Serikali imetoa
jumla ya Vitabu 297, 891 kwa ajili ya wanafunzi wa Shule za Msingi wa Darasa la
kwanza mpaka darasa la Tatu Mkoani Simiyu
Akizungumza
kabla ya makabidhiano ya vitabu hivyo Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI
Ndabazi Stephano amesema vitabu hivyo vitakidhi mahitaji ya wanafunzi kwa
kuwa idadi yake ni kubwa zaidi ya idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la
tatu ambao wako 261,257 kwa mkoa mzima.
Amesema
azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila shule ina vitabu vinavyojitosheleza
na inaendelea kuchapisha vitabu vya darasa la nne, ambapo Ofisi ya Rais
TAMISEMI imeanza kugawa vitabu hivyo katika mikoa mbalimbali na
akabainisha kuwa mkoa wa Simiyu nao utapewa vitabu hivyo.
"Tunaendelea
kugawa vitabu vya darasa la nne katika mikoa mbalimbali hapa nchini, hadi sasa vimegawanywa
katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi,
Mtwara, Ruvuma, Njombe, Iringa, Dodoma, Morogoro na awamu inayokuja ni Mikoa ya
Kanda ya Ziwa ukiwemo Simiyu” alisema Stephano.
“Vitabu
hivi ni original (halisi) kabisa hamna
kitabu feki hapa, maana kuna taarifa zinasambaa mitandaoni kuwa vitabu hivi
vimekosewa, niwaeleze walimu na
wanafunzi mliopo hapa vitabu hivi tunavyovigawa ni halisi na havijakosewa” alisisitiza Ndabazi Stephano
Aidha, Bw.
Gaitan Romwald kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) amesema vitabu hivi vinagawiwa
kwa awamu, hivyo vipo vitabu vingine vya darasa la kwanza mpaka la tatu ambavyo
kwa Mkoa wa Simiyu vitagawiwa pamoja na vitabu vya darasa la nne awamu ijayo.
Akizungumza
na walimu na wanafunzi walioshuhudia makabidhiano ya vitabu hivyo, Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewataka wanafunzi kuvitunza na kuvisoma ili
viwasaidie katika masomo yao, huku akiwataka walimu kuvitumia vitabu
hivyo kuwafundisha wanafunzi kwa moyo.
Afisa
Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Julius Nestory ameishukuru Serikali kwa kuleta
vitabu hivyo ambavyo amesema vitatatua tatizo la upungufu wa vitabu uliokuwepo
kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa mwaka hadi mwaka.
Walimu na
wanafunzi pia wameishukuru Serikali kwa kupeleka vitabu hivyo Mkoani Simiyu ambavyo
vitakuwa chachu na njia mojawapo ya
kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
“Tunaishukuru
sana Serikali kwa kuleta hivi vitabu, vitatusaidia katika masomo yetu maana
tutajisomea ili tujifunze na kupata uelewa zaidi" Eliasi John mwanafunzi
Shule ya Msingi Somanda A
“Kwa niaba
ya walimu wenzangu na wanafunzi wetu, napenda kuishukuru Serikali kutuletea
vitabu hivi, vitakuwa msaada mkubwa sana kwa wanafunzi wetu lakini hata kwetu
pia na vitatusaidia sana kuboresha mazingira yetu ya kufundishia watoto”
Mwalimu Janeroza Gabriel
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka(mwenye suti ya bluu) na baadhi ya walimu na wanafunzi wa Shule ya
Msingi Somanda A na B Mjini Bariadi, wakipokea vitabu vilivyoletwa na Serikali kwa ajili ya
wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka darasa la tatu mkoani humo, (wa tatu kulia) Ndabazi Stephano kutoka Ofisi
ya Rais TAMISEMI na (wa nne kulia) Gaitan Romwald kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania, kulia Afisa
Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Julius Nestory.
Sehemu ya sehena ya
vitabu 297, 891 vilivyoletwa na Serikali kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la
kwanza mpaka darasa la tatu mkoani Simiyu vikiwa vimeandaliwa tayari kwa
kupelekwa katika Halmashauri Mkoani humo ili viweze kupelekwa katika shule zote
za msingi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Somanda
A na B Mjini Bariadi, mara baada ya kupokea vitabu vilivyoletwa na Serikali kwa ajili ya
wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka darasa la tatu mkoani Simiyu(havipo
pichani).
0 comments:
Post a Comment