Thursday, August 2, 2018

DKT MWANJELWA APONGEZA SIMIYU KUJENGA JENGO LA KUDUMU UWANJA WA NANENANE, ASHAURI KANDA NYINGINE KUIGA


Naibu waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa kujenga Jengo la Kudumu (Simiyu Exhibition Hall), katika Uwanja wa Maonesho wa Nanenane wa Kanda ya Ziwa Mashariki na akashauri  kanda zote za Maonesho ya nanenane kuiga mfano kwa mkoa wa Simiyu,  ili wananchi waweze kupata elimu endelevu katika teknolojia za kilimo.

Mwanjelwa ameyasema hayo katika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi, wakati akikagua  jengo la maonesho la mkoa wa Simiyu ambalo limegharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 600 mpakakulikamilisha.

Aidha, amewapongeza viongozi wa mkoa wa Simiyu kwa jitihada za kuamua kujenga jengo hilo  katika Uwanja wa Nanenane ambalo litatumika kwa Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa, ambapo watu kutoka mataifa mbalimbali kuja kuonesha bidhaa na tekonlojia zitakazowasaidia wananchi kwenda kwenye uzalishaji wenye tija.

“ Mahali hapa patakuwa ni sehemu ya kuwainua wakulima na wananchi kwa ujumla ili kupata uzoefu wa kilimo, hii itapanua wigo na uelewa wa wakulima wetu wa Tanzani, lakini nichukue fursa hii kuziomba kanda nyingine kuiga mfano wa Simiyu wa kuwa na majengo ya kudumu ya maonesho, yatakayotumika kila baada ya muda fulani si nanenane tu” alisema.

Katika hatua nyingine Dkt. Mwanjelwa amewashauri viongozi wa Mkoa wa Simiyu kuona namna kuhamasisha wafanyabiashara kujenga hoteli maeneo ya jirani na jengo hilo ili kujiandaa na huduma kwa watu watakaokuwa wakifika kwa ajili ya maonesho hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa utaendelea kufanya maonesho ya Teknolojia mbalimbali kila baada ya miezi mitatu katika Jengo hilo,  ili kuwapunguza kazi Watanzania kwenda nje ya nchi kushuhudia maonesho hayo lakini pia kuvutia mataifa pengine kuja nchini kuonesha teknolojia  mbalimbali za kilimo.

“ Baada ya nanenane maeneo mengi shughuli za maonesho huwa zinasimama, sisi tumejipanga kufanya maonesho ya teknolojia mbalimbali hapa na ndiyo maana pamoja na kujenga jengo hilo tumeamua kuweka miundombinu kama umeme, maji, vyoo vya kudumu , JKT nao watajenga majengo yao ya kudumu na ulinzi wa jeshi la polisi utakuwa wa kudumu pia” alisema.

“ Matarajio yetu kama Wizara mtakubaliana na sisi tungehitaji kuwa na Simiyu Agri-Exhibition (Maonesho ya Kilimo Simiyu) kila baada ya miezi mitatu, tunataka hiki kinachofanyika kwenye nanenane kijirudie miezi mitatu ijayo, ili wananchi wetu wapate mahali pa kujifunza teknolojia za kilimo biashara, usindikaji na kuongeza thamani katika mazao ya kilimo” alisema Mtaka.

Ameongeza kuwa katika maonesho hayo wakulima watapata nafasi ya kuona zana bora za kilimo, hivyo akatoa wito kwa waonyeshaji wa teknolojia za kilimo kutambua kuwa baada ya Nanenane watapata fursaya kuonesha tena teknolojia hizo.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kulia) akiwaongoza Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa (wa tatu kulia) na viongozi wengine mara baada ya kukagua Jengo la Maonesho la Mkoa( Simiyu Exhibition Hall), katika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi Agosti 02, 2018.
Kutoka kushoto Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Jumanne Sagini, Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakifurahia jambo mara baada ya kukagua Jengo la Maonesho la Mkoa (Simiyu Exhibition Hall), katika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi Agosti 02, 2018.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akitoa maelezo ya Jengo la Maonesho la Mkoa( Simiyu Exhibition Hall), kwa Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa mara baada ya kukagua jengo hilo katika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi Agosti 02, 2018.
Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa akikagua baadhi ya bidhaa za wajasiriamali katika mabanda ya maonesho ya Mkoa wa Mara, katika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi Agosti 02, 2018
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) na Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa wakiwa katika picha ya pamoja na binti aliyevaa vazi la kabila la Wataturu, baada ya viongozi kutembelea mabanda ya maonesho ya Mkoa wa Mara, katika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi Agosti 02, 2018.

Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa akijaribu kutumia mashine ya kupukuchua mahindi wakati alipotembelea banda la maonesho la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu mkoa wa Shinyanga, katika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi Agosti 02, 2018.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu (kulia), Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja mama na binti yake aliyevaa vazi la kabila la Wataturu, baada ya viongozi kutembelea mabanda ya maonesho ya Mkoa wa Mara, katika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi Bariadi Agosti 02, 2018

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!