Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amezindua
zoezi la utoaji wa chanjo ya Surua-Rubella kwa watoto wenye umri kuanzia miezi
tisa hadi miezi 59 (chini ya miaka mitano) na kuwahimiza wananchi kuwapeleka
watoto kupata chanjo hiyo inayotolewa bila malipo kwenye vituo vya kutolea
huduma za afya na vituo vya muda vilivyotengwa
vipatavyo 405, ili kuwakinga watoto hao na maradhi.
Akizungumza na wananchi walioshiriki katika uzinduzi
wa zoezi hilo Oktoba 17, 2017 katika Kituo cha Afya cha Muungano Mjini
Bariadi, Mtaka amesema ni vema wananchi
hao watumie siku zilizotengwa kutoa chanjo hiyo kuanzia Oktoba 17-21, 2019
kuwapeleka watoto kwenye chanjo na wawe
mabalozi wema kwa wenzao.
“Madhara ya Surua ni pamoja na masikio ya mtoto
kutoa usaha utakaosababisha mtoto kuwa kiziwi, vidonda vya macho vinavyoweza
kusababisha upofu, utapiamlo, kuvimba ubongo, udumavu wa akili na kifo; mliokuja
leo mkawe mabalozi wema kwa wenzenu wawalete watoto chanjo ili watoto wakingwe
dhidi ya haya magonjwa,” alisema Mtaka.
Katika hatua nyingine Mtaka amewataka wananchi kutumia vituo vya kutolea
huduma za afya vilivyopo kwenye maeneo yao kupata huduma za matibabu ili waweze
kupata tiba sahihi kwa wakati sahihi badala ya kwenda kwa waganga kupiga ramli.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Festo
Dugange amesema watoto takribani 420,000 wanatarajiwa kupata chanjo ya
Surua-Rubella, ambapo chanjo hiyo itakuwa ikitolea kuanzia saa moja asubuhi
hadi saa 12 jioni.
Kwa upande wake mmoja wa wazazi waliowapeleka watoto
wao kwenye Bw. Hamza Adam amesema ni vema kila mzazi mwenye mtoto wa umri chini
ya miaka mitano ampeleke akapate chanjo ya Surua-Rubella, ili wawakinge na
maradhi hayo na kuwaomba wasiwapeleke kwa waganga wa jadi wanapokuwa wagonjwa.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Benki Mjini Bariadi, Consolata
Cosmas amesema wenyeviti wa Mitaa na Vijiji
mkoani Simiyu wameshiriki kikamilifu katika kuhamasisha waananchi kupeleka
watoto kupata chanjo, hivyo imani yao ni kwamba zoezi hilo litafanikiwa kwa
kuhakikisha watoto wote waliopangwa kupewa chanjo wanapewa na lengo linafikiwa.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka (wa pili kulia) na viongozi wengine wa mkoa wa Simiyu wakishuhudia
mtoto akipewa chanjo ya Surua-Rubella
wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji chanjo hiyo kimkoa Oktoba 17, 2019
katika Kituo cha Afya cha Muungano, Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka (wa pili kulia) akipokea maelezo kutoka kwa mtaalam kuhusu
chanjo ya Surua-Rubella wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji chanjo hiyo
kimkoa Oktoba 17, 2019 katika Kituo cha Afya cha Muungano, Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe . Anthony Mtaka akizungumza na wananchi waliowapeleka watoto wao kupata
chanjo ya Surua-Rubella , wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji chanjo hiyo
kimkoa Oktoba 17, 2019 katika Kituo cha Afya cha Muungano, Mjini Bariadi.
Muuguzi akifanya
maandalizi kwa ajili ya kutoa chanjo ya Surua-Rubella, wakati wa uzinduzi wa
zoezi la utoaji chanjo hiyo kimkoa Oktoba 17, 2019 katika Kituo cha Afya cha
Muungano, Mjini Bariadi.
Baadhi ya wakina mama
waliowapeleka watoto wao kupata chanjo
ya Surua-Rubella, wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji chanjo hiyo kimkoa
Oktoba 17, 2019 katika Kituo cha Afya cha Muungano, Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment