Monday, August 27, 2018

DARASA LA SABA SIMIYU WAOMBA WASIMAMIZI WENYE TABIA YA KUWATISHA WATAHINIWA WAACHE


Wanafunzi wa darasa la saba shule za msingi za Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wamemuomba Mkuu wa Mkoa, Mhe Anthony Mtaka, kuwataka  wasimamizi wa Mtihani wa Taifa wenye tabia ya kuwatisha wanafunzi wakiwa katika chumba cha mtihani waache tabia hiyo ili wanafunzi wafanye Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba, mwaka 2018 kwa uhuru pasipo uoga.

Wanafunzi hao wametoa ombi hilo Agosti 27, 2018, wakati Mkuu Mkuu huyo wa Mkoa alipokutana na wanafunzi wa darasa la saba takribani 782 wa shule tano za msingi za Mjini BARIADI, katika Shule ya Msingi Sima B, lengo likiwa ni kuwahimiza kusoma kwa bidii katika siku chache zilizobakia na kuwatakiwa kila la heri katika mtihani wa Taifa utakaofanyika Septemba 05 na 06, 2018.

Wamesema kuwa wamepata taarifa kutoka kwa wenzao waliowatangulia kuwa siku za nyuma kulikuwa na baadhi ya wasimamizi wa Mtihani wa Darasa la Saba ambao walikuwa wakiwatisha na kuwanyanyasa watahiniwa, hivyo kuwafanya wanafunzi kufanya mtihani wakiwa na hofu jambo lililofanya baadhi yao kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao.

“ Miaka ya nyuma tunasikia kuna wasimamizi walikuwa wanawatishia sana wanafunzi, tunaomba  Mkuu wa mkoa utusaidie na sisi wasije wakatutishia tukashindwa kufanya mtihani wetu wa Taifa vizuri” alisema John Isack Mwanafunzi wa darasa la Saba Shule ya Msingi Sima A, Bariadi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewahakikishia wanafunzi hao kuwa hakutakuwa na vitisho wala manyanyaso yoyote kutoka kwa wasimamizi wa mitihani na akawaeleza kuwa atakutana na wasimamizi wa mitihani ambao wapo katika semina elekezi na  kuwapa angalizo hilo.

“Nikitoka hapa sasa hivi naenda kuongea na wasimamizi wa mitihani, niwahakikishie tu kwamba hamtatishwa msiwe na wasiwasi wowote, endeleeni kujisomea mjiandae vizuri na mtihani na mkiwa kwenye chumba cha mtihani mkawe watulivu na kumwomba Mungu awakumbushe yote mliyokuwa mnajisomea” alisema Mtaka.

Akizungumza na wasimamizi wa Mtihani wa Darasa la Saba, Mtaka amewataka wasimamizi hao ambao ni walimu kuwasimamia wanafunzi hao huku wakitambua kuwa wao ni walezi, hivyo wanapaswa kusimamia kwa kufuata taratibu zilizowekwa pasipo kuwatisha wala kuwanyanyasa watahiniwa.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameahidi kutoa zawadi ya shilingi milioni moja kwa mwanafunzi wa kiume, milioni moja na laki tano kwa mwanafunzi wa kike atakayekuwa miongoni mwa wanafunzi kumi bora Kitaifa katika Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2018 na shilingi milioni tatu kwa Shule ya Msingi ya Mkoa huo itakayokuwa miongoni mwa shule kumi bora Kitaifa.

Nao wanafunzi wa Darasa la Saba Mjini Bariadi wamemhakikishia mkuu wa mkoa kuwa watafanya vizuri katika Mtihani wa Taifa kwa kuwa wameandaliwa vizuri na walimu wao katika shule zao na katika kambi za Kitaaluma walizokaa kwa siku 21 mwezi Juni kujiandaa na mtihani huo.

“Tunakushukuru sana Mkuu wa Mkoa kwa kutuwezesha kuwa na kambi za kitaaluma, zimetusaidia kutuandaa na mtihani wa Taifa maana tulijifunza vitu vingi, tukapata maarifa mapya, sasa pia hivi walimu wetu wametuandaa vizuri tuko tayari kwa Mtihani wa Taifa, tunakuahidi tutafanya vizuri” alisema Hilda Mgalula Mwanafunzi wa darasa la saba Sima B.

Afisa Taaluma Mkoa wa Simiyu, Mwl. Onesmo Simime amesema jumla ya watahiniwa elfu 35 Mkoani Simiyu wanatarajia kufanya mtihani wa darasa la saba Septemba tano na sita, mwaka 2018.

MWISHO

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba Mjini Bariadi kwa lengo la kuwatakia kila la heri katika mitihani yao wanapojiandaa kuelekea kwenye Mtihani wa Taifa  wa Kumaliza Elimu ya Msingi utakaofanyika Septemba 05 na 06, 2018.
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba Mjini Bariadi wakinyosha mikono ili kujibu maswali waliyokuwa wakiulizwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) wakati akizungumza nao kwa lengo la kuwatakia kila la heri wanapojiandaa kuelekea kwenye Mtihani wa Taifa  wa Kumaliza Elimu ya Msingi utakaofanyika Septemba 05 na 06, 2018
John Isack mwanafunzi wa darasa la saba kutoka Shule ya Msingi SIMA A Mjini Bariadi akiwasilisha ombi lake kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) wakati akizungumza na waannfunzi wa darasa la saba wa Shule tano mjini Bariadi kwa lengo la kuwatakia kila la heri wanapojiandaa kuelekea kwenye Mtihani wa Taifa  wa Darasa la Saba utakaofanyika Septemba 05 na 06, 2018.
Mwalimu Aloyce Masejo kutoka Shule ya Msingi SIMA mjini Bariadi akizungumza na wanafunzi na baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba Mjini Bariadi ambao walikusanyika kuzzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) kwa lengo la kuwatakia kila la heri katikamitihani yao wanapojiandaa kuelekea kwenye Mtihani wa Taifa  wa Kumaliza Darasa la Saba utakaofanyika Septemba 05 na 06, 2018.
Afisa Taaluma Mkoa wa Simiyu, Mwl. Onesmo Simime akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba Mjini Bariadi kwa lengo la kuwatakia kila la heri katika mitihani yao wanapojiandaa kuelekea kwenye Mtihani wa Taifa  wa Kumaliza Elimu ya Msingi utakaofanyika Septemba 05 na 06, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba Mjini Bariadi kwa lengo la kuwatakia kila la heri katika mitihani yao wanapojiandaa kuelekea kwenye Mtihani wa Taifa  wa Darasa la Saba utakaofanyika Septemba 05 na 06, 2018.

Baadhi ya walimu ambao wasimamizi wa Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba Mkoani Simiyu  wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka  wakati alipozungumza nao wakiwa katika semina elekezi  Mjini Bariadi, kwa ajili ya maandalizi kuelekea katika usimamizi wa Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba utakaofanyika   Septemba 05 na 06, 2018.
Baadhi ya walimu ambao wasimamizi wa Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba Mkoani Simiyu  wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka  wakati alipozungumza nao wakiwa katika semina elekezi  Mjini Bariadi, kwa ajili ya maandalizi kuelekea katika usimamizi wa Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba utakaofanyika   Septemba 05 na 06, 2018.
Hanifa Makoti  mwanafunzi wa darasa la saba shule ya Msingi Bariadi, akizungumza jambo wakati wanafunzi wa shule tano za msingi mjini Bariadi walipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na kuzungumza nao kwa lengo la kuwatakia kila la heri katika mitihani yao wanapojiandaa kuelekea kwenye Mtihani wa Taifa  wa Darasa la Saba utakaofanyika Septemba 05 na 06, 2018.
Isack Sayi mwanafunzi wa darasa la saba shule ya Msingi Sima A,  akizungumza jambo wakati wanafunzi wa shule tano za msingi mjini Bariadi walipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka  na kuzungumza nao kwa lengo la kuwatakia kila la heri katika mitihani yao wanapojiandaa kuelekea kwenye Mtihani wa Taifa  wa Darasa la Saba utakaofanyika Septemba 05 na 06, 2018.
Mwalimu Janeth Kato kutoka Shule ya Msingi Bariadi mjini Bariadi akizungumza na wanafunzi na baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba Mjini Bariadi ambao walikusanyika kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) kwa lengo la kuwatakia kila la heri katikamitihani yao wanapojiandaa kuelekea kwenye Mtihani wa Taifa  wa Darasa la Saba utakaofanyika Septemba 05 na 06, 2018.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!