanya kazi za mashtaka mkoani Simiyu wanatuhumiwa kuwafutia
watuhumiwa saba kesi ya mauaji namba moja ya mwaka 2019 ya mauaji ya bibi
kikongwe Nchambi Sing’hini, ambapo alibainika
kuwa watuhumiwa wawili walifutiwa kesi hiyo Desemba 31, 2019 na wakili Twahab Yahaya na
watano walifutiwa kesi hiyo Juni 17 mwaka huu na wakili Amani Kirua kinyume
cha taratibu.
MWISHO
Mkurugenzi Mkuu wa mashtaka nchini Bw. Biswalo Mganga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Julai 10, 2020 mjini Bariadi katika Ofisi ya Katibu Tawala wa mkoa wa Simiyu, juu ya hatua alizochukua kwa mawakili wawili wa serikali mkoani Simiyu ambao wanatuhumiwa kuwafutia kesi watuhumiwa wa kesi ya mauaji bila kuzingatia taratibu, (kushoto ) ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga.
Mkurugenzi Mkuu wa mashtaka nchini Bw. Biswalo Mganga(kulia)
akisikiliza maswali kutoka kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) Julai 10,
2020 Mjini Bariadi katika Ofisi ya Katibu
Tawala wa mkoa wa Simiyu, mara baada ya kuzungumza nao juu ya hatua alizochukua
kwa mawakili wawili wa serikali mkoani Simiyu ambao wanatuhumiwa kuwafutia kesi
watuhumiwa wa kesi ya mauaji bila kuzingatia taratibu, (kushoto) ni
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga
0 comments:
Post a Comment