Mwalimu
Akwilina Ernest Marenge kutoka Shule ya Msingi Salunda katika Halmashauri ya
Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, amepata zawadi ya shilingi 500,000/= kwa ajili ya
pongezi kwa kufanikiwa kutoa Alama A kwa wanafunzi 90 kati ya wanafunzi 147
katika Somo la Kiswahili katika mtihani wa Darasa la Saba mwaka 2017.
Fedha hizo
zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa mwalimu huyo
mbele ya baadhi ya viongozi wa mkoa huo, wanafunzi na walimu wengine wa
Shule ya Msingi Salunda.
Akikabidhi fedha hizo Mtaka amesema
Serikali imetambua juhudi za mwalimu huyo ambaye Katika somo lake la
Kiswahili alikuwa na ufaulu mzuri ambapo alitoa alama A 90, Alama B 55 na Alama
C 2, hivyo kama kiongozi ameona ni vema
mwalimu huyu akapewa motisha.
"Siku
ya Mei Mosi alipewa shilingi laki tano kama mfanyakazi hodari na mimi nikasema
nitampa shilingi 500,000 za kwangu siyo za Serikali, kama kiongozi niliona ni
jambo la kupongezwa, Fedha hii haifanani na alichofanya kwa watoto ila
najua wanafunzi wake watamkumbuka daima" alisema Mtaka.
Kwa upande
wake Mwl. Akwilina Marenge ambaye anatarajia kustaafu mwezi Juni mwaka 2018
amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa kutambua juhudi zake
na kuona umuhimu wa kumpongeza na akatoa wito kwa walimu wengine kujituma na
kupenda kazi yao.
Nao Walimu
wenzake na Mwalimu Akwilina wamempongeza na kubainisha kuwa anastahili
kupata zawadi zote hizo kwa kuwa pamoja na kuwa umri mkubwa amekuwa ni
mtu wa kujituma na kufanya kazi kwa bidii zaidi ya walimu vijana.
"Mwalimu
Akwilina ni mwalimu wa tofauti na walimu wengine, pamoja na kwamba yeye umri
wake umekwenda sana anawahi kazini, anaipenda kazi yake, anajituma kuliko hata
walimu vijana, ni mcheshi; hata sasa hivi tunavyosikia anaenda kustaafu
tunasikitika kwa sababu anaondoka mtu mchapakazi" alisema mwalimu Tabitha
Erasto.
"
Huyu mama ni mtu mzima lakini anajituma kuliko baadhi ya walimu vijana ni kitu
cha kushangaza mno, japo anaelekea kustaafu sisi wenzake tunaobaki
tunapaswa tuige mfano wake kwa kweli" Alisema Mwalimu Joyce Mishana.
Akitoa
shukrani kwa niaba ya walimu wengine Mwalimu Mkuu wa Shule ya Salunda, Mwl. Nchambi
Tupendane amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kwa kutambua mchango wa mwalimu
Akwilina na kubainisha kuwa zawadi hiyo imekuwa ni chachu kwao ya kufanya
vizuri zaidi katika Mtihani wa Taifa mwaka huu na miaka ijayo.
Kutokana
na utendaji kazi mzuri Mwalimu Akwilina pia alitambuliwa na Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuwa Mfanyakazi Hodari na siku ya Mei Mosi
alizawadiwa shilingi laki tano na cheti.
0 comments:
Post a Comment