Katika kutekeleza mpango Mkakati wa Mapinduzi ya
Kilimo cha Pamba wa miaka mitano (2019-2024) wa Mkoa wa Simiyu, mkoa unakusudia
kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma za ugani kwa lengo la kuongeza tija
katika uzalishaji kutoka kilo 175 kufikia kilo 600 kwa ekari ifikapo mwaka
2024.
Hayo
yamebainishwa na Katibu Tawala msaidizi sehemu ya mipango na uratibu Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Donatus Weginah wakati akitoa mada katika mafunzo
ya maafisa ugani, maafisa ushirika na viongozi waandamizi wa wilaya na
Halmashauri juu utekelezaji wa mpango mkakati huo yaliyofanyika Julai 18, 2020
Mjini Bariadi.
Weginah
amesema kutokana na upungufu wa maafisa ugani wapatao 200 katika mkoa wa
Simiyu, mkoa unatarajia kutoa mafunzo ya muda mfupi ya kilimo bora cha pamba
kwa baadhi ya vijana ili waweze kuwasaidia wakulima kulima kilimo chenye tija hususani
katika maeneo ambayo hakuna maafisa ugani.
“Tunataka
kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa kilo 175 zinazozalishwa sasa hivi mpaka
kufikia kilo 600 kwa ekari ifikapo mwaka 2024, ili tuweze kufikia hapo ni
lazima tuhakikishe huduma za ugani ambazo ni changamoto zinapatikana, tutatumia
vijana ambao watapa mafunzo ya muda mfupi ili waweze kuwapatia elimu wakulima
wetu huko vijijini,” alisema Weginah.
Aidha,
Weginah amebainisha kuwa mafunzo yataanza kwa vijana wataohudumia Vyama vya
Msingi vya Ushirika (AMCOS) 26 vilivyochaguliwa kuwa maeneo ya mfano ya kuanzia
(pilot areas) kwa mwaka huu na baadaye kuanzia mwaka 2021 vijana hao
watapelekwa katika mkoa mzima hususani katika maeneo yenye upungufu mkubwa wa
maafisa ugani.
Afisa
ugani wa kata ya Chinamili wilayani Itilima, Bw. Gaudence Mlay amesema vijana
hao watakaopewa mafunzo pamoja na wakulima wawezeshaji watawasaidia maafisa
ugani katika utoaji wa elimu kwa wakulima na watawafikia wakulima wengi zaidi
kuliko ilivyo sasa ambapo katika baadhi ya maeneo afisa ugani mmoja anahudumia vijiji
vitatu mpaka vinne.
Kwa
upande wake Afisa Ushirika wa Halmashauri ya mji wa Bariadi, Bw. Billwater Mbilinyi
amesema mkakati wa mapinduzi ya kilimo cha pamba umeanza kutekelezwa kwa
kuwatambua wakulima, ukubwa wa maeneo wanayolima na mahitaji ya pembejeo jambo
ambalo litasaidia wakulima kupata kiasi cha pembejeo kinachotakiwa kwa wakati.
Wakati
huo huo Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Simiyu, Bw. Ibrahimu
Kadudu amesema katika utekelezaji wa mkakati huo mkoa wa Simiyu utahakikisha unasimamia
matumizi ya mizani za kidijitali ambazo zitatatua changamoto ya mizani
kuchezewa hivyo mkulima atapata kile anachostahili kupata wakati anapouza pamba
yake.
Awali
akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amesema
mpango mkakati huo umekuja katika kipindi muafaka huku akitoa wito kwa
wananchi, viongozi wa serikali, iongozi wa dini na wadau wengine wa pamba
kuunga mkono utekelezaji wa mkakati huu kwa manufaa ya mkoa na Taifa kwa
ujumla.
Kaimu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mhandisi, Mashaka Luhamba akifunga mafunzo
hayo amewataka washiriki wote wa mafunzo hayo kila mmoja akatimize wajibu wake katika
kutekeleza mkakati huo kwa lengo la kufikia matokeo yaliyotarajiwa ikiwa ni pamoja
na kuongeza tija ya kilimo cha pamba kwa
wakulima.
Mkakati wa Mapinduzi ya Kilimo cha Pamba wa miaka
mitano (2019-2024) wa Mkoa wa Simiyu ulizinduliwa rasmi tarehe 05 Machi 2020 na Naibu Waziri wa kilimo, Mhe.
Hussein Bashe, ambapo utekelezaji wake umeanza na Vyama vya msingi vya ushirika
(AMCOS) 26 na baadaye utatekelezwa
katika mkoa wote wa Simiyu.
MWISHO
Katibu Tawala
Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Bw. Donatus Weginah akitoa mada katika mafunzo ya viongozi na wataalam juu ya
utekelezaji wa mpango Mkakati wa Mapinduzi ya Kilimo cha Pamba wa miaka mitano
(2019-2024) wa Mkoa wa Simiyu yaliyofanyika Julai 17, 2020 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga (kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka) akifungua mafunzo ya viongozi na wataalam juu ya utekelezaji wa mpango Mkakati wa Mapinduzi ya Kilimo cha Pamba wa miaka mitano (2019-2024) wa Mkoa wa Simiyu yaliyofanyika Julai 17, 2020 Mjini Bariadi.
Afisa Tarafa kutoka wilayani Maswa akichangia hoja katika mafunzo ya viongozi na wataalam juu ya utekelezaji wa mpango Mkakati wa Mapinduzi ya Kilimo cha Pamba wa miaka mitano (2019-2024) wa Mkoa wa Simiyu, yaliyofanyika Julai 17, 2020 Mjini Bariadi.
Baadhi ya viongozi na watalaam wa kilimo na ushirika wakifuatilia mada iliyowasilishwa katika mafunzo ya viongozi na wataalam juu ya utekelezaji wa mpango Mkakati wa Mapinduzi ya Kilimo cha Pamba wa miaka mitano (2019-2024) wa Mkoa wa Simiyu yaliyofanyika Julai 17, 2020 Mjini Bariadi.
Baadhi ya viongozi na watalaam wa kilimo na ushirika wakifuatilia mada iliyowasilishwa katika mafunzo ya viongozi na wataalam juu ya utekelezaji wa mpango Mkakati wa Mapinduzi ya Kilimo cha Pamba wa miaka mitano (2019-2024) wa Mkoa wa Simiyu yaliyofanyika Julai 17, 2020 Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment