Sunday, July 29, 2018

JKT YAJIPANGA KUFUNDISHA WANANCHI TEKNOLOJIA ZA UFUGAJI SAMAKI MAONESHO YA NANENANE SIMIYU


Naibu  Mkurugenzi  Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa(SUMA JKT),  Luteni Kanali Peter Lushika  amesema  JKT  limedhamiria kuwafundisha wananchi watakaofika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi  Mkoani Simiyu, teknolojia mbalimbali za ufugaji wa samaki ikiwa ni pamoja na ufugaji kwa kutumia mabwawa, matenki  na vizimba(ndani ya ziwa), ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa samaki na kuzuia uvuvi haramu.

Luteni Kanali Lushika ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya maandalizi ya Jeshi hilo katika maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2018  na namna walivyojipanga kutoa elimu wa wananchi katika maeneo mbalimbali hususani katika kilimo, ufugaji na uvuvi.

“Tunajua wengi wanafahamu ufugaji wa samaki kwenye mabwawa, mwaka huu tunawaletea teknolojia ya ufugaji wa samaki kwenye matenki, walioko ziwani tutaonesha ufugaji wa samaki kwenye vizimba, teknojia hizi zitamsaidia mvuvi kuvua kuwa na uhakika wa upatiakanaji wasamaki, uhifadhi wa mazingira na kuondokana na uvuvi haramu” alisema Luteni Kanali Lushika.

Amesema JKT itawaeleza wananchi kuwa ufugaji wa samaki ni njia pekee ya kumwezesha mvuvi kupata samaki wakati wowote atakaohitaji hasa ufugaji  kwa kutumia  matenki.

Ameongeza kuwa pamoja na kuona teknolojia hizo  JKT itaandaa madarasa katika uwanja wa nanenane kwa ajili ya kufundisha wakulima, wafugaji, wavuvi, wajasiriamali ili waweze kuona mbinu za kilimo, ufugaji na uvuvi bora na matumizi bora ya pembejeo.

Katika hatua nyingine Luteni Kanali Lushika amesema ili kufikia Tanzania ya Viwanda lina mpango wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata pamba ambacho kitachakata pamba kutoka ikiwa ghafi mpaka kufikia kwenye zao la mwisho ambalo ni nguo, hivyo kitaliongezea zaidi thamani zao la pamba.

Naye Luteni Joseph Lyakurya Meneja wa Mradi Sumaponics amesema teknojia ya kufuga samaki kwa kutumia matenki ni nzuri kwa kuwa inatumia eneo dogo la ardhi , maji kidogo lakini inakuwa na uwezo wa kuchukua samaki wengi ikilinganishwa na teknolojia ya mabwawa, hivyo akatoa wito watu wafike Uwanja wa Nanenane wajifunze.

Kwa upande wao Vijana wa JKT wamesema mafunzo waliyoyapata katika teknolojia mbalimbali yamewawezesha kupata maarifa ambayo yanaweza kuwasaidia kujiajiri wenyewe,  hivyo wakatoa wito kwa wananchi kwenda kuona teknolojia hizo.

“Kama mtaalam  wa masuala ya uvuvi niliyehitimu chuo cha uvuvi Kigoma, nikiwa JKT nimepata elimu ya vitendo zaidi ya kile nilichokipata chuoni, tukiwa hapa Nanenane Bariadi  tutatoa elimu kuhusiana na masuala ya uvuvi kwa kutumia vizimba, nawaomba wananchi waje wajifunze, maana ufugaji wa samaki nao una tija katika Tanzania ya Viwanda” alisema Almasi Idd Yusuph kikosi cha 822 Lwamkoma JKT.

“Miimi nikiwa JKT nimejifunza namna ya kuandaa bustani kutokana na mafunzo niliyopata naweza kutambua  udongo mzuri na ambao  si rafiki kwa kilimo cha bustani kama huu, kupitia maonesho haya wananchi wataelewa ni namna gani wanaweza wakaufanya udongo huu ukafaa na wakalima bustani” alisema Nasri Mataka Kijana wa JKT 822 KK Lwamkoma Mara.

Naye Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa SUMA JKT Meja Peter Sebyiga amesema JKT inatoa huduma na kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa kuzingatia ubora , muda unaokubalika na jamii kwa bei rafiki kwa wateja, hivyo akatoa wito kwa wananchi kufika kwenye maonesho ya Nanenane ili kuona bidhaa hizo kutoka kwenye viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi.

Meja Sebyiga ametoa wito kwa Taasisi, Makampuni na watu binafsi kutumia samani zinazotengenezwa na Kiwanda cha Jeshi la Kujenga Taifa kwa ajili ya matumizi ya Ofisi na nyumbani na kusisitiza kuona umuhimu wa Watanzania kupenda vya kwao.

MWISHO
Naibu  Mkurugenzi  Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) Luteni Kanali Peter Lushika akitoa maelezo kwaMkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT)  Meja Jenerali Martin Busungu na  Viongozi wa Mkoa wa Simiyu, wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka, kuhusu ufugaji wa samaki kupitia teknolojia ya matanki yaliyojengwa na jeshi hilo kwa ajili ya maonesho ya Nanenane yatakayofanyika Kitaifa, 2018 Uwanja wa Nyakabindi katika Halmashauri ya mji Bariadi.
Naibu  Mkurugenzi  Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)  juu ya maandalizi maonesho ya Nanenane yatakayofanyika Kitaifa, 2018 Uwanja wa Nyakabindi katika Halmashauri ya mji Bariadi.

Viongozi wa JKT na  mkoa wa Simiyu wakiangalia moja ya mabwawa ya samaki yaliyoandaliwa na Jeshi la kujenga Taifa(JKT) kwa ajili ya maonesho ya Nanenane yatakayofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Nanenane wa kanda ya ziwa mashariki, uliopo Nyakabindi Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Luteni Joseph Lyakurya Meneja wa Mradi Sumaponics  akiwaeleza  waandishi wa habari juu ya teknolojia ya ufugaji wa samaki kupitia matanki ambayo itaoneshwa kwa wananchi wakati wa Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima (Nanenane) yatakayofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Nanenane wa kanda ya ziwa mashariki, uliopo Nyakabindi Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Nasri Mataka Kijana wa JKT 822 KK Lwamkoma Mara akiwaeleza  waandishi wa habari juu ya bustani zilizolimwa kisasa ambazo zitaoneshwa kwa wananchi wakati wa Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima (Nanenane) yatakayofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Nanenane wa kanda ya ziwa mashariki, uliopo Nyakabindi Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa SUMA JKT Meja Peter Sebyiga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)  juu ya maandalizi maonesho ya Nanenane yatakayofanyika Kitaifa, 2018 Uwanja wa Nyakabindi katika Halmashauri ya mji Bariadi.


0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!