Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka
amewaongoza mamia ya waomboleaji kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mara, Mwanza,
Simiyu na nchi jirani ya Kenya katika mazishi ya aliyekuwa mwalimu na mwimbaji
wa Kwaya ya Kanisa la Wadventista Wasabato (SDA) Kurasini, Mwl.Samson Kibaso
ambaye pia ni mtunzi wa wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mazishi
hayo yamefanyika Juni 30, 2020 katika Kijiji cha Ingrichini Halmashauri ya
Wilaya ya Rorya Mkoani Mara na kuhudhuriwa na viongozi wa Kitaifa wa Kanisa la
SDA, Wachungaji kutoka konferensi mbalimbali za Kanisa hilo pamoja na viongozi
wa Serikali akiwemo Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mwita
Waitara .
Akizungumza
na waombolezaji, Mtaka amesema Mwalimu Samson Kibaso amefanya kazi kubwa ambayo
imeacha alama ya utumishi wake si tu katika Kanisa la Waadvenista Wasabato(SDA)
bali hata katika madhehebu mengine ambayo amefanya kazi nayo kupitia kazi yake
ya utunzi wa nyimbo.
“Yapo
maandiko yanasema hubirini kwa sauti ya kuimba, kupitia yeye (Kibaso) ameongoa
wengi, amegusa wengi, tuna wachungaji ambao wangeweza kufa ndani ya kanisa wanaofahamika
kimataifa lakini wasingetoka watu Kenya wakaja hapa; wote tunajua kuna shida ya
kusafiri lakini kuna watu kutoka Kenya wakasema lazima wafike kuona safari ya
mwisho ya huyu mtu mwema,” alisema Mtaka.
Aidha,
Mtaka amesema atakuwa tayari kushiriki katika mambo ambayo Kanisa litayafanya
kwa kumuenzi Mwalimu Samson Kibaso huku akibainisha kuwa heshima aliyopewa
Mwalimu Kibaso inabeba taswira ya namna kazi ya Kwaya ya Kurasini
inavyopokelewa na watu.
Katika
hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa wazazi na walezi katika Halmashauri ya
Wilaya ya Rorya kuthamini elimu kwa kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule
ili wapate elimu huku akisisitiza kuwa elimu ndiyo inaweza kuwawafanya
wakashindana na watu kutoka maeneo mengine.
Akitoa
mahubiri kabla ya mazishi ya Mwalimu Kibaso, Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato(SDA)
Jimbo la Kusini mwa Tanzania, Mch. Mark
Malekana amemzungumzia Kibaso kuwa alikuwa na mchango mkubwa kwa kanisa, mtu
mnyenyekevu pamoja na kipaji alichokuwa nacho, hivyo akatoa wito kwa waimbaji
na walimu wengine kuacha kiburi na kutumia vipaji vyao kwa utukufu wa Mungu.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Mwita Waitara
ametoa pole kwa familia, kwaya ya Kurasini na Kanisa la SDA na kubainisha kuwa
anatambua kazi kubwa iliyofanywa na Mwalimu Samson Kibaso hivyo atakuwa tayari
kushirikiana na familia, kwaya na kanisa katika kuenzi kazi zake.
Nao
wanakwaya wa Kwaya ya SDA Kurasini wamesema wamempoteza, nguli wa muziki,
mwalimu mahiri wa uimbaji na rafiki yao, huku wakiahidi kumuenzi kwa kuendelea
kumuimbia Mungu ili kupitia uimbaji wao watu waendelee kumuona Mungu.
Mwalimu Samson Kibaso alizaliwa mwaka 1956 na
amekuwa mwalimu wa kwaya ya SDA Kurasini tangu mwaka 1985, ambapo pamoja na
kuwa mwalimu katika Kwaya ya SDA Kurasini Kibaso pia amefundisha kwaya ya madhehebu
mbalimbali kama KKKT, Anglican na Moravian.
Pia alitunga na kufundisha nyimbo za taasisi
mbalimbali ikiwemo muhimili wa mahakama pamoja na kutunga wimbo wa jumuiya ya
Afrika Mashariki ambao mpaka sasa umekuwa ukiimbwa katika nchi zote zinazounda
Jumuiya hiyo.
MWISHO
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa
aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso
kabla ya mazishi yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini Halmashauri
ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Picha
inayomuonesha Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini marehemu mwalimu
Samson Kibaso akipiga gitaa enzi za uhai wake.Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso likishushwa kaburini wakati wa mazishi yake yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso kabla ya mazishi yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kulia) akiteta jambo na Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato(SDA) Jimbo la Kusini mwa Tanzania, Mch. Mark Malekana katika mazishi ya aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso, yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara(kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika mazishi ya aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso, yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akiimba na pamoja na baaadhi ya waimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini kabla ya mazishi ya aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya hiyo mwalimu Samson Kibaso, yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
0 comments:
Post a Comment