Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu- Simiyu
Co-Operative Union (SIMCU) kimefanya Uchaguzi wa Viongozi wa Chama hicho, ikiwa
ni kwa mara ya kwanza kwa Chama hicho kufanya Mkutano wake Mkuu, tangu
kuanzishwa kwake baada ya Simiyu kujitoa Uanachama kwenye Vyama vya Ushirika vya NYANZA
na SHIRECU.
Katika Mkutano huo uliofanyika Mjini Bariadi Septemba 04, 2018, Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amewataka viongozi waliochaguliwa kuendesha
ushirika wa kisasa ambao utakuwa wa tofauti huku akihimiza SIMCU kuwekeza
katika maendeleo ya elimu, afya na ujenzi wa vitega uchumi.
“Viongozi vaeni mawazo ya kisasa muendeshe Ushirika kisasa,
ningependa kuona Chama chetu cha Ushirika cha mkoa(SIMCU) kinajipambanua kwenye
maendeleo hasa elimu na afya; wekezeni katika kujenga vitega uchumi, haiwezekani
mkusanye zaidi ya bilioni moja kutokana pamba kwenye AMCOS halafu mkashindwa
kujenga vitega uchumi” alisema Mtaka.
Naye
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Titus Kamani amewaasa
viongozi wa SIMCU pamoja na vongozi wa Vyama vya Ushirika vya msingi (AMCOS)
kusimamia ushirika mkoani humo kwa uadilifu na kuiacha historia ya zamani
ambayo baadhi ya viongozi walichukulia ushirika kama mahali pa kupiga dili na
mali isiyo na mwenyewe.
Mwenyekiti
wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu(SIMCU), Bw. Charles Madata, amesema atahakikisha
SIMCU inafanya mambo ya maendeleo kama Mkuu wa Mkoa huo alivyosema, ikiwa ni
pamoja na kuwekeza katika elimu, afya, kujenga vitega uchumi na kusimamia Vyama
vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) ili vijiendeshe kibiashara.
Aidha,
Madata amebainisha mikakati yake mingine kuwa ni kusimamia nidhamu ya matumizi
ya fedha na mali za Ushirika, kutafuta
soko la pamba ndani na nje, ili bei ya pamba iweze kupanda na kufikia zaidi ya
shilingi 1500/= na kuwahamasisha wakulima kujiunga na ushirika ili kuboresha
maisha yao.
Nao
wanachama wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) ambavyo ndivyo vinavyounda
Chama cha Ushirika cha Mkoa(SIMCU) wamesema, wana matumaini makubwa na Chama hicho na
wanaamini kitawasaidia katika kuboresha bei ya zao la pamba, kama ilivyoanza
kuonekana katika baadhi ya AMCOS wakati wa msimu wa mwaka 2018.
“Tunaimani
SIMCU itatusaidia kuimarisha bei ya pamba , mwaka huu bei elekezi ilikuwa
1100/= lakini kupitia mpango wa wenye makampuni kununua kupitia AMCOS baadhi ya
maeneo bei iliongezeka ikafikia 1250/=, tunajua viongozi watasimamia tutapata
bei nzuri na wakulima tutanufaika kupitia ushirika” alisema Magima Mageme
mwanachama kutoa Itilima
“Ushirika
ukisimamiwa vizuri unawasaidia wakulima mambo mengi, mwaka huu wakulima
walikuwa wanapewa hela zao cash(taslimu) na wanunuzi wa pamba wa makampuni
maana hela zote zilikuwa zinaletwa kwenye AMCOS, viongozi wetu tuliowachagua
leo watusaidie kusimamia ushirika vizuri” alisema Nkumbamboi Mchunga wa
Budalabujiga.
Naye
Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Ibrahim Kadudu, amesema Chama Kikuu cha
Ushirika Mkoa wa Simiyu(SIMCU), kitakuwa na wanachama (Vyama vya Ushirika vya
msingi (AMCOS) 379, huku akibainisha kuwa AMCOS hizo hadi sasa zimezalisha
takribani kilo milioni 100.4 za zao la pamba.
Bw.
Kadudu amesema kutokana na uzalishaji huo wa kilo milioni 100.4 za zao la pamba
AMCOS zimepata bilioni 3.3 kutokana na ushuru ambao AMCOS inapata shilingi 33/=
kwa kila kilo moja ya pamba na Chama cha Ushirika cha Mkoa (SIMCU) kitapokea
shilingi Bilioni moja na milioni 40 kutokana na ushuru wa shilingi 10/= katika kila
kilo moja ya pamba.
Viongozi wa SIMCU waliochaguliwa ni pamoja na
Charles Madata(Mwenyekiti), wajumbe wngine ni Mabula Bwire, Emmanuel Mboi,
Simon Magoma, Kulwa Bupuma, Filimoni Sambe na Tuma Magagi.
MWISHO
Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wanachama wa Chama Kikuu cha
Ushirika cha Mkoa huo(SIMCU) katika Mkutano Mkuu wa kwanza, kwa lengo la
kuchagua viongozi wa Chama uliofanyika Septemba 04, 2018 Mjini Bariadi, (wa
tatu kushoto) Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Titus Kamani na
wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu(SIMCU), Bw. Charles
Madata .
Baadhi ya wanachama wa
Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU) wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa Chama Kikuu cha
Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU), uliofanyika Septemba 04, 2018 Mjini Bariadi
kwa lengo la kupata viongozi wa chama hicho.
Mwenyekiti wa Tume ya
Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Titus Kamani (kulia) akiteta jambo na Mrajisi
Msaidizi wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Ibrahim Kadudu (katikati) mara baada ya Mkutano
Mkuu wa kwanza wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU), uliofanyika
Septemba 04, 2018 Mjini Bariadi kwa lengo la kupata viongozi wa chama hicho.
Baadhi ya wanachama wa
Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU) wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa Chama Kikuu cha
Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU), uliofanyika Septemba 04, 2018 Mjini Bariadi
kwa lengo la kupata viongozi wa chama hicho.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama
vya Ushirika Mkoa wa Simiyu, Bw. Ibrahim Kadudu (kulia) akipokea maelekezo
kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Anthony Mtaka, katika Mkutano Mkuu wa kwanza
wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU), uliofanyika Septemba 04,
2018 Mjini Bariadi kwa lengo la kupata viongozi wa chama hicho.
0 comments:
Post a Comment