Kukamilika kwa kiwanda cha ushonaji katika Halmashauri ya Mji wa
Bariadi kutasaidia kuongeza ajira, ujuzi na vipato vya wananchi wa Simiyu
hususani wanawake na vijana.
Kiwanda hicho kinakadiriwa kujengwa kwa
fedha kiasi cha shilingi milioni 85 hadi kukamilika kwake ambapo itatoa pia
fursa kwa wakazi wa mji wa Bariadi na Mkoa mzima kwenda kujifunza ushonaji na
ubunifu wa mitindo mbalimbali ya nguo ambayo baadae wataweza kujiajiri na
kujiongezea kipato.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa kiwanda
hicho mbele ya kiongozi wa Mbio za
Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 Ndg. Charles Kabeho kabla ya kuweka jiwe la msingi kiwanda hicho
,Mhandisi wa Halmashauri ya Mji Samwel Msolini amesema Halmashauri
ilipokea msaada wa vyerehani 50, kutoka
Serikali ya Jamhuri ya China, vyerehani 25 vikiwa vya umeme na vingine 25 ni vya
kawaida.
Ameongeza kuwa baada ya kupokea msaada
huo Halmashauri imeamua kuanzisha Kiwanda hicho ili kuviwezesha kutumika na
hatimaye Halmashauri ipate mapato, kutoa ajira kwa wananchi na wananchi kupata
huduma za mavazi yenye kiwango.
“”Lengo la Ujenzi wa Kiwanda cha
Ushonaji ni kwa ajili ya kushona nguo kwa mahitaji mbalimbali ikiwa ni pamoja
na nguo zinazovaliwa kwenye sherehe
mbalimbali, sare za shule na maeneo ya kazi, mradi huu ukikamilika utaongeza
mapato ya Halmashauri, kutoa ajira kwa wananchi na wananchi watapata huduma ya
mavazi” alisema Msolini..
Aidha, akiweka jiwe la msingi katika kiwanda hiki,
kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho
amefurahishwa sana na akapongeza Halmashauri kwa kubuni mradi huo ambao amesema
utakuwa na manufaa kwa wananchi na Halmashauri.
“Kiwanda hiki kitawasaidia wajasiriamali wanaojihusisha na
masuala ya ushonaji kupata kipato,
kitawasaidia wananchi kujiajiri wenyewe, lakini pia Halmashauri nayo itapata
mapato” alisema Charles Kabeho..
Angello Michael mkazi wa mji wa Bariadi
alisema kiwanda hicho kitasaidia vijana na wanawake wengi ambao hawana kazi za
kufanya na kubadilisha maisha na vipato vyao kwa baadaye.
Katika hatua nyingine Kiongozi wa Mbio
za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018 amewapongeza Wananchi na Viongozi katika
Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwa namna walivyoshirikiana katika ujenzi wa
Miundombinu ya Elimu katika Shule ya msingi Kilulu na akatoa wito wananchi
kwenda kujifunza ujenzi wa majengo mazuri yenye kiwango kwa gharama nafuu.
Aidha Mwenge wa Uhuru ukiwa katika
Halmashauri Mji wa Bariadi, pamoja na
kuweka Jiwe la Msingi la kiwanda cha ushonaji, umepitia miradi mingine katika
Sekta ya Elimu, Afya, Mazingira, Sekta Binafsi na Ujenzi.
MWISHO
Kiongozi wa Mbio za
Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo akiweka jiwe la Msingi
la Jengo/Kiwanda cha Ushonaji Mjini Bariadi, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru
katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Agosti 16, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya
ya Meatu, Mhe. Dkt. Joseph Chilongani katika makabidhiano Kijiji cha Gambasingu
Wilayani Itilima, Agosti 16, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga(kulia), Katibu Tawala Mkoa(kushoto) wakiwa pamoja
na baadhi ya Wakimbiza Mwenge Kitaifa mwaka 2018 na Paroko wa Parokia ya
Mtakatifu John mara baada ya Mwenge wa uhuru kuona msitu wa asili na mradi wa
maji.
Kiongozi wa Mbio za
Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo akifungua mabomba ya maji
ili kujiridha kama ni kweli yanatoka, kabla ya Kufungua mradi wa maji wa Gitoya
Mjini Bariadi, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Agosti 16, Bariadi.
Askari wa Kikosi cha
Kuzuia Ghasia(FFU) na baadhi ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, wakielekea
eneo la Mradi wa kufungua madarasa matatu katika Shule ya Msingi Kilulu Mjini
Bariadi, Agosti 16, 2018.
Mfanyabiashara wa
Mjini Bariadi, Bw. John Sabu na akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru mara baada ya
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo( wa
pili kushoto), kuweka Jiwe la Msingi la Hoteli yake ya SweetDream,(kulia)ni mtoto wao.
0 comments:
Post a Comment