Friday, September 28, 2018

RC MTAKA APONGEZA GEITA KWA UBUNIFU KUFANYA MAONESHO YA KIPEKEE YA DHAHABU NCHINI


Mkuu wa Mkoa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi. Robert  Gabriel kwa ubunifu waliofanya wa kufanya Maonesho ya Kipekee ya Teknolojia Bora ya  dhahabu hapa nchini.

Mtaka ameyasema hayo mara baada ya kuzungumza na viongozi wa Mkoa wa Geita na kutembelea mabanda ya maonesho katika Maonesho ya Dhahabu yanayofanyika  Uwanja wa CCM Kalangalala Mjini Geita kuanzia Septemba 24, 2018.

Amesema Watanzania wengi wamekuwa wakienda kushiriki maonesho ya dhahabu katika mataifa mbalimbali barani Afrika na nje ya bara la Afrika lakini kupitia maonesho haya Watanzania wameanza kujionea teknolojia mbalimbali za uchimbaji wa madini hapa nchini.

“ Ninawapongeza sana viongozi wa Geita kwa kuandaa maonesho haya ya kipekee hapa nchini, tumekuwa na shughuli nyingi sana za uchimbaji madini lakini sisi sote ni mashahidi shughuli hizi tumekuwa tukiziona wakati wa Mei Mosi kupitia kile chama kinachohusisha watu wanaofanya kazi za madini, hatujapata jambo linaloonesha shughuli za migodini na mazao yanayotokana na migodi kama dhahabu” alisema Mtaka.

Ameongeza kuwa ubunifu huo uliofanywa na Viongozi wa Mkoa wa Geita hasa wa kuyapa maonesho haya jina la Kiswahili ya “Maonesho ya Dhahabu” ambalo linasadifu shughuli zinazofanyika katika mkoa huo ambao ni mzalishaji mkubwa wa dhahabu, utachangia kuongeza watalii na wageni wengi watakaokuja hapa nchini kupitia maonesho hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi. Robert Gabriel ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kushuhudia maonesho hayo ili kujionea teknolojia za uchimbaji madini, kupata huduma za kifedha katika taasisi za kifedha, kupata huduma na elimu juu ya utatuzi wa changamoto za kibiashara hususani upatikanaji wa mitaji na changamoto za uchimbaji katika kliniki ya biashara.

Aidha, Mhandisi. Gabriel amesema maendeleo katika mkoa wa Geita hayaepukiki kutokana na sekta ya madini kuwa na  mchango mkubwa katika uchumi ambapo amebainisha kuwa kupitia uchimbaji dhahabu mkoa unapata ushuru, fedha za msaada kwa jamii (Corporate  Social Responsibility) kutoka kwenye makampuni yanajihusisha na uchimbaji madini zilizosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Mhe. Leonald Bugomola amesema maonesho ya dhahabu mwaka 2019 yataanza mapema na Halmashauri yake kama mwenyeji wa maonyesho hayo imejipanga kutafuta eneo kubwa zaidi ekari 100 ,  kwa kuwa mpango wa mkoa ni kuwa na maonesho yenye hadhi ya Kimataifa yatakoshirikisha washiriki wengi ikilinganishwa na mwaka huu.

Nao baadhi ya wachimbaji wadogo wameshukuru uanzishwaji wa maonesho hayo ambayo yatasaidia kupata utaalamu juu teknolojia mbalimbali zinazotumika kuchimba madini na kupata elimu ya namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika sekta ya madini kutokana na wadau mbalimbali kukutanishwa pamoja na kujadiliana kuhusu maendeleo ya sekta ya madini.

Maonesho ya Teknolojia Bora  ya Dhahabu mkoani Geita yameanza Septemba 24, 2018 na yanatarajiwa kuhitimishwa Septemba 30, 2018 yakiwa na Kauli Mbiu: TEKNOLIJIA BORA YA UZALISHAJI WA DHAHABU KWA MAENDELEO YA KIJAMII NA UCHUMI WA VIWANDA”
MWISHO.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (katikati) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi. Robert  Gabriel(kulia) wakati alipofika Mjini Geita kujionea Maonesho ya Dhahabu yanayofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mjini Geita, kuanzia Septemba 24 hadi Septemba 30, 2018.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi. Robert  Gabriel(kulia) wakifuatilia masuala mbalimbali yalikuwa yakiwasilishwa na wadau wa sekta ya madini katika kikao kilichofanyika Uwanja wa CCM Kalangalala Mjini Geita, kwenye Maonesho ya  Dhahabu kuanzia Septemba 24 hadi Septemba 30, 2018. 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akisaini kitabu cha wageni katika banda la Kampuni ya NGM Gold Mine inayomilikiwa na Bw. Gungu Silanga ambaye ni mkazi wa Simiyu wakati alipofika Mkoani  Geita Mjini Geita kujionea Maonesho ya Dhahabu yanayofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mjini Geita, kuanzia Septemba 24 hadi Septemba 30, 2018. 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akisalimiana na Mbunge wa Geita Mjini Mhe. Constantine Kanyasu mara baada ya kuwasili Mkoani Geita, kujionea Maonesho ya Dhahabu yanayofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mjini Geita, kuanzia Septemba 24 hadi Septemba 30, 2018.




 Baadhi ya Viongozi na wadau wa Madini wakifuatilia kikao kilichofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kalangalala Mjini Geita, wakati wa  Maonesho ya  Dhahabu yanayofanyika kuanzia Septemba 24 hadi Septemba 30, 2018. 


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony akiangalia bidhaa za Wajasiriamali katika Maonesho ya Dhahabu yanayofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mjini Geita, kuanzia Septemba 24 hadi Septemba 30, 2018.
Baadhi ya wananchi wa Mji wa Geita wakiangalia teknolojia mbalimbali zinazotumika katika uchimbaji wa dhahabu, katika Maonesho ya Dhahabu yanayofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mjini Geita, kuanzia Septemba 24 hadi Septemba 30, 2018.
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi. Robert  Gabriel  wakitoka katika Banda la Maonesho la Mamlaka ya Mapato Tazania (TRA), katika Maonesho ya Dhahabu yanayofanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mjini Geita, kuanzia Septemba 24 hadi Septemba 30, 2018. 

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!