Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki ametoa wito kwa wakulima (wanaushirika) kuchagua viongozi waadilifu wanaojali maslahi ya wote badala ya kuangalia maslahi binafsi.
Mhe. Kairuki amesema hayo Agosti 03, 2020 wakati akitoa ujumbe
maalum wa ushirika kwa katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa 2020 yanayoendelea
katika Viwanja vya Nyakabindi Bariadi mkoani Simiyu akimwakilisha Waziri Mkuu
wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.
Aidha,
Waziri Kairuki ameipongeza wizara ya kilimo kwa uamuzi wa kuvifuta vyama vya
ushirika 2,539 ambavyo vilikuwa na utendaji mbovu uliosababisha kero kwa wanaushirika
nchini hatua itakayowawezesha wanaushirika ambao ni wakulima, wavuvi na
wafugaji kunufaika na kazi zao ndani ya ushirika .
“Ninawapongeza
sana Wizara kwa hatua mliyochukua yakuvifuta vyama vya ushirika 2,539 kwasababu
ya kutofanya kazi iliyokusudiwa.” Alisema Waziri Kairuki.
Waziri Kairuki alisema katika kipindi cha 2018/2019 jumla ya viwanda 75
vimeanzishwa na vyama vya ushirika vinavyochakata alizeti, chikichi,
kutengeneza samani za majumbani, kuchakata pamba na mazao ya nafaka pamoja na
usindikaji wa maziwa.
“ Viwanda vinavyomilikiwa na vyama vya ushirika vimeongezeka kutoka
viwanda 133 mwaka 2018 hadi kufikia viwanda 208 mwaka 2019” alisema Waziri
Kairuki.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ameiagiza Tume ya Maendeleo ya
Ushirika kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (EGA) kuangalia namna bora
ya kuweka mfumo shirikishi wa TEHAMA utakaoweza kuongeza uwazi katika usimamizi
wa vyama vya ushirika hususan AMCOS.
Naye Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema wizara yake itaendelea
kuhakikisha wakulima, wavuvi na wafugaji nchini wananjiunga na vyama vya
ushirika ambavyo vitawasaidia kupata nguvu ya kuweza kupata mitaji, masoko,
pembejeo na huduma za ugani ili wakuze uzalishaji.
Maonesho ya Kilimo ya Nane nane Kitaifa yameingia siku ya tatu leo ambapo
wananchi na wakulima toka mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga wanaendelea kupata
elimu kwenye mabanda na vipando vilivyoandaliwa.
Kauli mbiu ya Nane nane mwaka huu inasema“ Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo
na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020”
MWISHO.
TAZAMA PICHA MBALIMBALI WAZIRI KAIRUKI ALIPOTEMBELA MABANDA MABALIMBALI YA MAONESHO YA NANENANE NYAKABIDHI BARIADI SIMIYU
0 comments:
Post a Comment