Thursday, July 19, 2018

WAZIRI KIGWANGALA AAGIZA WALIOVAMIA PORI LA AKIBA LA KIJERESHI KUONDOKA KWA HIARI


Na Stella Kalinga, Simiyu
Waziri wa maliasili na utalii, Dk Hamis Kigwangala, amewataka wananchi wa vijiji  vinavyopakana na Hifadhi ya pori la akiba kijereshi lililoko Wilayani Busega Mkoani Simiyu, ambao wameanzisha makazi na kufanya shughuli za kijamii kwenye eneo la mitaa 500 (buffer zone) kutoka kwenye mpaka wa pori hilo kuondoka mara moja.


Ametoa agizo hilo jana alipotembelea pori hilo ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi, baada ya kushuhudia makazi na shughuli nyingine za kibinadamu ndani ya pori hilo kutoa agizo hilo na kusema kuwa sheria za uhifadhi wa wanyamapori haziruhusu vitendo hivyo ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria pamoja na kingo zake (buffer zone) ambazo ni mita 500 kutoka kwenye mpaka halisi wa eneo la hifadhi.

"Mpaka itakapofika tarehe 31 mwezi ujao wananchi wote hawa wawe wameshaondoka eneo hili kwa hiari yao wenyewe, muwatangazie na mpime eneo hili vizuri muweke alama ili wajue ni wapi wanatakiwa kuondoka.

"Na ikifika tarehe 1 Septemba kama kuna watakaokuwa wamekaidi agizo hili, basi mfanye oparesheni maalum muwaondoe na msafishe kila kitu, ni lazima ifike mahali kila mmoja aheshimu sheria za nchi" alisema Dk. Kigwangalla kuuagiza uongozi wa pori hilo.

Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla ametoa miezi mitatu kwa mwekezaji wa hoteli ya kitalii ya Kijereshi Tented Camp kurudisha kwa Kamishna wa Ardhi hati miliki ya kipande cha ardhi chenye ukubwa wa hekta 464 kilichopo ndani ya pori hilo kwakuwa ni batili; kwa kuwa pori hilo lilianzishwa mwaka 1994 wakati mwekezaji huyo anadai kumilikishwa eneo hilo mwaka 1995.

Aidha, amemtaka pia mwekezaji huyo kuheshimu sheria na taratibu za uwekezaji katika eneo hilo ikiwemo kulipa ada na tozo mbalimbali.

Awali akimweleza Waziri Meneja wa Pori hilo Diana Chambi alisema kuwa wananchi waliovamia hifadhi ya pori hilo ni kutoka kwenye vijiji vya Lukungu, Mwabayanda, mwakiloba, kijirishi pamoja na Igwata, ambao alieleza waliomba kupewa muda mpaka mwezi Agosti mwaka huu wavune mazao waliyolima ili waondoke kwa hiari kwenye eneo la hifadhi hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe.Tano Mwera, alimuomba waziri kuisaidia idara ya Ardhi na Maliasili ya halmashauri hiyo Gari kwa ajili ya kufanya doria mbalimbali kwenye hifadhi ya pori hilo ili kukabiliana na vitendo vya ujangili pamoja na wanyama kuvamia makazi ya wananchi.

Mara baada ya kutembelea pori hilo, Mhe.Waziri Kigwangala alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ambaye amesema Mkoa huo unafanya juhudi katika kukuza utalii kwa kujenga uwezo wa utamaduni wa ndani na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo ikiwa ni pamoja na Mapori ya Akiba ya Maswa  na Kijereshi.

Aidha, Mtaka aliongeza kuwa Serikali imepanga kujenga uwanja wa ndege katika eneo la Igegu wilayani Bariadi ambapo ni jirani kabisa na Hifadhi ya Taifaya Serengeti hivyo itawarahisishia watalii kufikia kwa urahisi hifadhi ya Taifa ya Serengeti kufanya shughuli za Kitalii.

Pori la Akiba Kijereshi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 65.72 linasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA na lilipandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba mwaka 1994 kwa Tangazo la Serikali Na. 215 la terehe 10 Juni, 1994 na hiyo ni kutokana na umuhimu wake kiuchumi na kiikolojia hususan katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.





Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akioneshwa mipaka ya Pori la Akiba Kijereshi na Meneja wa pori hilo, Dianna Chambi alipotembelea pori hilo jana kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi katika wilaya ya Busega mkoani Simiyu. Alitoa siku 45 kwa wananchi wote waliovamia kingo/bafa za hifadhi hiyo kuondoka kwa hiari yao. Kulia ni Mkuu wa Kanda wa Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya Serengeti, Johnson Msella.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akitoa maelekezo kwa Meneja wa Pori la Akiba Kijereshi, Dianna Chambi (wa pili) kuhusu wananchi waliovamia hifadhi hiyo alipotembelea pori hilo jana kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi katika wilaya ya Busega mkoani Simiyu.  
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akikagua eneo la hoteli ya kitalii ya Kijereshi Tented Camp iliyopo ndani ya Pori la Akiba Kijereshi alipotembelea pori hilo jana kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi katika wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa kijiji cha Logolambogo katika wilaya ya Itilima mkoani Simiyu alipolitembelea Pori la Akiba Maswa jana kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi na kutatua changamoto zake. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alipowasili mkoani humo jana kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja ya kukagua shughuli za uhifadhi na kutatua changamoto zake.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akikagua moja ya eneo la kingo/bafa la Pori la Akiba Maswa ambalo limevamiwa na wananchi kwa ajili ya shughuli kilimo alipolitembelea pori hilo jana kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi katika wilaya ya Itilima mkoani Simiyu. Kulia kwake ni Mbunge wa Itilima, Njalu Silanga na Meneja wa Pori hilo, Lusato Masinde.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati wa ziara yake Mkoani humo jana.
Baadhi ya viongozi wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua shughuli za uhifadhi jana mkoani humo. 
Meneja wa Pori la Akiba la Maswa mkoani Simiyu, Lusato Masinde akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua shughuli za uhifadhi jana mkoani humo. 


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akisaini Kitabu cha wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi, wakati akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za uhifadhi mkoani humo.



0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!