Kutokana na kuchelewa kuanza kwa maonesho ya Nanenane
Mwaka 2020 katika baadhi ya kanda serikali imetangaza kuongeza siku mbili za
maonesho hayo ambapo kwa mwaka huu yatahitimishwa Agosti 10 badala ya Agosti 8.
Taarifa hiyo imetolewa Agosti 04, 2020 na Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga wakati
alipotembelea Banda la Chama cha wajasariamali wanawake Tanzania (TABWA) kwenye
viwanja vya Maonesho ya wakulima (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika
Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Hasunga amesema kuwa kulingana na mahitaji ya wadau mbalimbali na wananchi
kuendelea kujifunza mbinu bora za kilimo hususani ambao hawakupata fursa awali
watatumia siku hizo zilizoongezwa katika kanda zote kujionea mbinu bora za
kilimo, mifugo na uvuvi na teknologia za kisasa.
“Awali tulipanga kufanya maonesho ya nanenane mwaka 2020 siku nane lakini kutokana na maombi ya wadau na wananchi
pamoja na baadhi ya kanda kuchelewa kufungua maonesho haya, kwa mamlaka niliyopewa natangaza rasmi leo
kuongeza siku mbili za maonesho, kwa hiyo tutahitimisha Agosti 10, 2020”
alisema Hasunga.
Wakati huo huo mhe. Hasunga amewataka wananchi wote nchini, wakiwemo
wafugaji, wavuvi na wakulima kutumia fursa hiyo ya siku zote 10 za maonesho
kwenda kujifunza zaidi, teknologia mpya za kilimo, uvuvi na ufugaji.
Awali
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga akizungumzia kuongezwa muda wa maonesho
ya nane nane alisema amelipokea vizuri tamko hilo na watazitumia
vizuri siku hizo zilizoongezwa hasa kujifunza mambo ambayo wasingeweza kuyapata
pasipo kuongezewa muda huku akitoa rai kwa wakulima kujitokeza kwa wingi kufika
kwenye maonesho hayo kujifunza teknolojia mbalimbali .
Kwa upande
wake Luteni Kanali Peter Lushika ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi
ya nane nane katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) akizungumza kwa niaba ya
washiriki wa maonesho hayo alisema kuwa wamefurahia agizo hilo ambalo limewapa
fursa ya kuendelea kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ambao
hawajapata fursa hiyo.
Aidha Luteni Kanali Lushika ametoa rai kwa wananchi kutembelea banda lao kujifunza teknolojia nyingi ambazo Jeshi hilo limeandaa hatua itakayowawezesha kubadilisha mfumo wa utendaji kazi zao hatua ambayo itawasaidia kuongeza thamani kwenye mazao yao.
Aliyekuwa katibu tawala wa Mkoa wa Simiyu Jumanne Sagini amesema kuwa maonesho ya mwaka 2020 yana maboresho makubwa ya mazao na teknolojia nyingi huku akitoa rai kwa wananchi kutembelea viwanja hivyo ili kupata elimu itakayowaletea kuboresha shughuli zao za Kilimo, Mifugo na Uvuvi hatua ambayo itapelekea kuongeza tija kwenye shuguli zao.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment