Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri
kupitia kwa wahandisi wa ujenzi kuwatambua na kuwajengea uwezo mafundi wote wanaotoka
kwenye jamii wanaofanya kazi za serikali kwa kutumia mfumo wa ujenzi usiotumia
wakandarasi (Force Account) hususani waliofanya kazi nzuri kwenye ujenzi wa
hospitali za wilaya ya Mkoa wa Simiyu.
Mtaka ameyasema hayo mapema jana mara baada ya kufanya ziara
katika hospitali za wilaya ya Itilima, Bariadi na Busega zinazoendelea kujengwa
lengo ni kujua hatua ziizofikiwa katika ujenzi, ambapo amesema mafundi hao wakitambuliwa na kujengewa uwezo utendaji wao
utaimarishwa na kazi watakazofanya zitafanywa katika ubora.
“Ni lazima kama Mkoa tuwe na mfumo wa kuwatambua mafundi wote
waliofanya kazi ya kujenga hospitali zetu zote tatu na tuanze kuwajengea uwezo,ili
miradi yetu ya Serikali tunayoendelea kuifanya tusiwe na watu wapya sana na
kama tukipata wapya watakuwa wanafanya kazi chini ya uangalizi wa watu wenye
uwezo mzuri zaidi” Mtaka
Mbali na hayo amezipongeza wilaya hizo kwa mfumo walioutumia wa kununua
vifaa kiwandani moja kwa moja kwani umesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo
zimefanikisha ujenzi kufikia katika hatua nzuri, huku akizisisitiza wilaya hizo
kuwashirikisha Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwenye ununuzi wa vifaa vya umeme
ili kupunguza gharama zisizo za lazima.
Kwa upande wao Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya SACF James
John (Bariadi) Elizabeth Gumbo (Itilima) wamesema kuwa miongoni mwa
changamoto zilizopelekea kutokamilisha kwa miradi hiyo ambayo ilitakiwa kukamilika
Juni 30 , 2019 ni fedha kutotosheleza na
kusisitiza kuwa ikiwa watapokea fedha mapema watakamilisha majengo yote.
“Tulipokea bilioni 1.5 tumebakiwa na shilingi milioni 75 kwa
ajili ya kulipa mafundi tulioingia nao mkataba, ili tuweze kukamilisha hatua
zilizosalia katika ujenzi wa majengo saba ya awali tunahitaji shilingi milioni
370” alisema James John mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
“Tulipokea shilingi bilioni 1.5 tumebakiwa na shilingi milioni
ambazoo zimetengwa kwa ajili ya malipo ya mafundi, tukiongezewa shilingi
milioni 360 tutamaliza majengo kwa hatua zilizobaki” alisema Elizabeth Gumbo mkurugenzi
Halmashauri ya Wilaya ya Itilima.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Busega Tano Mwera amebainisha kuwa
kwa hatua walioyofikia fedha zinatosha kukamilisha mradi na kwamba changamoto
iliyopelekea wasiweze kukamilisha kwa wakati ni ucheleweshwaji wa mfumo na
kwamba ikifanyiwa kazi mradi utakamilika kwa wakati.
Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesisitiza
Halmashauri za Wilaya ya Bariadi, Busega na Itilima kumalizia ujenzi wa
Hospitali za wilaya kwa wakati ambapo pia alitoa rai ya kuhakikisha barabara zinatengenezwa,
miti na bustani za maua zinapandwa katika
maeneo hayo ambayo zinajengwa hospitali hizo.
Katika ujenzi wa hospitali za wilaya ya Bariadi, Itilima na
Busega ambao ni wa awamu ya kwanza kuna jumla ya majengo takribani ishirini na moja
yanapaswa kujengwa (21) ikiwa ni majengo
saba kwa kila Hospitali (kwa awamu ya kwanza) ambayo yapo katika hatua
mbalimbali.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) akizungumza na
Viongozi wa Wilaya ya Busega, Itilima na Bariadi katika majumuisho ya Ziara ya
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa katika Hospitali za Wilaya hizo,
iliyofanyika Julai 03,2019. .
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi(kushoto)
akimuongoza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na wajumbe wengine wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya
Itilima, Julai 03, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(mwenye koti jeusi) na
viongozi wengine wakitoa katika moja ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya
Bariadi wakati wa ziara maalum ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo iliyofanyika
Julai 03,2019
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(mwenye shati la kitenge
mbele) na viongozi wengine wakitoa katika moja ya majengo ya Hospitali ya
Wilaya ya Busega wakati wa ziara maalum ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo
iliyofanyika julai 03, 2019
Baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakikagua
Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bariadi Julai 3, 2019.
Baadhi ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Busega
yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi
0 comments:
Post a Comment