Balozi
wa Indonesia hapa nchini Prof.Dkt. Ratlan Pardede amewaahidi viongozi wa Mkoa
wa Simiyu kuwa atawaalika wawekezaji wa Viwanda vya nguo, viwanda vya kuchakata
ngozi na viwanda vya kutengeneza mbolea kutoka nchini Indonesia kuja kuwekeza
Mkoani Simiyu.
Mhe.
Balozi Pardede ameyasema hayo Mei 15, alipokuwa katika ziara yake Mkoani Simiyu
mara baada ya kutembelea kiwanda cha Kuchambua pamba cha Kasoli Alliance kilichopo
Wilayani Bariadi na Kiwanda cha kuchakata ngozi cha Senani wilayani Maswa.
Amesema atawaalika
wafanyabiashara kutoka nchini Indonesia kuja Simiyu ili wakutane na viongozi wa
mkoa huo pamoja na wafanyabiashara wenzao kujadili juu ya kuongeza uzalishaji
wa pamba bora, bei ya pamba na kuona namna ya kuuza pamba ya Simiyu (Tanzania)
nchini Indonesia moja kwa moja.
Pamoja na kuahidi kuwaalika
wawekezaji wa viwanda vya kuchakata bidhaa za ngozi, Balozi Pardede akiwa
katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Senani Maswa ameahidi
kusaidia kuleta wataalam kutoka Indonesia watakaosaidia wafanyakazi wa kiwanda kutengeneza
bidhaa bora za ngozi na kuwapeleka wafanyakazi hao Indonesia kujifunza na kupata
maarifa na uzoefu.
Meneja mkuu wa Kiwanda cha
kuchambua pamba cha Alliance Bw. Boaz Ogola amesema ujio wa Balozi wa Indonesia
ni fursa kubwa kwa wanunuzi wa pamba kutokana na nchi hiyo kuwa na uhitaji
mkubwa wa pamba kwa ajili ya viwanda vya nguo na utafungua milango ya
majadiliano na wafanyanyabiashara wa Indonesia na kufanya biashara ya moja kwa
moja.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka amesema wamezungumza na Mhe.Balozi kumuomba awaalike wafanyabiashara
wa Indonesia Mkoani humo kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata ngozi, ili
viwanda vidogo vilivyopo na vitakapojengwa viwanda vikubwa uwekezaji wake uanze
na malighafi kutoka ndani ya mkoa.
Aidha, Mtaka amesema Simiyu kama
mkoa unaojihusisha na kilimo na unaopakana na mikoa inayofanya shughuli za
kilimo unaona ipo haja ya kuwa na wawekezaji wanaotengeneza mbolea jambo ambalo
limepokelewa na Mhe. Balozi na kuahidi kulifanyika kazi kwa kuwaalika
wawekezaji.
“Tumezungumza na Mhe. Balozi na
ameona uhitaji na umuhimu wa kuwakaribisha wawekezaji kulingana na mkoa jinsi
ulivyo, jambo hili la kupata wawekezaji kwenye uzalishaji wa mbolea lipo pia
katika mwongozo wetu wa uwekezaji kwa ajili ya kusaidia mikoa inayotuzunguka
kama sehemu ya kuboresha eneo la kilimo” alisema.
Wakati huo huo Mtaka amesema wamezungumza
na Mhe. Balozi kuona uwezekano wa kutoa nafasi kwa Mkoa wa Simiyu kuwa mwenyeji wa mkutano
kati ya Wizara ya Kilimo ya Indonesia na Wizara ya kilimo ya Tanzania ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu.
Mhe.Balozi alipata nafasi ya
kutembelea kiwanda cha Chaki wilayani Maswa, ambapo Mkuu wa Mkoa amesema
Serikali imetoa shilingi bilioni 8.2 kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda hicho na
ujenzi wa kiwanda cha vifungashio, hivyo akawataka vijana wanaofanya kazi
katika kiwanda hicho kufanya kazi kwa bidii ambapo amewahakikishia kuwa baada
ya upanuzi wa kiwanda hicho watakuwa waajiriwa wa kudumu.
Mhe. Balozi bado anaendelea na
ziara yake mkoani Simiyu ambapo amepata nafasi ya kutembelea kiwanda cha
kuchambua pamba Kasoli Alliance, Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi na
kiwanda cha chaki wilayani Maswa.
MWISHO
Balozi wa Indonesia
hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede (wa tatu kulia) akipewa maelezo juu ya
hatua za utengenezaji wa kiatu cha ngozi wakati alipotembelea kiwanda cha
kutengeneza bidhaa za ngozi kilichopo Senani wilayani Maswa akiwa katika ziara
yake Mkoani Simiyu.
Balozi wa Indonesia
hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede akiweka
saini katika ubao kwa kutumia Maswa Chalks wakati alipotembelea kiwanda cha
kutengeneza Chaki wilayani Maswa akiwa
katika ziara yake Mkoani Simiyu.
Balozi
wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede (wa tatu kushoto) akiwa na
viongozi wengine wa mkoa wa Simiyu wakati alipotembelea kiwanda cha kuchambua
Pamba cha Kasoli Alliance kilichopo wilayani Bariadi akiwa katika ziara yake Mkoani
Simiyu.
Meneja mkuu wa Kiwanda
cha kuchambua pamba cha Alliance Bw. Boaz Ogola(kushoto) akitoa maelezo kwa Balozi
wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede( wa nne kushoto) wakati alipotembelea
kiwanda hicho, kilichopo wilayani Bariadi
akiwa katika ziara yake Mkoani Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka(kulia) akiteta jambo na Balozi wa Indonesia hapa nchini,
Prof. Dkt. Ratlan Pardede wakati wa ziara yake katika wilaya ya Maswa mkoani
humo Mei, 15 mwaka huu.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa,
Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe (kulia), Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt.
Ratlan Pardede(katikati) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka
wakionesha boksi la Chaki za Maswa(Maswa Chalks) wakati wa ziara ya Balozi huyo
katika kiwanda cha kutengeneza Chaki wilayani humo.
Meneja
Mkuu wa Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Bw. Boaz Ogola(kulia) akitoa
maelezo kwa Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede wakati alipotembelea kiwanda hicho, kilichopo wilayani Bariadi akiwa katika ziara
yake Mkoani Simiyu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Enock Yakobo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Senani Wilaya
ya Maswa wakati wa ziara ya Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan
Pardede katika kiwanda cha kuchakata bidhaa za ngozi wilayani humo, akiwa
katika ziara ya siku nne Mkoani Simiyu.
Mwenyekiti wa Halmashauri
ya Wilaya ya Maswa, Mhe. Lucas Mwaniyuki akizungumza na wananchi wa Kijiji cha
Senani Wilaya ya Maswa wakati wa ziara ya Balozi wa Indonesia hapa nchini,
Prof. Dkt. Ratlan Pardede katika kiwanda cha kuchakata bidhaa za ngozi wilayani
humo, akiwa katika ziara ya siku nne Mkoani Simiyu.
Kikundi cha Ngoma ya
Asili cha Wagoyangi cha Wilaya ya Maswa kikitumbuiza wakati wa ziara ya Balozi
wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede wilayani humo, akiwa katika
ziara ya siku nne Mkoani Simiyu.
0 comments:
Post a Comment