Wizara ya Madini kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu
wa Rasilimali Madini (SMMRP) imekabidhi eneo la ujenzi wa Kituo cha Umahiri
Bariadi Mkoani Simiyu kwa Mkandarasi wa ujenzi huo SUMA JKT ambao unaotarajiwa kuanza
mwezi huu wa Julai 2018.
Makabidhiano hayo yamefanyika jana Mjini Bariadi
Mkoani Simiyu na kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka, mara
baada ya timu ya wataalam wa Wizara ya Madini na SUMA JKT kutembelea eneo la ujenzi
lililopo Nyaumata Mjini Bariadi.
Akizungumzia kituo hicho Afisa Madini Mkoa wa Simiyu,
Bw. Fabian Mshai amesema “Kituo hiki ni Jengo
la Ofisi ambalo litakuwa na kumbi za
kutolea mafunzo mbalimbali yahusianayo na uchimbaji wa madini unaozingatia
kanuni za afya, usalama, uchambuzi wa madini na uhifadhi wa mazingira kwa
wachimbaji wadogo ili uchimbaji uwe wenye tija”
Mshai ameongeza Kituo hiki cha Umahiri Bariadi
kitajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.3 na Kampuni ya Ujenzi ya SUMA
JKT na kusimamiwa na Kampuni ya Sky Actate Consultants.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameishukuru
Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuamua kujenga Kituo hicho kwa kuwa mkoa
huo ni mpya na unahitaji majengo mengi, hivyo amaesema ujenzi huo utajibu
mahitaji ya mkoa katika kuwasaidia wachimbaji wadogo kuondokana na uchimbaji wa
kienyeji na kwenda kwenye uchimbaji wa kisasa
"Wachimbaji wetu wadogo wamekuwa wakifanya
shughuli zao kienyeji lakini uwepo wa kituo hiki utajibu mahitaji yao kwa
sababu kitakuwa ni sehemu sahihi ya wao kupata elimu juu ya uchimbaji bora,
wataalam wa madini watakuwa karibu kwa kuwa ukamilishaji wa kituo hiki utaenda
sambamba na uwepo wa rasilimaliwatu" alisema Mtaka.
“ Sisi kama mkoa tuna faida ya uwepo wa rasilimali madini
tuna nikeli, shaba, dhahabu, cobalt, tuna chumvi katika wilaya ya Meatu lakini
pia tuna madini ya ujenzi kama kokoto, mchanga na mengine, hivyo uwepo wa kituo
cha umahiri kutasaidia wachimbaji kufanya kazi zao katika utaalam ili uchimbaji
ufanyike kwa ufanisi na uwe na tija” alisema.
Ameongeza kuwa uwepo wa kituo hicho pia utachangia
kuboresha mazingira ya utendaji kazi ndani ya mkoa tofauti na ilivyo sasa,
ambapo watumishi hao wanatumia majengo ya kukodi ambayo wakati mwingine
hayakidhi mahitaji yao.
Amesema kuwepo kwa kituo hicho pia kutasaidia kufikia
lengo la Serikali la kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa moja ya vyanzo vikubwa
vya mapato kwa kuwekeza utaalam wa rasilimali watu, majengo, upimaji na utaalam
mbalimbali wa kusaidia wachimbaji wadogo; hivyo akasisitiza SUMA JKT
kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kwa wakati.
Naye Luteni Kanali Petro Ngata Meneja wa SUMA JKT
Kanda ya Ziwa amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kuwa
kazi ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Bariadi itafanyika kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony
Mtaka (katikati) akishuhudia makabidhiano ya nyaraka za Ujenzi wa Kituo Mahiri
cha Mkoa wa Simiyu kati ya Meneja wa SUMA JKT Kanda ya Ziwa Luteni Kanali Petro
Ngata na Meneja na Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP),
Bw. Andrew Erio kutoka Wizara ya Madini,
yaliyofanyika jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mara baada ya makabidhiano
ya eneo la ujenzi wa kituo hicho Mjini Bariadi.
Baadhi ya Viongozi wa SUMA JKT na
Wizara ya Madini wakikagua eneo la Ujenzi wa Kituo Mahiri Bariadi Mkoani
Simiyu, kabla ya kufanya makabidhiano ya eneo hilo jana Mjini Bariadi.
Baadhi ya Viongozi wa SUMA JKT na
Wizara ya Madini wakiangalia mchoro wa Jengo la Kituo cha Umahiri Bariadi
Simiyu, katika eneo la Ujenzi wa Kituo hicho
kabla ya kufanya makabidhiano ya eneo hilo
jana Mjini Bariadi, kwa ajili ya kuanza taratibu za ujenzi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka(wa sita kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa SUMA JKT
baada ya kushuhudia makabidhiano ya nyaraka za ujenzi wa Kituo cha
Umahiri Bariadi kati ya Mkandarasi ambaye ni SUMA JKT na Wizara ya Madini yaliyofanyika
jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya makabidhiano ya eneo
la ujenzi wa kituo hicho Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa SUMA JKT baada ya
kushuhudia makabidhiano ya nyaraka za ujenzi wa Kituo cha Umahiri Bariadi
kati ya Mkandarasi ambaye ni SUMA JKT na Wizara ya Madini yaliyofanyika jana katika
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa
kituo hicho Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment