Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga
amevitaka vyombo vya utoaji haki hapa nchini ikiwemo jeshi la polisi na
Mahakama kutochelewesha utoaji wa haki ili kuepuka msongamano wa mahabusu
katika magereza na badala yake vyombo
hivyo vitende haki na kwa wakati.
Waziri Mahiga ameyazungumza hayo Julai 14, 2019 wakati
akizungumza na waandishi wa habari Mjini Bariadi mara baaada ya kuhitimisha
ziara yake na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka, Biswalo Mganga mkoani Simiyu ambayo
ililenga kujionea mazingira ya utoaji haki na haki jinai katika mikoa ya Simiyu
na Mara.
“Kuna ucheleweshaji wa kutoa haki kabla mahabusu hajapelewa
mahakamani, unaweza kuwa miezi sita, mwaka mmoja na wengine hata miaka miwili
bado wanasubiri kwenda mahakamani; hilo nalo linachangia si tu uchache na
nafasi ndani ya gereza lakini pia utaratibu wa upelelezi unachelewa ili
kukamilisha mashtaka,lakini pia kazi za mahakimu zinatakiwa ziende haraka ili
kupunguza mrundikano wa kesi” alisema Waziri Mahiga.
Aidha, Dkt. Mahiga amesema katika ziara hiyo pia wamebaini kuwa
katika mikoa ya Simiyu na Mara mahabusu wengi wanakabiliwa na kesi za kuingilia
hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wizi wa mifugo, ugomvi utokanao na wizi wa
mifugo na matatizo yatokanayo na jamii.
Ameongeza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP), Biswalo
Mganga kwa mamlaka aliyopewa na sheria
ya kusamehe baadhi ya makosa kwa utaratbiu na vigezo Fulani, katika kila Gereza
walilopita DPP aliweza kuwasamehe baadhi ya mahabusu kwa kuzingatia vigezo
kadhaa ambavyo ni wazee waliozidi miaka 70, watoto chini ya miaka 18, watu
wenye ulemavu na wale wenye makosa madogo kama wizi wa kuku na wamekaa mahabusu
kwa muda mrefu.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa
Mashtaka(DPP), Biswalo Mganga amesema pamoja
na vigezo vilivyotajwa na waziri Mahiga baadhi ya wahabusu walioachiwa ni wale
waliopelekwa gerezani au mahakamani wakati hawakustahili ikiwa ni pamoja na
wale waliobambikiwa kesi.
“Kwa hapa Bariadi kuna kesi 46 ambazo zina watu wanaoweza kufika
100, Tarime nako ni watu wengi kidogo lakini idadi haitusaidia, itoshe kusema
kuna watu walioachiwa baada ya kuangalia vigezo fulani; kuna watu wanapelekwa
mahakamani ambao pengine hawakustahili, ni kwa sababu ya kubambikiwa kesi,
mfano mtu amekopa fedha na baada ya kushindwa kulipa badala ya kupelekwa kwenye
kesi ya madai, mdai anampeleka polisi kumshtaki kwa kujipatia fedha kwa
udanganyifu” alisema DPP.
Kwa upande wake mmoja wa wananchi Mjini Bariadi, Hangi Sapoti
amesema ili kuzuia msongamano katika magereza ameshauri mahakama na jeshi la
polisi kujiridhisha kabla ya kuwapeleka mahabusu gerezani na ikiwa watuhumiwa
wamefanya makosa yanayoruhusu kupewa dhamana wapewe ili wabaki wale tu ambao
wamefanya makosa yasiyo na dhamana.
MWISHO
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga
(kushoto) akizungumza na waandishi wa habari Julai 14, 2019 Mjini Bariadi mara
baada ya kuhitimisha ziara yake mkoani Simiyu, (kulia ) Mkurugenzi Mkuu wa
Mashtaka, Bw. Biswalo Mganga.
Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka(DPP), Bw. Biswalo Mganga (kulia ) akizungumza na waandishi wa habari Julai 14,
2019 Mjini Bariadi mara baada ya kuhitimisha ziara yake na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt.
Augustine Mahiga mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza kabla ya
kumkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (wa pili kushoto)
azungumze na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha ziara yake Mkoani
Simyu, Julai 14, 2019.
Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka(DPP), Bw. Biswalo Mganga(kushoto)
akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka mara baada ya kuhitimisha
ziara yake na Waziri wa Katiba na
Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga mkoani Simiyu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga(wa pili
kushoto) akizungumza jambo na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Simiyu, mara baada
ya kuhitimisha ziara yake mkoani Simiyu, (kushoto) Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka(DPP),
Bw. Biswalo Mganga na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka.
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga(katikati)
akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka(kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka(DPP), Bw. Biswalo Mganga mara baada
ya kuhitimisha ziara yake Mkoani Simyu, Julai 14, 2019.
0 comments:
Post a Comment