Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
inatarajia kuanzisha vituo vya Elimu na huduma kwa walipakodi hivi karibuni, ambavyo vitawasaidia
walipakodi kupata ushauri wa masuala ya kodi pamoja na kujua haki na wajibu wao.
Hayo
yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Charles Kichere Mjini
Bariadi, wakati akizungumza na wafanyabiashara, Viongozi na watendaji wa Wilaya
na Mkoa Mkoani Simiyu, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Elimu
na Usajili kwa Walipakodi mkoani humo.
Kamishna Kichere amesema uamuzi wa TRA
wa kuanzisha vituo hivyo umelenga
kusogeza huduma karibu kwa walipakodi ambapo wafanyabiashara(walipakodi) watapata huduma za ushauri kuhusu masuala ya
kodi bila malipo katika vituo hivyo vitakavyokuwa nje ya Ofisi za TRA.
“Tunajua elimu ni muhimu sana kwa
walipakodi wetu, tunataka itolewe kwa walipa kodi kila siku siyo kwa misimu;
ili kusogeza huduma karibu hivi karibuni tutaanzisha vituo vya Elimu na Huduma
kwa walipakodi nje ya TRA, ambavyo vitatoa huduma ya ushauri kwa walipakodi
bure” alisema Kichere
Aidha, Kichere ametoa wito kwa
Wafanyabishara wa Mkoa wa Simiyu ambao ameutaja kama mkoa wenye fursa nyingi za
kibiashara kujitokeza kwa wingi kujisajili katika vituo vya elimu na usajili wa walipakodi, kupitia
zoezi linaloendelea mkoani humo ambalo limezinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa huo,
Mhe.Anthony Mtaka, Mei 08, 2018.
Ameongeza kuwa ni vema
wafanyabiashara wakatambua umuhimu wa kulipa kodi stahiki kwa wakati stahiki,
ili Serikali iendelee kutoa huduma bora kwa wananchi kupitia kodi hizo na
akasisitiza wafanyabiashara ambao bado hawajarasimisha biashara zao wajisajili na
kuanza kulipa kodi .
Wafanyabishara wa Mkoa wa Simiyu
wameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Simiyu kwa kufanya nao kazi kwa
ushirikiano na wakaomba changamoto mbalimbali zilizopo kufanyiwa kazi ili
waweze kutimiza wajibu wao kikamilifu kama walipakodi.
“ Tunaomba Ofisi ya Mkoa ya TRA
iboreshwe iendane na hadhi ya Mkoa, Wilaya zetu mpya za Busega na Itilima ziwe
na Ofisi za TRA ili kuwaondolea wafanyabiashara wenzetu shida ya kufuata huduma
katika wilaya nyingine na pia wafanyabiashara tunahitaji elimu ya mara kwa mara
kwenye masuala ya kodi” alisema Christina Matulanya Katibu wa TCCIA Simiyu.
“Tunaomba TRA waziangalie upya
sheria zao, lakini pia waangalie viwango vya kodi wanavyowakadiria wafanyabiashara ili viendane na hali halisi
ya biashara za Watanzania tulio wengi” alisema Davis Mateko Mfanyabiashara
kutoka Wilaya ya Busega.
Akizindua kampeni ya Elimu na Usajili
kwa walipakodi , Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka ameiomba TRA kutatua
changamoto za mashine za kutolea risiti (EFD), huku akitangaza dhamira yake ya
kuona biashara zinafanyika saa 24 katika Makao Makuu ya Wilaya na Baadhi ya
Vituo (Centres) vikubwa kuiwezesha TRA
kukusanya kodi zaidi.
Katika hatua nyingine Mtaka amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani
humo kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli la kuzingata maeneo ya wafanyabiashara wadogo wakati wa
Ujenzi wa Vituo vya Mabasi na akasisitiza wafanyabiashara wadogo kujisajili ili
waweze kupewe kipaumbele vituo hivyo vitakapojengwa.
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (wa pili kushoto)
akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Kampeni ya Elimu na Usajili wa Walipakodi Mkoani humo leo Mjini Bariadi, ambayo inaendeshwa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA).
Katibu wa Chama
cha Wafanyabiashara(TCCIA) Mkoa wa Simiyu, Bibi. Christina Matulanya akichangia
hoja mbele ya wafanyabiashara wenzake wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Elimu na
Usajili wa Walipakodi Mkoani humo ambao umefanyika leo mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Serikali pamoja na
Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Elimu na
Usajili wa Walipakodi Mkoani humo ambao umefanyika leo mjini Bariadi.
Katibu Tawala
Mkoa wa Simiyu, Bw.Jumanne Sagini akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Serikali pamoja na
Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Elimu na
Usajili wa Walipakodi Mkoani humo ambao umefanyika leo mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akipata maelezo kutoka kwa Afisa wa TRA kuhusu namna
Wafanyabiashara watakavyokuwa
wakisajiliwa , mara baada ya Uzinduzi wa Kampeni ya Elimu na Usajili wa
Walipakodi Mkoani humo ambao umefanyika leo mjini Bariadi.
Mfanyabiashara
Gungu Emmanuel Silanga akichangia hoja mbele ya wafanyabiashara wenzake wakati
wa Uzinduzi wa Kampeni ya Elimu na Usajili wa Walipakodi Mkoani Simiyu ambao umefanyika leo mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa
Chama cha Wafanyabiashara Wilaya ya Busega, Bw.Davis Mateko akichangia hoja
mbele ya wanyabiashara wenzake wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Elimu na
Usajili wa Walipakodi Mkoani Simiyu
ambao umefanyika leo mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment