Thursday, July 4, 2019

KAMATI YA ULINZI NA USALAMA MKOA SIMIYU YARIDHISHWA NA KASI YA TBA UJENZI WA OFISI YA DC BUSEGA


Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Anthony Mtaka imeridhishwa na kasi ya Ujenzi  wa  jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega na majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, chini ya Mkandarasi Wakala wa Majengo nchini  (TBA ).

Hayo yamebainishwa na kamati hiyo ,mara baada ya kukagua ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Busega ambapo ujenzi umeanza mwezi Aprili mwaka huu na  unatarajia kukamilika ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema miradi yote inayotekelezwa na TBA Simiyu imekuwa ikitekelezwa kwa wakati na wakati mwingine imekuwa ikitekelezwa na kukamilika kabla ya muda uliopangwa katika mkataba, huku akiishukuru serikali kwa kutenga fedha za  ujenzi wa ofisi ya mkuu wa wilaya ya Busega  ambayo itatua changamoto za  wananchi za upatikanaji wa huduma kwa karibu .

“Tumepata Meneja mzuri wa TBA ambaye anatekeleza miradi yake kwa wakati, miradi yote tuliyompa imetekelezwa mbele ya muda uliowekwa kwenye mkataba; kwa mradi huu umeenda kwa kasi ambayo inaendana na uhitaji wa wananchi wa Busega waliokuwa wanahitaji mahali pa kupata huduma” alisema Mtaka.

Mkuu wa wilaya ya Busega Mhe.Tano Mwera amesema utendaji wa kazi kwa sasa ni mgumu kutokana na ufinyu wa jengo wanalolitumia kama ofisi, hivyo kukamilika kwa jengo hilo kutawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi.

“Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kutupa fedha za ujenzi wa jengo hili, litakapo kamilika litatuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi kwa sababu ofisi tunayoitumia sasa hivi ni finyu sana na watendaji wametawanyika sana hivyo inatuwia vigumu kiutendaji”alisema Mwera.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema kazi zote  zinazofanywa na Wakala wa majengo nchini TBA Mkoa wa Simiyu zimekuwa zikifanywa kwa viwango na zinakamilika kwa wakati, huku akiahidi kulipa fedha zilizobakia kwa wakati.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Majengo nchini TBA Mhandisi Likimaitare Naunga amesema mkataba wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega ni miezi mitano na wanatarajia kukamilisha ujenzi kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu.
Kukamilika kwa ujenzi awamu ya kwanza ya jengo hilo  utagharimu kiasi cha shilingi milioni mia saba  nukta saba.
MWISHO


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu ya kukagua ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega, Julai 04, 2019.

Meneja wa Wakala wa Majengo nchini TBA Mhandisi Likimaitare Naunga (wa pili kulia) akiwaongoza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu kukagua ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega, Julai 04, 2019.
Meneja wa Wakala wa Majengo nchini TBA Mhandisi Likimaitare Naunga akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu kukamilisha ziara ya kukagua ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega, Julai 04, 2019.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu kukamilisha ziara ya kukagua ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega, Julai 04, 2019.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akizungumza katika majumuisho ya ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu ya kukagua ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega, Julai 04, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka( wa tatu kushoto) na viongozi wengine wakikagua ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega, Julai 04, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka( wa sita kushoto) katika picha ya pamoja na viongzoi mabalimbali wa mkoa wa Simiyu mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kukagua ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega unaoendelea wilayani Busega, Julai 04, 2019. 
Sehemu ya nyuma ya Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busaga ambalo linatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu na wananchi kuanza kupata huduma.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!