Jumla ya miradi 36 yenye thamani ya shilingi bilioni 8.4 iliyopo katika Halmashauri sita za Mkoa wa
Simiyu itapitiwa na Mwenge wa Uhuru ambao umeanza rasmi mbio zake mkoani humo,
Agosti 15, 2018.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka wakati akisoma salamu za mkoa wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru
katika Kijiji cha bukundi wilayani Meatu ukitokea wilaya ya Mkalama Mkoani
Singida Agosti 14, 2018.
Mtaka amesema kuwa miradi hiyo inayotarajiwa kupitiwa
na Mwenge wa Uhuru ni kutoka katika Idara ya Elimu, Afya, Maji, Viwanda,
Kilimo, Maliasili, Barabara,Utawala, Sekta binafsi na Vijana na Wanawake.
Akizungumzia Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 ambao
umejikita zaidi katika Elimu kwa kauli Mbiu “ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA; WEKEZA SASA KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU” amesema,
Elimu ni kipaumbele cha kwanza kwa mkoa huo, ambapo wameweka mikakati
mbalimbali ya kuinua elimu na ujenzi wa miundombinu ya elimu.
“ Simiyu ni mkoa pekee ambao wanafunzi wa madarasa ya
mitihani wanakaa katika kambi za kitaaluma, pia ufaulu wa wanafunzi wetu
umeongezeka mfano, mwaka 2017 mkoa wa Simiyu ulikuwa wa 26 Kitaifa kati ya
mikoa 31 lakini mwaka 2018 mkoa umeshika nafasi ya 10 katika matokeo ya kidato
cha Sita” alisema.
Aidha,
Mtaka amesema Simiyu inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu kwa kushirikisha
jamii na wadau mbalimbali ikiwa na mkakati wa kujenga shule tatu ambazo ni Shule
ya Sekondari ya Ufundi Simiyu, Shule ya Sekondari ya Wasichana na Shule ya
Sekondari ya Wavulana.
Hata
hivyo Mwenge wa Uhuru ukiwa wilayani Meatu umepita katika miradi mbalimbali ikiwa
ni pamoja na mradi wa vyumba vya madarasa katika shule shikizi ya Mwanyahina, Mradi
wenye majengo manne katika Hospitali ya Wilaya; (jengo la wodi ya wazazi, jengo
la upasuaji, maabara na nyumba ya mtumishi), mradi wa ujenzi wa mahakama ya
mwanzo Itinje na mradi wa ushonaji wa wanawake wa Kijiji cha Mwamishali.
Akizungumza
kwa nyakati tofauti katika miradi iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru, Kiongozi wa
Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho
amewataka viongozi na watendaji kusimamia miradi ya maendeleo kwa weledi na kuhakikisha
inatekelezwa kwa wakati kwa viwango
vinavyohitajika na kuzingatia thamani ya fedha(value for maoney) ili wananchi
wapate huduma
.
“Utawala
wa Awamu ya tano unataka watu wafanye kazi na kuwajibika kweli,tunaposema HAPA
KAZI TU Mhe. Rais anamaanisha, tukisimamia miradi kwa ulegelege hatutaweza
kufika, inawezekana hata kuchelewa kwa miradi ni kwa sababu watu wanataka
maslahi yao na kusababisha huduma za kijamii zinakwama ili wao wanufaike,
watendaji wa aina hiyo awamu ya tano hatuwahitaji” alisema Kabeho
Kwa
upande wake mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani akizungumza mara
baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kuweka jiwe la msingi
mradi wa madarasa ya shule shikizi ya Mwanyahina amesema Viongozi wa wilaya watasimamia
ujenzi wa mradi huo na kuhakikisha unajengwa kwa viwango na kwa wakati ili shule hiyo
iwanufaishe wananchi wa vijiji jirani vinavyoizunguka.
Mwenge wa
Uhuru umeanza mbio zake mkoani Simiyu katika Wilaya ya Meatu Agosti 14, 2018,
Agosti 15 utakuwa halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Agosti 16 Halmashauri ya
mji wa Bariadi, Agosti 17 Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Agosti 18
Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Agosti 19 Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na
tarehe Agosti 20, utakabidhiwa mkoani Shinyanga.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kulia) akipokea Mwenge wa Uhuru
kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi katika Kijiji cha
Bukundi wilayani Meatu, Agosti 14, 2018.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) akimkabidhi Mwenge wa
Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dkt. Joseph Chilongani mara baada ya
Mapokezi ya Mwenge wa Uhuru katika Kijiji cha Bukundi ukitokea Wilayani
Mkalama, mkoani Singida, Agosti 14, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho
akiondoka mara baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Vyumba vya madarasa
katika Shule shikizi ya Mwanyahina wilayani Meatu, Agosti 14, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho
akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya
Sekondari ya Bukundi,wilayani Meatu, Agosti 14, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho
akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka mara baada ya
makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na Mkuu wa Mkoa
wa Singida, katika Kijiji ca Bukundi, wilayani Meatu, Agosti 14, 2018.
Wananchi wa Wilaya ya Meatu jamii ya Wataturu wakitoa burudani kwa
wananchi wa Bukundi kabla ya makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru, kati ya Mkoa wa
Simiyu na Mkoa wa Singida katika Kijiji cha Bukundi wilayani humo, Agosti 14, 2018.
Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Issa Abass Mohamed kutoka
Kusini Pemba akisalimiana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne
Sagini mara baada ya kukabidhi rasmi kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu kutoka
Singida katika Kijiji cha Bukundi wilayani Meatu Agosti 14, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis
Kabeho(wa pili kulia) akishangilia pamoja na wakina mama wa kikundi cha
ushonaji Mwanyahina wilayani MEATU baada ya kuwafungulia mradi wao, Agosti 14, 2018.
0 comments:
Post a Comment