Shirika lisilo la Kiserikali la AMREF kupitia
mradi wa UZAZI UZIMA limetoa msaada wa vifaa kinga kuunga mkono Serikali katika
tahadhari dhidi ya maambukizi ya Virusi vya CORONA kwa mkoa wa Simiyu.
Akikabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi
ya shilingi millioni 23, Mratibu wa AMREF Kanda ya Ziwa, Bw. Gaspery Misungwi Julai 09, 2020 Mjini Bariadi, amesema Shirika hilo linatambua kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika
mapambano dhidi ya Corona hivyo kama wadau wameona waungane na serikali katika
kutokomeza kabisa janga hilo.
Aidha, Bw. Misungwi amevitaja vifaa hivyo kuwa
ni pamoja na mmipira ya kuvaa mikononi wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa,
barakoa,vitakasa mikono (ujazo tofauti), sabuni za maji za kunawia mikono(ujazo
tofauti) na ndoo kwa ajili ya kunawia mikono.
Akipokea msaada huo, Katibu Tawala wa Mkoa, Bi.
Miriam Mmbaga amelishukuru shirika hilo kwa msaada huo huku akibainisha kuwa
vifaa kinga hivyo havitatumika katika tahadhari dhidi ya corona peke yake maana
utakasaji unazuia magonjwa mengi.
Mmbaga ameongeza kuwa mkoa wa Simiyu uko tayari
kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau wote kwa kuzingatia sheria kanuni na
taratibu za Serikali kwa kuwa nia ya serikali ni kurahisisha utoaji huduma kwa
wananchi.
Katika hatua nyingine Mmbaga ameelekeza vifaa
hivyo vipelekwe katika maeneo yaliyokusudiwa na wala visipelekwe stoo.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt.
Khamis Kulemba amesema pamoja na AMREF kutoa vifaa kinga hivyo shirika hilo
limekuwa likisaidia katika ujenzi wa miundombinu hususani majengo ya upasuaji
katika baadhi ya vituo, uchimbaji wa visima Vya maji na katika huduma za afya
ya mama na mtoto.
Dkt. Kulemba
ameongeza kuwa kwa ushirikiano kati ya AMREF na serikali hali ya mahudhurio ya
wakina mama wajawazito kuhudhuria kliniki imeongezeka kufikia asilimia 80 na
wanawake kujifungulia katika vituo Vya kutolea huduma za afya.
MWISHO
Mratibu wa AMREF Kanda ya Ziwa, Bw. Gaspery Misungwi (wa pili
kulia) akikabidhi msaada wa vifaa kinga kwa ajii ya tahadhari ya maambukizi ya
virusi vya Corona mkoani Simiyu kwa Katibu Tawala wa mkoa huo, Bi. Miriam Mmbaga(wa
pili kushoto) Julai 09, 2020 Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment