Saturday, September 29, 2018

SIMIYU YADHAMIRIA KUWAKOMBOA WAFUGAJI KWA KUWASAIDIA WAFUGE KISASA

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.  Anthony Mtaka amewataka wataalamu wa mifugo na kilimo kuachana na utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea huku akiwataka kuongeza ubunifu sambamba na kupanua wigo wa kutoa elimu kwa wafugaji ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo ambayo ni ya pili katika kuchangia pato la mkoa.


Mtaka ametoa kauli hiyo wakati akifungua warsha ya kujadili maendeleo ya sekta ya mifugo na mnyororo wake wa thamani iliyofanyika mjini Bariadi na kusema kuwa baada ya warsha hiyo anategemea kuwaona maafisa ugani na wataalamu wa mifugo wakiwaelimisha zaidi wafugaji mbinu bora za ufugaji wa kisasa ambazo zitabadili sura ya mkoa huo.

“ Hivi kwa nini tunakuwa watu wa kusifia nchi nyingine badala ya kujipanga ili na sisi hatimaye tuweze kuwa kama wao, utasikia mtu anasema ukitaka kujifunza mbinu bora za ufugaji nenda Ethiopia au Botswana, hivi sisi tunashindwa nini kuwa kama wao”, alihoji Mtaka.

Akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu kwa wafugaji Mtaka  amewasisitiza wataalamu wa mifugo katika halmashauri  zote za wilaya mkoani Simiyu kuhakikisha wanatumia ubunifu wao kadiri iwezekanavyo kuwajengea uwezo wafugaji ili waweze kunufaika na sekta hiyo halikadhalika waweze kuchangia katika ukuaji wa sekta ya viwanda vitakavyohitaji malighafi zinazotokana na mifugo.

Kwa upande wake mwakilishi wa balozi wa Ireland ambaye ni mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Ubalozi huo Dkt. Niall Moris amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika suala zima la kuwajengea uwezo wataalamu wa mifugo mkoani Simiyu ili na wao wawe chachu ya kuisambaza elimu na ujuzi huo kwa wafugaji.

Dkt. Niall ameongeza kuwa serikali ya Ireland imevutiwa kushirikiana na mkoa wa Simiyu kutokana na mipango yake mizuri na sera zenye mwelekeo unaotia matumaini ya kumkomboa mfugaji na kuongeza kuwa hiyo ndio njia pekee itakayosaidia kuleta mapinduzi katika sekta ya mifugo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa tume ya Sayansi na teknolojia Dkt. George Mulamula amesema mabadiliko katika sekta ya mifugo yatasaidia kuleta msukumo katika sekta ya viwanda mkoani Simiyu na kusisitiza kuwa ongezeko la malighafi zitokanazo na mifugo zitaongeza msukumo kwa serikali na wadau wa maendeleo kufungua viwanda vingi zaidi.
 MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akizungumza na Watalaam kutoka kwa Ireland wakati walipofika ofisini kwake kabla ya kufanya warsha ya kujadili maendeleo ya sekta ya mifugo na mnyororo wake wa thamani iliyofanyika mjini Bariadi.

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!